Sura ya Al-Ahzab, aya ya 49-50 (Darsa ya 755)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 49-50 (Darsa ya 755)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 755 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 49 ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا
Enyi mlio amini! Mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha mkawapa t'alaka kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayo ihisabu. Basi wapeni cha kuwaliwaza, na muwawache kwa kuwachana kwa wema.
Kama tulivyowahi kueleza katika utangulizi wa sura hii, sehemu kubwa ya aya za Suratul Ahzab zinazungumzia masuala ya kifamilia. Aya hii tuliyosoma inawahutubu waumini wote kuhusu moja ya hukumu za masuala ya ndoa na kueleza kwamba: Endapo baada ya kufunga akdi na kabla ya kufanya tendo la ndoa, mke na mume wataamua kutalikiana, hakuna ulazima kwa mwanamke kukaa eda, bali anaweza mara tu baada ya kupewa talaka kuolewa na mwanamme mwengine. Muda wa eda ya talaka ni kupitisha vipindi vitatu vya hedhi ambapo katika mazingira ya kawaida inawalazimu wanawake kusubiri katika muda huu ili hali yao ya ujauzito iweze kujulikana. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba hata kama halitofanyika tendo la ndoa baina ya mke na mume, lakini wakati mwanamme anapotoa talaka, inampasa ampatie mwanamke hidaya maridhawa ya kumliwaza, ambapo kwa mujibu wa aya ya 237 ya Suratul Baqarah, ni kumpa mwanamke nusu ya mahari yaliyoainishwa wakati wa kufunga akdi. Lakini mbali na hayo, haifai kuachana na kutalikiana kwao mume na mke kukaambatana na maneno na vitendo visivyopendeza, bali wawili hao watengane kwa kuheshimiana pasi na kufanyiana mambo yoyote ya utovu wa maadili na kuvunjiana heshima. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Uislamu ni dini kamili ambayo imejumuisha mambo yote na yenye mafundisho maalumu ya kujenga na kutengeza kwa ajili ya masuala ya kifamilia na kiakhlaqi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, talaka ina athari na matokeo hasi ya kiroho kwa mke; kwa hivyo inapasa kuzifidia kwa kiwango fulani athari hizo kwa kuamiliana naye vyema na kumpa nusu ya mahari yake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba utamaduni wa mafundisho ya Qur’ani unataka hata wakati wa kuachana na kutengana pia kusiwepo uadui, manyanyaso na kufanyiana ukatili mke na mume seuze wakati wawili hao wanapoishi pamoja katika maisha ya ndoa.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 50 ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِنَّا أَحْلَلْنَا لَكَ أَزْوَاجَكَ اللَّاتِي آتَيْتَ أُجُورَهُنَّ وَمَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ مِمَّا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَيْكَ وَبَنَاتِ عَمِّكَ وَبَنَاتِ عَمَّاتِكَ وَبَنَاتِ خَالِكَ وَبَنَاتِ خَالَاتِكَ اللَّاتِي هَاجَرْنَ مَعَكَ وَامْرَأَةً مُّؤْمِنَةً إِن وَهَبَتْ نَفْسَهَا لِلنَّبِيِّ إِنْ أَرَادَ النَّبِيُّ أَن يَسْتَنكِحَهَا خَالِصَةً لَّكَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ ۗ قَدْ عَلِمْنَا مَا فَرَضْنَا عَلَيْهِمْ فِي أَزْوَاجِهِمْ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ لِكَيْلَا يَكُونَ عَلَيْكَ حَرَجٌ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari yao, na ulio wamiliki kwa mkono wako wa kulia katika alio kupa Mwenyezi Mungu, na mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada za mama yako walio hama pamoja nawe; na mwanamke Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, ikiwa Nabii mwenyewe atataka kumwoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Tunajua tuliyo wafaradhishia wao katika wake zao na wanawake ilio wamiliki mikono yao ya kulia. Ili isiwe dhiki juu yako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Aya hii inamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW na inahusu wanawake anaoweza kuwaoa, ambapo ukiondoa hali moja tu ambayo ni maalumu kwa mtukufu huyo, katika hali nyingine zote zilizobaki hakuna tofauti baina ya Mtume na Waislamu wengine. Kwa