Sura ya Al-Ahzab, aya ya 26-31 (Darsa ya 750)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 26-31 (Darsa ya 750)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 750 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 26 na 27 ambazo zinasema:
وَأَنزَلَ الَّذِينَ ظَاهَرُوهُم مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ مِن صَيَاصِيهِمْ وَقَذَفَ فِي قُلُوبِهِمُ الرُّعْبَ فَرِيقًا تَقْتُلُونَ وَتَأْسِرُونَ فَرِيقًا
Na akawateremsha wale walio wasaidia (maadui) katika Watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao. Baadhi yao mkawa mnawauwa, na wengine mnawateka.
وَأَوْرَثَكُمْ أَرْضَهُمْ وَدِيَارَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ وَأَرْضًا لَّمْ تَطَئُوهَا ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرًا
Na akakurithisheni ardhi zao na nyumba zao na mali zao, na ardhi msiyo pata kuikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Kwa mujibu wa mapokeo ya historia, katika mji wa Madina walikuwa wakiishi watu wa makabila matatu ya kaumu ya Mayahudi ya Bani Qainuqa'a, Bani Nadhiir na Bani Quraidhah, ambapo kila kabila lilifungiana mkataba na Waislamu wa kuishi kwa amani na masikilizano. Makabila ya Bani Qainuqa'a na Bani Nadhiir yalivunja makubaliano hayo katika mwaka wa pili na wa nne hijria kwa utaratibu na kula njama dhidi ya Waislamu; na matokeo yake wakatimuliwa na kutolewa nje ya mji wa Madina. Lakini watu wa kabila la Bani Quraidhah ambao waliendelea kuishi mjini humo, katika mwaka wa tano hijria na wakati wa vita vya Ahzab waliungana pamoja na washirikina wa Makka na baadhi ya makabila ya kandokando mwa mji wa Madina. Katika vita hivyo washirikina walioungana na Bani Quraidhah walishindwa; na Mayahudi hao ikawabidi wakimbilie kwenye ngome zao ili kujihami na kujilinda. Katika hali na mazingira hayo, Bwana Mtume Muhammad SAW akaamriwa na Mwenyezi Mungu achukue hatua ya kuwatokomeza moja kwa moja wavunja ahadi na wakiukaji hao wa makubaliano. Kwa ajili ya hilo Waislamu wakaizingira ngome ya Mayahudi wa Bani Quraidhah na baada ya siku kadhaa wakaingia ndani yake. Katika tukio hilo baadhi ya Mayahudi hao waliojaribu kubariziana na Waislamu waliuawa lakini wengi wao walisalimu amri na kuweka chini silaha zao. Matokeo ya vita hivyo yalikuwa ni kufukuzwa na kutolewa nje ya mji wa Madina Mayahudi wavunja ahadi na makubaliano. Kwa upande wa kiuchumi, vita hivyo vilikuwa na ngawira na ghanima nyingi mno kwa Waislamu zikiwemo konde na ardhi za kilimo zilizogawanywa baina yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Uislamu unausia kuishi kwa amani na masikilizano na wasio Waislamu, tab'an ikiwa watu hao pia wataishi kwa usalama na amani na Waislamu; na si kushirikiana na maadui wa Uislamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusiregee wala tusiyumbishwe na silaha kubwa kubwa na zana za kisasa za adui, kwa sababu wakati mwengine, Mwenyezi Mungu huzitia hofu na kiwewe nyoyo za maadui na kutuwezesha kupata ushindi dhidi yao. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika upangaji wa masuala ya jamii ya Kiislamu, mbali na mahesabu ya kimaada tuweke nafasi pia ya kutarajia kupata auni na msaada wa ghaibu wa Mwenyezi Mungu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 28 na 29 ambazo zinasema:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا
Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri.
وَإِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا
Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa.
Baada ya aya kadhaa za sura hii ya Ahzab kuzungumzia habari za vita vya Ahzab, aya tulizosoma hivi punde zinarejea tena kwenye maudhui ya aya za mwanzoni mwa sura hii kuhusu wake wa Bwana Mtume Muhammad SAW na kuwahutubu kwamba: Nyinyi wake wa Mtume, mnapaswa kama alivyo mtukufu huyo muwe mfano mzuri wa kuigwa na wake na mabinti wa Waislamu. Na si kuwa na matarajio ya kuwa kama walivyo wake wa wafalme, wenye kila aina ya vito vya dhahabu, mapambo ya kidunia, nguo za thamani ya juu na nyumba za fahari.
