Sep 06, 2017 02:48 UTC

Sura ya Al-Ahzab, aya ya 35-38 (Darsa ya 752)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 752 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 35 ambayo inasema:

 إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا 

Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wakweli wanaume na wakweli wanawake, na wanaume wanao subiri na wanawake wanaosubiri, na wanyenyekevu wanaume na wanyenyekevu wanawake, na watoao sadaka wanaume na watoao sadaka wanawake, na wanaume wanao funga na wanawake wanaofunga, na wanaume wanao jihifadhi tupu zao na wanawake wanao jihifadhi tupu zao, na wanaume wanao mkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi na wanawake wanao mkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi- Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia amri ya Allah kwa wake wa Bwana Mtume Muhammad SAW na Waislamu wote wanawake ya kujihifadhi na kujiepusha na wanaume wachafu na wasio na staha. Aya hii ya 35 inazungumzia sifa za mtu aliyekamilika, awe mwanamme au mwanamke katika hali tofauti za kiimani na kiitikadi, na kitabia na kiakhlaqi na kuinasibisha moja moja kati ya sifa hizo kwa jinsia zote mbili ili kuonyesha wazi kwamba hakuna tofauti yoyote baina ya mwanamke na mwanamme katika kufikia ukamilifu wa kiutu na kimaanawi. Hayo ni pamoja na masuala kama imani juu ya Allah, kudhibiti ulimi, tumbo na matamanio, kuwahudumia na kuwasaidia wahitaji, kuwa na subira na uvumilivu wakati wa masaibu na matatizo, kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kuomba dua na kufanya munajati, kunong’ona na Mola n.k. Kinyume na wanavyodhani baadhi ya watu, imani ya mtu haihusiani na Sala na Saumu tu. Na ndiyo maana katika aya hii, sambamba na utekelezaji wa faradhi za dini yameashiriwa pia mambo kama subira, ukweli na unyenyekevu ambavyo ni vielelezo na madhihirisho ya sifa za kitabia na kimatendo za Muislamu wa kweli. Kwa hivyo kama mtu atakuwa dhaifu katika kupambika na sifa hizo, hiyo itakuwa ishara ya kuwa dhaifu kiimani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba tofauti zilizopo baina ya mwanamme na mwanamke zinahusiana na jinsia zao, wakati ukamilifu wa mtu unahusiana na roho yake, ambapo katika hili hakuna tofauti yoyote kati ya mwanamke na mwanamme. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mtu kwa mtazamo wa Uislamu ni kiumbe aliyekamilika pande zote kwa kujumuisha imani na itikadi, tabia na akhlaqi pamoja na amali na matendo yake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba mwanamke na mwanamme wana hali sawa katika kujengeka kwa ukamilifu wa kimaanawi na kupata malipo na thawabu mbele ya Allah. Tofauti iliyopo baina ya wawili hao ni katika masuala kama urithi na diya, ambayo yanahusu nafasi na wajibu wa kila mmoja wao katika mfumo wa familia, si mbele ya Allah SW.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 36 ambayo inasema:

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo amua jambo kuwa na khiari katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi.

Baada ya aya iliyotangulia, iliyoeleza kwamba kumtii Mwenyezi Mungu ni moja ya sifa za mtu muumini, aya hii inatilia mkazo zaidi juu ya suala hilo kwa kusisitiza kwamba hukumu ya Allah na Mtume wake zinaitangulia irada na matakwa ya muumini; na mtu anayejiitakidi yeye mwenyewe kuwa ni muumini wa kweli hawezi katu kutanguliza takwa lake mbele ya amri na hukumu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa sababu anajua, jambo hilo litamfanya apotoke na kuishia kwenye dhalala na upotofu. Kimsingi hasa ni kwamba, imani ya kweli ni kusalimu amri bila ya hoja na masharti mbele ya amri ya Allah SW. Kwa maana hiyo, kama mtu atakuwa anatekeleza yale maamrisho anayoyapenda yeye mwenyewe tu na anayoyahisi kuwa ni mazuri, na akaasi kuyatekeleza maamrisho yasiyoipendeza nafsi yake au asiyoyajua uzuri wake, huwa kwa kweli anatii utashi wa moyo wake si takwa na amri ya Mola wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuonyesha uja kwa kutii amri za Mwenyezi Mungu na Mtume na kufuata mafundisho na maamrisho ya dini ni alama ya imani ya kweli. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, uhuru wa mtu unakubalika unapojifunga na mipaka ya sharia za Mwenyezi Mungu, si kuwa na uhuru wa kiholela usio na mipaka na kujifanyia mtu lolote atakalo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba sharia zinazotungwa na wanadamu ambazo zinapingana na sharia za Allah huwa sababu ya kupotoka watu na kutanzwa na kila aina ya masaibu.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 37 na 38 ambazo zinasema:

