Sura ya Al-Ahzab, aya ya 51-54 (Darsa ya 756)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 51-54 (Darsa ya 756)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 756 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 51 ambayo inasema:
تُرْجِي مَن تَشَاءُ مِنْهُنَّ وَتُؤْوِي إِلَيْكَ مَن تَشَاءُ ۖ وَمَنِ ابْتَغَيْتَ مِمَّنْ عَزَلْتَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكَ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن تَقَرَّ أَعْيُنُهُنَّ وَلَا يَحْزَنَّ وَيَرْضَيْنَ بِمَا آتَيْتَهُنَّ كُلُّهُنَّ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا فِي قُلُوبِكُمْ ۚوَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَلِيمًا
Unaweza kuakhirisha zamu kwa umtakaye katika wao, na umsogeze umtakaye. Na kama ukimtaka yule uliye mtenga, basi si vibaya kwako. Kufanya hivi kutapelekea yaburudike macho yao, wala wasihuzunike, na wawe radhi juu ya kile unacho wapa wao wote. Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa ni baada ya kufariki dunia bibi Khadija (as), ndipo Bwana Mtume Muhammad SAW, tena akiwa na umri wa miaka 53, alioa wake wengine kadhaa. Baadhi ya ndoa hizo zilitokana na maombi ya baadhi ya makabila ya kutaka Bwana Mtume aoe kwao, ili kwa njia hiyo wapate fahari na heshima ya kuwa na ujamaa na mtukufu huyo. Na baadhi ya ndoa hizo alifunga kwa madhumuni ya kuwatunza wanawake wajane. Ni vyema tukumbushe tena pia kwamba, ukiondoa mke wake mmoja tu, wake wengine wote aliooa Bwana Mtume SAW baada ya kufariki dunia bibi Khadija walikuwa wajane; na ndio maana hakupata nao watoto. Kwa kuzingatia kuwa akthari ya ndoa hizo hazikutokana na takwa la mtukufu huyo, baadhi ya wanawake aliowaoa walikuwa radhi waolewe bila ya kupewa mahari, lakini wapate heshima tu ya kuwa wake wa Mtume wa Allah. Kwa sababu hiyo, katika aya hii tuliyosoma, Mwenyezi Mungu SW anampa ruhusa Mtume wake ya kugawa muda wake kwa ajili ya wake zake kwa namna anayohisi yeye mwenyewe kuwa inafaa, na kuwatayarishia mazingira ya kuwafurahisha na kuwaridhisha. Bila ya shaka kila mmoja kati ya wake zake Bwana Mtume SAW alikuwa na matamanio na matarajio yake ambayo yalikuwa nje ya uwezo wa mtukufu huyo; na kutokana na jukumu zito la Utume alilokuwa nalo haikuyumkinika kuyakidhi; lakini kwa kadiri hali ilivyoruhusu na yeye mwenyewe aliona inafaa, aliwatimizia. Na sababu ni kwamba kufurahika mke kuna nafasi muhimu katika utulivu wa maisha ya mtu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kutekeleza majukumu mazito ya kidini na kijamii kusiwe sababu ya kumfanya mtu asitimize mas-ulia aliyonayo kwa familia yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa wakati mume anapokuwa mtu mwenye mas-ulia na majukumu mazito ya kijamii, jamaa wa familia hasa mke wanatakiwa waielewe hali hiyo na wawe wasaidizi kwake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kuandaa mazingira ya amani na utulivu yatakayoleta uchangamfu na furaha na kuondoa ghamu na huzuni kwa mke ni miongoni mwa majukumu aliyonayo baba wa familia.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 52 ambayo inasema:
لَّا يَحِلُّ لَكَ النِّسَاءُ مِن بَعْدُ وَلَا أَن تَبَدَّلَ بِهِنَّ مِنْ أَزْوَاجٍ وَلَوْ أَعْجَبَكَ حُسْنُهُنَّ إِلَّا مَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ رَّقِيبًا
Hawakuhalalikii wanawake (wengine) baada ya hawa, wala kuwabadilisha kwa wake wengine ijapokuwa uzuri wao utakupendeza; isipo kuwa uliye mmiliki kwa mkono wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu ni Mchungaji wa kila kitu.