upande wa wanawake ambao ni jamaa zake mtu, anaweza kuoana na binti ya ami, shangazi, mama mdogo na mjomba wake; na kwa upande wa wasio jamaa zake, anaweza kuoana na mwanamke yeyote yule muumini. Katika hali zote hizo mbili kuainishwa mahari ni miongoni mwa masharti ya akdi ya ndoa ambayo yanalipwa wakati wa kufunga ndoa au mwanamme anajikubalisha kuyalipa hapo baadaye. Kuna nukta moja inayopasa kuashiriwa hapa kuhusiana na wajakazi; nayo ni kwamba Uislamu sio ulioasisi mfumo wa utumwa. Katika zama hizo, utumwa lilikuwa jambo lilioenea na kukubalika ulimwengu mzima, ambapo wasichana na wanawake waliopatikana kama mateka wa vita walikuwa wakifanywa wajakazi. Katika hali hiyo, bila ya shaka Uislamu usingeweza kuchukua hatua ya upande mmoja kuifuta kanuni hiyo ya vita iliyokuwako zama hizo. Pamoja na hayo, dini hiyo tukufu iliweka baadhi ya sharia na kutoa motisha na vishajiishaji vya aina mbalimbali kwa madhumuni ya kuufuta mfumo wa utumwa. Miongoni mwa ratiba ulizoweka Uislamu, ilikuwa ni kuwashajiisha kuwakomboa na kuwapa uhuru wao watumwa pamoja na kuwafanyia ukarimu. Ni kwa sababu hiyo kuachia huru na kumkomboa mtumwa ni moja ya amali bora kabisa na pia imewekwa kuwa ni kafara ya makosa na madhambi mbalimbali. Mtazamo huo wa Uislamu uliwahamasisha Waislamu kuwanunua na kuwakomboa watumwa au kwa kuwaoa wajakazi na kuzaa nao, kuwafanya watu wengine waache kuwaonea na kuwatendea vibaya watumwa. Aya hii aidha imeashiria hali moja maalumu ya ndoa ambayo inajuzu kutekelezwa na Bwana Mtume SAW peke yake; nayo ni kumuoa mwanamke atakayependa kuolewa na mtukufu huyo na kupata heshima ya kuwa mke wake pasi na kupokea mahari. Katika hali hiyo, ikiwa Bwana Mtume mwenyewe atapendezwa na jambo hilo anaweza kumuoa mwanamke kama huyo kwa njia ya akdi. Inafaa pia kuashiria hapa suala la Bwana Mtume Muhammad SAW kuoa wake wengi na kuzijibu baadhi ya tuhuma za maadui au masuali yanayoibuliwa na wale wasio na uelewa. Kwa mujibu wa historia, wakati Bwana Mtume SAW alipotimiza umri wa miaka 25 alimuoa Bibi Khadija ambaye kiumri, alikuwa mkubwa zaidi kuliko mtukufu huyo. Historia inashuhudia kwamba katika muda wote wa uhai wa Bibi Khadija, Bwana Mtume hakuoa mwanamke mwengine yeyote, ilhali ilikuwa ndivyo ilivyozoeleka baina ya Waarabu mtu kuoa wake wengine wakati akiwa angali na mke wake wa mwanzo. Wakati bibi Khadija alipoaga dunia, Bwana Mtume SAW alikuwa na umri wa miaka 53. Maana yake ni kwamba, tangu akiwa na umri wa miaka 25 hadi 53 aliishi na bibi Khadija peke yake, na ndoa nyengine zote alizofunga ilikuwa ni baada ya kuaga dunia mke wake huyo. Kama bwana Mtume angelikuwa mtu mwenye uchu wa wanawake, kulingana na mila na desturi za Waarabu hakukuwa na kizuizi chochote kwake cha kuoa wake wengi katika kipindi kile kile cha ujana wake. Lakini nukta ya pili ni kuwa ukiondoa Aisha, wake wengine wote aliowaoa baada ya kufariki dunia bibi Khadija, walikuwa wanawake wajane. Hii yenyewe ni ushahidi na ithbati kwamba, kuoa tena mtukufu huyo hakukuwa kwa lengo la kuwa na wake vijana na mabikira, bali alifanya hivyo kwa madhumuni ya kuwatunza na kuwasitiri wanawake wajane; na nyingi ya ndoa hizo zilitokana na matakwa ya wao wanawake wenyewe. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika suala la ndoa mwenye mamlaka ya kuainisha uhalali na uharamu wake ni Allah SW, si ridhaa tu ya pande mbili za mwanamke na mwanamme. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa wanadamu wote wanahitaji kufunga ndoa; na haiwezekani kumnyima mtu yeyote jambo hilo hata akiwa mateka wa vita. Aidha aya hii inatutaka tuelewe kwamba Uislamu umeweka mahari kuwa kitu cha dhamana ya ndoa kwa ajili ya wanawake ili kulinda haki zao za mali na milki. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 755 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azibariki ndoa zetu na azifanye ziwe sababu ya kuwa na mwisho mwema sisi na vizazi vyetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.