Alaa kulli hal, ili kulinda nafasi ya Bwana Mtume SAW, ambaye Mwenyezi Mungu amemfanya kuwa ruwaza ya kufuatwa na mfano wa kuigwa na Waislamu wote inabidi mas-ulia na jukumu lake la Utume lipewe kipaumbele na umuhimu zaidi kuliko jambo jengine lolote. Kwa sababu hiyo ilipasa awatangazie wake zake kwamba kama mnataraji kuwa, kwa vile nyinyi ni wake wa Mtume inapasa muwe na maisha mazuri na ya juu zaidi kuliko watu wengine katika jamii, hamtokidhiwa matarajio hayo na ni aula mtengane na mimi. Lakini kama mko tayari kuishi maisha ya kawaida kama walivyo wanawake wengine wa Kiislamu na kuwa tayari kuvumilia shida na tabu za dunia kwa ajili ya Allah, na kufanya mambo mema na ya kheri kila inapolazimu, basi Yeye Mola atakupeni malipo makubwa ya thawabu Siku ya Kiyama. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba haifai familia za viongozi katika mfumo na utawala wa Kiislamu kuishi maisha ya kitajiri na ya kifahari. Macho ya watu wa kawaida katika jamii huwa muda wote yanawafuatilia viongozi na watu walio karibu nao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kiongozi wa jamii ya Kiislamu anatakiwa asijisahau, akaghafilika na nafasi na wadhifa alionao kwa kuathiriwa, kwa sababu mbalimbali, na matakwa yasiyostahiki ya aila na watu wa familia yake. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika utamaduni wa Kiislamu, matakwa ya mke au mume kwa mwenzake yasikinzane na mafundisho na maamrisho ya dini. Mke au mume halazimiki kutekeleza na kumtimizia mwenzake haja na matakwa ya aina hiyo.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 30 na 31 ambazo zinasema:
ا نِسَاءَ النَّبِيِّ مَن يَأْتِ مِنكُنَّ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ يُضَاعَفْ لَهَا الْعَذَابُ ضِعْفَيْنِ ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا
Enyi wake wa Nabii! Atakaye fanya uchafu dhaahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
وَمَن يَقْنُتْ مِنكُنَّ لِلَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتَعْمَلْ صَالِحًا نُّؤْتِهَا أَجْرَهَا مَرَّتَيْنِ وَأَعْتَدْنَا لَهَا رِزْقًا كَرِيمًا
Na miongoni mwenu atakeye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akatenda mema, tutampa malipo yake mara mbili, na tutamwandalia riziki ya ukarimu.
Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusu nafasi ya wake wa Bwana Mtume SAW na kuwa kigezo na mfano katika jamii na kueleza kwamba: Kwa kuwa matendo yenu mema na mabaya yanafuatiliwa na kuonekana mbele ya macho ya Waislamu wengine hasa Waislamu wanawake, yana taathira kubwa katika kuenea matendo mema na mabaya katika jamii. Kwa hivyo, malipo ya thawabu na adhabu ya amali na matendo muyafanyayo si sawa na ya watu wa kawaida. Na sababu ni kuwa kwa upande mmoja nyinyi mnaishi ndani ya Nyumba ya wahyi na mna ufahamu na uelewa wa hukumu za dini; na kwa upande mwengine matendo yenu nyinyi ni kigezo cha kufuatwa na mfano wa kuigwa na wanawake wengine. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kiwango cha malipo ya thawabu na adhabu anayolipwa mja na Mola kinazingatia uelewa wa mtu kwa jema na baya aliliotenda na pia taathira ya jema na baya hilo ndani ya jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika mfumo wa sharia wa Allah, uhusiano wa nasaba na wa ujamaa anaokuwa nao mtu na viongozi wa dini akiwemo hata Mtume mwenyewe haumfanyi mtu huyo awe na haki maalumu, bali hata adhabu anayopewa kwa kosa analofanya huwa maradufu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba makosa na madhambi yanayofanywa na watu wakubwa yana tofauti na watu wa kawaida. Kwa maneno mengine, baadhi ya wakati dhambi yao ndogo huwa kubwa zaidi ya dhambi kubwa inayofanywa na watu wa kawaida. Kwa hivyo athari za makosa yao huwa kubwa zaidi kuliko za watu wengine. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 750 ya Quráni imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na atupe mema akhera na atulinde na adhabu ya Moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.