Sep 06, 2017 07:22 UTC

Sura ya Al-Ahzab, aya ya 43-48 (Darsa ya 754)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 754 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 43 na 44 ambazo zinasema:

هُوَ الَّذِي يُصَلِّي عَلَيْكُمْ وَمَلَائِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا 

Yeye na Malaika wake ndio wanaokurehemuni ili kukutoeni vizani mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini.

تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ ۚ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا

Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa: Salaam! Na amewaandalia malipo ya ukarimu.

Katika darsa iliyopita tuliona jinsi Qur'ani tukufu ilivyowausia waumini kukithirisha kumtaja na kumsabihi Mwenyezi Mungu katika hali zote. Aya hizi tulizosoma zinasema: Kila mnapomkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu muwe na hakika kwamba Yeye Allah SW pia anakukumbukeni na kukuteremshieni rehma zake. Ni kama inavyosema aya ya 152 ya Suratul Baqarah ya kwamba: Basi nikumbukeni nitakukumbukeni. Nao malaika pia wanawaombea rehma na maghurifa waumini; na rehma na maghufira hayo ya Mola humfanya mtu atoke kwenye giza la madhambi na dhulma na kumuelekeza kwenye nuru na utakasifu. Kwa hakika kudumisha dhikri na utajo wa Allah huwa sababu ya mtu kupata rehma na fadhila za mtawalia na uongofu maalumu wa Mola. Uongofu ambao humfungulia mtu njia pale anapotanzwa katika maisha na kumuepusha na hilaki na maangamizi pale anapokumbwa na dhoruba kali za kutisha. Siku ya Kiyama pia watu wa aina hiyo wataombewa rehma maalumu na malaika wa Mwenyezi Mungu na watakuwa katika amani na utulivu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba akili na elimu tu ya mwanadamu havitoshi kumwepusha mtu na dhulma na giza la maisha; hivyo anahitaji msaada wa Mwenyezi Mungu ili kuweza kuokoka na giza hilo na kuifikia nuru ya uongofu. Na bila ya shaka dhikri na utajo wa Allah ni utangulizi wa kuifikia nuru hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa imani ya kweli ni ufunguo wa kufungulia milango ya rehma za Allah, rehma ambazo humletea mtu nuru ya uongofu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutakiana rehma kwa watu wa peponi kutafanyika kwa neno Salam, lenye maana ya amani. Na hapa duniani pia waumini wameusiwa wanapokutana waamkiane kwa kutumia tamko hili la kuvutia na lenye maana kubwa.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 45 na 46 ambazo zinasema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ شَاهِدًا وَمُبَشِّرًا وَنَذِيرًا

Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na mwonyaji,

وَدَاعِيًا إِلَى اللَّـهِ بِإِذْنِهِ وَسِرَاجًا مُّنِيرًا

Na mlinganiaji kwa Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa yenye kutoa nuru. 

