Sura ya Al-Ahzab, aya ya 32-34 (Darsa ya 751)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 32-34 (Darsa ya 751)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 751 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 32 ambayo inasema:
يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاءِ ۚ إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا
Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia wake wa Bwana Mtume Muhammad SAW ambazo zilionyesha nafasi yao yenye taathira kwa watu. Aya hii ya 32 ya Suratul Ahzab inabainisha suala hilo kwa uwazi kabisa na kueleza kwamba wake wa Mtume wana jukumu na mas-ulia mazito kutokana na uhusiano wao na yeye Bwana Mtume SAW na wala haipasi wao kujilinganisha na wanawake wengine. Kwa sababu watake wasitake, wao ni kigezo na mfano wa kuigwa na wanawake wengine katika jamii; na matendo yao mema na mabaya yana taathira ndani ya jamii. Kisha aya inaashiria moja ya vielelezo na mifano hai ya mienendo ya kijamii ya wanawake na kueleza kwamba: Katika mambo ya kukufanyeni muwe na taqwa na uchaMungu ni kwamba mnapozungumza na watu ambao si maharimu zenu, sauti na lahani zenu zisiwe za namna ya kuwatia tamaa wanaume wachafu na wenye maradhi ya nyoyo; bali zungumzeni kwa lahani inayotakiwa na inayostahiki kwa wanawake wasafi na wanaojistahi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba nyadhifa na hadhi za watu zina taathira katika kiwango cha mas-ulia waliyonayo. Kwa sababu hiyo, watu wenye hadhi za juu zaidi kijamii au kiukoo (kama koo na familia za viongozi wa kidini) wanatakiwa wajichunge zaidi kuliko watu wengine katika maneno na mienendo yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika kila jamii kuna watu wachafu na wenye maradhi ya nyoyo. Kwa sababu hiyo ili kujilinda na watu kama hao, wanawake wanatakiwa wajichunge katika mazungumzo na milahaka na miamala yao ya kijamii.
Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 33 na 34 ambazo zinasema:
وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا
Na kaeni majumbani kwenu, wala msidhihirishe mapambo kwa madhihirisho ya kijahilia ya kizamani. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika si mengineyo, Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni kabisa kabisa.
وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَىٰ فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ وَالْحِكْمَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ لَطِيفًا خَبِيرًا
Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Mwenyezi Mungu na hikima. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri, na Mwenye khabari.
Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia na kuwahutubu tena wake wa Bwana Mtume SAW kwamba: Kinyume na zama za kabla ya Uislamu ambapo wanawake walikuwa wakitembea katika jamii wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya staha na kujiremba kwa kila aina ya vito na mapambo, nyinyi wanawake waumini msitoke toke ovyo majumbani mwenu bila ya jambo la dharura. Na kama utakuwepo ulazima wa kushiriki kwenye hadhara na harakati za kijamii basi fanyeni hivyo mkiwa mumejisitiri kwa mavazi ya heshima na yanayostahiki kisheria, na jiepusheni kuonyesha maungo na mapambo yenu. Taabiri iliyotumiwa na Quráni katika aya hii ni ujahilia wa kizamani. Utadhani Kitabu hicho cha mbinguni kilikuwa kimeshatabiri kama kuna ujahilia mwengine ambao uko njiani unakuja ambapo vitendo vya kujiremba na kujipodoa na kujianika majiani vitazagaa na kuenea baina ya wanawake katika jamii. Suala ambalo linatekelezwa leo hii kwa propaganda kubwa na kwa majina mbalimbali ili kuwaweka utupu na kuwaendesha uchi wanawake, kiasi kwamba soko la vipodozi limekuwa moja ya masoko makubwa zaidi ya biashara duniani. Kisha aya zinaendelea kwa kukumbushia umuhimu wa kuzingatia mno wajibu na faradhi za dini kama Sala, Zaka na maamrisho mengine ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili isije ikadhaniwa kwamba kushika dini kwa wanawake kunahusu suala la mavazi tu na kujiepusha kuchanganyika na wanaume wasio maharimu zao. Au isije ikadhaniwa pia kwamba maamrisho yaliyotangulia yanawahusu wake wa Mtume tu peke yao lakini wanawake wengine hawalazimiki kuyachunga na kuyafuata.
Katika kuendelea kuzungumzia maamrisho hayo ya Allah, aya ya 34 inawahutubu wanawake kwamba: Kuwepo majumbani, ambalo ni jambo la kawaida kwa wanawake kusiwe kizuizi kwao cha kujijenga na kutukuka kimaanawi, bali wanapaswa kila mara wajishughulishe na usomaji Quráni na kujifunza mafundisho yake matukufu yaliyotukuka na ya hekima; na wala wasighafilike na jambo hilo.
Lakini katikati ya miongozo na maamrisho hayo, ambayo kwanza yaliwahutubu wake wa Mtume na mwishowe wanawake wote waumini, imekuja ibara ya maneno ambayo kinahau ni ya dhamiri ya kiume na hivyo kujipambanua na ibara za kabla na baada yake. Ibara na kifungu hicho cha maneno ambacho kimeanza na neno "Innamaa" inaonyesha kuwa irada ya Allah SW imehukumu "Ahlul-Bayt" wa Bwana Mtume Muhammad SAW wawe na Umaasumu maalumu; umaasumu ambao unawalinda wao na kila aina ya uovu na uchafu ili waweze kuwa kigezo na mfano wa kuigwa na kufuatwa na waumini wote. Umaasumu huo si wa namna ya ulazimishaji kiasi cha kuwafanya Ahlul-Bayt wasiwe na uwezo wa kufanya dhambi. La hasha, ila ni kwamba kutokana na amali na matendo yao matukufu wamekuwa na ustahiki wa kupata fadhila hizo maalumu za Allah, kwamba licha ya kuwa na uwezo na hiyari ya kuweza kufanya dhambi lakini hawaliendei tendo lolote ovu na wanabaki kuwa maasumu, yaani watu wasiofanya dhambi ya aina yoyote. Tabán kwamba muradi na makusudio ya hao "Ahlul-Bayt" ni watu gani, kuna tofauti za maoni baina ya wafasiri. Baadhi yao wametabikisha na kuhusisha ibara ya Ahlul-Bayt na wake wa Mtume, na baadhi yao, kwa kutegemea Hadithi kadha wa kadha zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume SAW kuhusiana na maudhui hiyo, wanaitakidi kuwa sehemu ya aya hii na ibara hii inawahusu watu watano tu ambao ni yeye mwenyewe Bwana Mtume Muhammad SAW, binti yake Fatimah, mkwe wake Ali bin Abi Talib na wajukuu zake wawli Hassan na Hussein. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kujiremba na kujionyesha wanawake katika hadhara na michanganyiko ya kijamii si alama ya ustaarabu, bali kwa mujibu wa Quráni ni nembo ya ujahilia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ulazima wa kutoa Zaka na kutumia sehemu ya mali yake mtu kuwasaidia wanyonge na wahitaji, hakuwahusu wanaume peke yao bali kunajumuisha wanawake pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba familia ya viongozi wa dini ambao wana jukumu la kuongoza jamii inapaswa kujiweka mbali na matendo maovu na machafu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa wanawake ambao ni mama wa nyumbani wasiofanya kazi nje ya majumba yao hawatakiwi kubaki nyuma katika masuala ya kutafuta elimu na kujiongezea maarifa ya kidini. Wawe na hima na bidii ya kujiinua na kujijenga kielimu na kimaanawi. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 751 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.