وَإِذْ تَقُولُ لِلَّذِي أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَأَنْعَمْتَ عَلَيْهِ أَمْسِكْ عَلَيْكَ زَوْجَكَ وَاتَّقِ اللَّـهَ وَتُخْفِي فِي نَفْسِكَ مَا اللَّـهُ مُبْدِيهِ وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّـهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَاهُ ۖ فَلَمَّا قَضَىٰ زَيْدٌ مِّنْهَا وَطَرًا زَوَّجْنَاكَهَا لِكَيْ لَا يَكُونَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ حَرَجٌ فِي أَزْوَاجِ أَدْعِيَائِهِمْ إِذَا قَضَوْا مِنْهُنَّ وَطَرًا ۚ وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ مَفْعُولًا

Na ulipo mwambia yule Mwenyezi Mungu aliye mneemesha, nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako aliyo taka Mwenyezi Mungu kuyadhihirisha, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t'alaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa.

 مَّا كَانَ عَلَى النَّبِيِّ مِنْ حَرَجٍ فِيمَا فَرَضَ اللَّـهُ لَهُ ۖ سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ ۚ وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ قَدَرًا مَّقْدُورًا 

Hakuna ubaya kwa Nabii kufanya aliyo mhalalishia Mwenyezi Mungu. Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa walio pita zamani. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni kudura iliyo kwisha kadiriwa.

Kwa mujibu wa mapokeo ya historia, Bibi Khadija (as) alikuwa na mtumwa aliyekuwa akiitwa Zaid, ambapo baada ya kufunga ndoa na Bwana Mtume Muhammad SAW alimtunukia mtukufu huyo mtumwa wake huyo; naye Bwana Mtume SAW, kwanza akamwachia huru Zaid na kisha akamfanya mwanawe wa kupanga. Baada ya hapo, akamposea Zaid binti ya shangazi yake yeye Bwana Mtume aitwaye Zainab. Japokuwa Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa akimuusia kila mara Zaid adumu na mkewe na ajiepushe na suala la talaka, lakini ndoa ya Zaidi na Zainab haikudumu kwa muda mrefu na mwishowe wawili hao wakaachana. Ili kupoza na kufidia hali hiyo Bwana Mtume SAW akaamua amuoe yeye Zainab, lakini akawa anachelea maneno ya watu wasije wakasema: Yeye ameamua kumuoa mke wa mwanawe wa kupanga. Kufanya hivyo lilikuwa tendo chafu na lenye kuchukiza mbele za watu katika zama za ujahilia. Kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu akamwambia Mtume wake: Wewe lifanye jambo hili ili kupambana na mila na desturi hiyo ya kijahilia, wala usihofie maneno ya watu. Kwa sababu kwa yale ambayo Mwenyezi Mungu anawaamuru Mitume wake, haiwapasi wao kumchelea mtu au kundi lolote lile au kutaka kuchunga mila na desturi mbovu zilizozoeleka katika jamii. Kwani kaida na utaratibu alioweka Mwenyezi Mungu katika zama zote za historia ni wa Mitume wake kuzivunja mila potofu na kukabiliana na ada na desturi zilizozoeleka ambazo hazina mantiki yoyote.  Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wakati zinapotokea hitilafu na ugomvi baina ya mke na mume haifai kukimbilia suala la talaka na kuachana na wala wao wasilione jambo jema la kuwashauri watu wengine kufanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa zinapozuka hitilafu kati ya mke na mume, tuwausie kumcha Mungu ili waache ugomvi na mzozo baina yao kwa kuchunga mipaka ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu taqwa na uchaji Mungu ni miongoni mwa mambo yanayoimarisha mfungamano wa kifamilia. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika kutekeleza maamrisho ya dini tumzingatie Allah tu peke yake wala tusishughulishwe na vijembe wala tusihofie kusemwa vibaya na watu. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba tuna wajibu wa kupambana na mila na desturi zisizo sahihi na wala tusihofu makelele na zahama zinazofanywa na watu tunapochukua hatua ya kuyaondoa mambo potofu yaliyozoeleka katika jamii. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah, atuwezeshe kuifanya Qur'ani kuwa katiba na mwongozo wa kila kipengele cha maisha yetu na kuachana na kila mila na desturi potofu zinazokinzana na kitabu hicho kitukufu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.