Katika aya ya 40 ya sura hii ya Ahzab ulizungumziwa Utume wa Nabii Muhammad SAW na kwamba yeye ni Mtume wa mwisho. Aya hizi zinamhutubu yeye Bwana Mtume ya kwamba: Ewe Mtume, wewe ni kigezo na ruwaza iliyokamilika; u miongoni mwa watu na unaishi pamoja nao; na wao wanajua kuwa wewe ni shahidi na mwangalizi wao. Wewe ni kigezo na mfano wa kuigwa na kufuatwa, ambapo mbinu ya wito na ulinganiaji wako imesimama juu ya misingi miwili ya malezi ambayo ni utoaji bishara njema na uonyaji. Bwana Mtume SAW aliwalingania watu wito wa kumwabudu Mungu pekee wa haki na si kuwataka wamnyenyekee na kumsujudia yeye. Kwa sababu kimsingi hasa Mitume wote wameletwa ili kuhakikisha watu hawamwabudu na kumsujudia yeyote ghairi ya Allah SW. Kwa hivyo Mitume hawakuwa wakiwalingania watu wawaabudu wao bali waliwakomboa na unyongeshwaji wa kulazimishwa kuwaabudu mataghuti na majabari na kuwataka wanadamu wote wamwabudu na kumdhihirishia uja wao Mola mmoja tu wa haki. Kuwepo Mitume katika umma wa watu ni mfano wa jua linaloangaza kwa kuwatoa watu kwenye giza la dhulma na ujahili na kuwaelekeza kwenye nuru na mwanga wa uadilifu ili kuhakikisha imani za watu zinajengeka juu ya msingi wa elimu na utambuzi, sio ujinga na khurafa! Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba sifa ya Mitume katika kuwalingania watu haikuwa kwa ndimi tu na maneno matupu bali kwa njia ya amali na matendo pia. Na ndiyo maana walikuwa na wangali vigezo na mifano bora ya kuigwa na kufuatwa kivitendo na wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Bwana Mtume Muhammad SAW ni shahidi na mwangalizi wa amali za watu wa umma wake. Kwa hivyo tuwe makini na kujihadhari katika mienendo na matendo yetu. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika malezi na miongozo kwa watu bishara njema na maonyo ni mambo mawili yanayopasa kuambatanishwa pamoja; kwa sababu kila moja bila ya jengine ima huwatia watu ghururi au kuwakatisha tamaa.

Darsa ya 754 ya Qur'ani inahitimishwa na aya ya 47 na 48 ambazo zinasema:

وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ بِأَنَّ لَهُم مِّنَ اللَّـهِ فَضْلًا كَبِيرًا 

Na wabashirie Waumini ya kwamba wana fadhila kubwa inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. 

 وَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَالْمُنَافِقِينَ وَدَعْ أَذَاهُمْ وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا 

Wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki, na usijali udhia wao. Nawe mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.

Katika aya zilizotangulia "bishara" na "indhari" zimetajwa kuwa ni mbinu ya malezi ya Mitume. Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo kwa kutaja mfano hai wa kila moja kati ya mawili hayo. Bishara njema ni kwa waumini wanaotekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa kuyashika ya wajibu waliyofaradhishiwa na kuyawacha makatazo waliyoharamishiwa. Watu hao watapata rehma maalumu za Allah na malipo ya juu mno na yenye thamani kubwa zaidi ya amali njema walizofanya. Lakini indhari na onyo ni kwa wanafiki na makafiri kwamba si wao peke yao watakaoadhibiwa, bali adhabu ya Allah itawapata pia wale waliowafuata na kutaka kuwaridhisha watu wao. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu anamhutubu Bwana Mtume, ikiwa na maana ya kuwaambia waumini kwamba: Vumilieni maudhi yao ya maneno na vitendo lakini msiwatii na kuwafuata katu; tawakalini na mtegemeeni Allah katika kuyakabili matatizo na tabu zinazokufikeni kwa sababu ya kusimama kwenu imara mbele ya matakwa ya watu hao; na jueni kwamba kama mtafanya hivyo, Yeye Mola atakutosheni kuwa mlinzi na tegemeo lenu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kiongozi wa jamii ya Kiislamu anatakiwa awape matumaini watu safi na wema katika jamii ya kupata rehma na fadhila za Mola na kuwatahadharisha na hatari ya kupatana na maadui wa Uislamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mtu anayetawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu ndiye anayeweza kusimama imara dhidi ya matakwa yasiyo na msingi ya makafiri na wanafiki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba japokuwa wanafiki wanaishi katika jamii ya Kiislamu na kidhahiri wanaonekana kwenye safu za Waislamu lakini kiuhalisia wako kwenye njia ya makafiri; fikra yao na njia wanayofuata wao wote ni moja. Kwa hivyo inapasa kulitambua vizuri kundi la watu hao na kujihadhari na njama zao. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu subira, azithibitishe imani zetu na atunusuru na shari za maadui zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.