Sura ya Al-Ahzab, aya ya 39-42 (Darsa ya 753)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 39-42 (Darsa ya 753)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 753 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 39 ambayo inasema:
الَّذِينَ يُبَلِّغُونَ رِسَالَاتِ اللَّـهِ وَيَخْشَوْنَهُ وَلَا يَخْشَوْنَ أَحَدًا إِلَّا اللَّـهَ ۗ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ حَسِيبًا
Ambao walifikisha risala za Mwenyezi Mungu na kumwogopa Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhisabu.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia habari ya ndoa ya Bwana Mtume SAW na aliyekuwa mke wa mwanawe wa kupanga, ambapo mwisho wa maudhui hiyo Mwenyezi Mungu alimtaka Mtume wake asichelee chochote katika kutekeleza amri zake Yeye Mola na wala asirudi nyuma katika kutekeleza aliyoamrishwa kwa kwa sababu ya makelele na maneno ya watu. Aya hii ya 39 inasema, jukumu kuu na la msingi la Mitume wa Mwenyezi Mungu ni kufikisha ujumbe wa Mola wao bila ya woga wala kuhofu chochote. Wao wanamhofu Mola wao tu, wala hawana ndani ya nyoyo zao hofu ya mwengine yeyote ghairi ya Allah SW. Ni wazi kwamba kusimama dhidi ya mila na desturi potofu zilizozoeleka katika jamii au matakwa yasiyo na msingi ya watu humfanya mtu akabiliwe na vitisho na njama za kutaka kumdunisha. Kwa hivyo pamoja na watu wengi kuelewa kwamba mambo wanayofanya si sahihi, lakini kwa sababu ya kuhofia maneno ya watu huamua kuyafanya mambo yanayopingana na akili na ufahamu wao. Lakini hayo ni kinyume kwa upande wa mawalii wa Allah na waumini wa kweli; wao wanamzingatia Mwenyezi Mungu tu wala hawashughulishwi na kauli chafu na maneno mabaya ya mtu yeyote. Kwa sababu wanajua Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwatosha kuwa mlinzi wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba tablighi na utangazaji dini unahitaji taqwa, kutawakali kwa Allah, ujasiri na msimamo thabiti; kwa hivyo mtu asiye na sifa hizi hawezi kufanikiwa katika kazi ya tablighi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa malipo ya tabu, shida na misukosuko wanayovumilia waumini kwa ajili ya kuilinda dini na kuifanyia tablighi na ufikishaji kwa watu yamehifadhiwa mbele ya Allah.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 40 ambayo inasema:
مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٤٠﴾ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا
Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia, kwanza kwa kuzikana mila za kijahilia na kueleza kwamba: Nabii Muhammad SAW hakuwa baba halisa wa Zaid bali Zaid ni mtoto wake wa kupanga; na kwa mtazamo wa sharia za Mwenyezi Mungu ndoa ya Bwana Mtume na mke aliyeachwa na mwanawe wa kupanga haina walakini wowote japokuwa jambo hilo linaonekana kitu kibaya katika mila za ujahilia. Aya hii inawahutubu waumini kwamba msimchukulie Mtume kuwa sawa na yeyote tu miongoni mwenu ambaye ana watoto na jukumu lake la msingi ni kukimu mahitaji ya watoto wake hao huku kukiwa na mambo tofauti yanayomgusa kuhusiana na mapenzi aliyonayo ya baba kwa mtoto wake. Ilhali yeye bwana Mtume Muhammad SAW ni baba wa umma mzima na inampasa kuchukua hatua kwa kuzingatia maslahi ya umma wake ili hadi Siku ya Kiyama uendelee kubaki kuwa umma imara na thabiti unaotekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Kisha aya inaendelea kwa kutaja nukta moja kuu na ya usuli ambayo ni kuhitimishwa jukumu la Utume na Nabii Muhammad SAW na kueleza kwamba: Bwana Mtume Muhammad SAW ana nafasi na hadhi maalumu kati ya Mitume wote; yeye ni Mtume wa Allah na pia ni Mtume wake wa mwisho. Mwenyezi Mungu amemfanya kuwa Mtume wake wa mwisho na amewaletea wanadamu mafundisho ya dini yaliyo jumuishi na yaliyokamilika zaidi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa Uislamu ni dini ya mwisho ya mbinguni na Qur'ani ni kitabu cha mwisho cha Allah ambacho Yeye Mola amekileta kwa ajili ya mwongozo na uongofu wa wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kufanywa Nabii Muhammad SAW kuwa Mtume wa mwisho kumetokana na elimu isiyo na mpaka wala kikomo ya Allah SW ambaye anajua kwamba kwa ujumbe aliompa bwana Mtume SAW mahitaji yote ya mwanadamu ya kuelewa njia ya saada ya duniani na akhera yatakuwa yamekidhiwa.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 41 na 42 ambazo zinasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا
Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru.
وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا
Na mtakaseni asubuhi na jioni.
Aya hizi tulizosoma zinawausia waumini kumdhukuru, kumtaja na kumsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu katika hali zote; kwa sababu katika muda wote wa usiku na mchana kuna mambo mengi ya kumtia mghafala na usahaulifu mwanadamu. Iwe ni mambo na sababu za batini kama hawaa na matamanio ya nafsi au mambo ya nje kama wasiwasi wa shetani na wa watu waovu na waharibifu. Ni wazi kwamba ili kupambana na mambo mbalimbali yaliyomzingira na kumzunguka mwanadamu hakuna njia nyengine ya kufanya isipokuwa kumkumbuka Allah kila wakati. Kusimamisha Sala tano alfajiri mchana na usiku ni sehemu moja tu ya usia huo anaopewa muumini. Lakini katika muda wote wa siku nzima mtu anatakiwa amtaje na kumkumbuka Mola kila wakati; na katika kila uamuzi na hatua anayotaka kuchukua afikirie kwanza kama Mwenyezi Mungu yuko radhi na hilo analotaka kulifanya au la? Ikiwa Allah analiridhia alifanye, la kama hayuko radhi na jambo hilo basi aliache hata kama litapingana na matashi ya nafsi yake au ya watu. Kumkumbuka Mwenyezi Mungu kunapasa kufanyike katika hali zote; kwa mtu kushukuru pale anapojaaliwa neema na kuwa saburi na mvumilivu pale anapofikwa na shida na matatizo. Wakati anapokabiliana na tendo la dhambi amche Mwenyezi Mungu na itokeapo kuteleza akafanya dhambi arejee haraka kwa Mola kwa kutubia na kuomba maghufira. Bila ya shaka mbali na kumkumbuka Allah kila mara moyoni, zimeusiwa pia dhikri na nyuradi mbalimbali za kusoma kwa ulimi katika hali tofauti; kama Bwana Mtume Muhammad SAW alivyomfunza binti yake Fatimatu-Zahra (as) dhikri na uradi uliousiwa kuusoma kila baada ya Sala ambayo ni kusema Allahu Akbar mara 34, Alhamdulillah mara 33 na kisha Subhanallah mara 33!
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kumkumbuka na kumtaja Allah si kwa ulimi na maneno tu, bali mtu anapaswa azingatie yale yanayomfurahisha na kumridhisha Mola wake katika kila fikra na harakati zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu huwa na taathira njema na chanya kwa mtu kunapofanyika kwa sura ya kudumu na ya kuendelea, si ya muda na ya msimu maalumu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kati ya dhikri na nyuradi mbalimbali, iliyousiwa zaidi ni dhikri ya kumsabihi na kumtakasa Allah SW. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 753 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wanaomtaja na kumkumbuka katika kila hali na wakati na kufaidika kiimani na kimatendo kutokana na dhikri hizo. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.