Aya hii inaendeleza maudhui kuhusu wake wa Bwana Mtume kwa kuzungumzia amri ya kumtaka mtukufu huyo akatishe kupokea maombi ya wanawake wanaotaka waolewe na yeye na kumwambia: Ewe Nabii! Usikubali tena ombi jengine lolote la ndoa, na waambie watu kwamba Mwenyezi Mungu amenizuia kuoa mke mwengine mpya. Ikiwa watakuomba uwape talaka baadhi ya wake zako ulionao sasa kisha uoe wake wengine wapya badala yao, hilo pia usilikubali hata kama atakayekuomba ufanye hivyo atakuwa ni mwanamke kijana na jamili wa sura, jambo ambalo kwa kawaida huwa chachu ya kumpa hamu zaidi mtu ya kuoa mke mwengine. Kwa mujibu wa historia, Bwana Mtume Muhammad SAW hakumtaliki yeyote kati ya wake zake wajane kwa ajili ya wanawake vijana waliomwomba afunge nao ndoa au kuongeza mke mwengine mpya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba miongoni mwa hoja za kuthibitisha ukweli wa Utume wa Nabii Muhammad SAW na kwamba Qur’ani ni Kitabu cha mbinguni ni aya zinazozungumzia mipaka ya kufanya mambo aliyowekewa mtukufu huyo. Ingekuwa Qur’ani ni kitabu kilichotungwa na Mtume mwenyewe musingekuwa ndani yake na aya zinazombana na kumwekea mipaka ya ufanyaji mambo mtukufu huyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kumdharau mtu mke aliyenaye au kumpa talaka kwa ajili ya kuoa mke mwengine aliye kijana na mzuri wa sura ni jambo lililokatazwa na Allah SW.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 53 na 54 ambazo zinasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَـٰكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنكُمْ ۖ وَاللَّـهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ ۚ وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ ۚوَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّـهِ وَلَا أَن تَنكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِن بَعْدِهِ أَبَدًا ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمًا
Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila mkipewa ruhusa kwenda kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapo itwa basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapo wauliza wake zake haja waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haikufalieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
إِن تُبْدُوا شَيْئًا أَوْ تُخْفُوهُ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا
Mkidhihirisha chochote kile, au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Aya hii ya 53 ya Suratul Ahzab inazungumzia baadhi ya adabu za kijamii na ugeni na kuwahutubu waumini haya yafuatayo:-
Mosi: Msiingie nyumbani mwa watu bila ya taarifa.
Pili: Kama mtakuwa mumealikwa nyumbani kwa mtu, nendeni katika ule muda mliopangiwa, si kabla yake; na baada ya kula chakula ondokeni, si kukaa mpaka mkajisahau.
Tatu: Kama hamkualikwa nyumbani kwa mtu lakini mkawa na shida naye ya kulazimika kwenda nyumbani kwake, katika hali hiyo kaelezeeni haja zenu mlangoni na mchunge mipaka ya faragha ya watu wanawake wa mwenye nyumba. Na mlahaka wenu usiwe wa kukufanyeni mtiliwe shaka, bali uwe wa murua na wa kiuchaMungu.
Adabu na maamrisho hayo yanatakiwa yatekelezwe kwa namna bora zaidi hasa inapokuwa ni katika nyumba ya Mtume na kwa watu wa nyumbani kwake. Isitoshe waumini wajiepushe na jambo lolote lile la kumkera na kumuudhi Bwana Mtume SAW. Mbali na aya hii, kuna aya nyingine kadhaa pia za Qur’ani zinazozungumzia nukta nyenginezo kuhusu adabu na desturi za ugeni. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuchunga akhlaqi na adabu za kijamii ni miongoni mwa masharti ya imani; na si kutosheka tu na kutekeleza amali za kiibada pekee. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa nyumba ina mipaka yake ya faragha, na hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuingia kwenye mipaka ya faragha ya mwenye nyumba bila ya idhini yake mwenyewe. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kumwalika mtu ugeni na kumkirimu mgeni ni jambo lililousiwa na Uislamu na viongozi wa dini; pamoja na hayo mgeni asiwe sababu ya maudhi na usumbufu kwa mwenye nyumba. Kadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa falsafa ya hijabu na kuwekwa mipaka katika uhusiano wa kijamii baina ya wanawake na wanaume ni kuhakikisha wawili hao wanachunga staha na usafi wao wa kimaadili na kujiweka mbali na mambo yenye madhara kiakhlaqi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 756 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuufuata Uislamu katika kila kipengele cha maisha yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.