Sura ya Al-Ahzab, aya ya 55-58 (Darsa ya 757)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 55-58 (Darsa ya 757)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 757 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 55 ambayo inasema:
لَّا جُنَاحَ عَلَيْهِنَّ فِي آبَائِهِنَّ وَلَا أَبْنَائِهِنَّ وَلَا إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ إِخْوَانِهِنَّ وَلَا أَبْنَاءِ أَخَوَاتِهِنَّ وَلَا نِسَائِهِنَّ وَلَا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ ۗوَاتَّقِينَ اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا
Hapana ubaya kwao (wake za Mtume) kuonana na baba zao, wala watoto wao, wala ndugu zao, wala watoto wa ndugu zao wanaume, wala watoto wa ndugu zao wanawake, wala wanawake wenzao, wala wale iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Na enyi wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu.
Katika kipindi kilichopita tulisoma aya iliyoashiria hukumu ya hijabu pale mwanamke anapokuwa mbele ya asiyekuwa maharimu yake. Aya hii tuliyosoma inazungumzia akraba na jamaa wa karibu ambao ni maharimu na kueleza kwamba: watu wa familia kama baba, kaka na mwana wa kiume, wao ni maharimu kwa binti, dada na mama zao. Katika ngazi inayofuatia, watoto wa kaka na dada yake mtu, wao pia ni maharimu kwa ami na mama zao wadogo, ili mabinti na wake za watu wasihisi hali ya tabu na dhiki wanapokuwa kwenye mchanganyiko wa ndani ya familia. Mbali na anapokuwa mbele ya mwanamme ajinabi asiye maharimu yake, mwanamke Muislamu anatakiwa avae vizuri pia anapokuwa mbele ya baadhi ya wanawake kama wanawake makafiri au mtumishi wake, kwa sababu wanaweza kwenda kuwasimulia waume zao au wanaume wengine maajinabi yale wanayoyaona kwake. Bila shaka lengo la hukumu zote hizi ni kuwahifadhi wanawake na uchafu wa kimaadili na kiakhlaqi. Na mbali na kulinda mwenendo wa nje na wa dhahiri, inatakiwa kuimarisha pia taqwa ya batini na ndani ya nafsi yake mtu ili usipatikane upenyo wa vishawishi vya kumtumbukiza kwenye uchafu wa madhambi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hukumu za Uislamu hazimweki mtu kwenye hali ya tabu na dhiki. Akraba na jamaa wa familia moja wanaoishi pamoja, wao kwa wao ni maharimu. Suala la kuchunga hijabu ni wajibu mbele ya majinabi na wasio maharimu wa mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika mahusiano na milahaka ya kifamilia na kijamii ya mtu na watu walio maharimu au wasio maharimu zake katika mambo yote, anatakiwa azingatie taqwa na usafi wa maadili. Hukumu ya hijabu pia imewekwa kwa msingi huohuo.
Ifuatayo sasa ni aya ya 56 ambayo inasema:
إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا
Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na msalimuni na jisalimisheni (kwa kutii amri yake).
Aya hii na nyingine mbili zinazofuatia zinatilia mkazo kulindwa heshima ya Bwana Mtume Muhammad SAW na waumini kwa ujumla na kuwataka Waislamu wawe wanamsalia Mtume wa Allah ambaye ni sababu ya wao kuufikia uongofu na saada na kutii maamrisho yake. Lakini kabla ya kutoa amri hiyo, Allah SW anasema, Mimi mwenyewe na malaika wangu pia tunamsalia Mtume na kuenzi tabu anazopata na jitihada kubwa anazofanya katika kufikisha risala ya Utume. Yeye ni mwenye pupa na hamu kubwa ya kuona nyinyi mnaongoka; na pasi na kutumainia chochote kwenu amejitahidi kwa uwezo wake wote kufanya kila lililowezekana kufanya katika njia hiyo; basi na nyinyi pia muenzini na msalieni pale linapotajwa jina lake. Imepokewa Hadithi kuwa masahaba walimuuliza Bwana Mtume Muhammad SAW kuhusu namna ya kumsalia yeye. Bwana Mtume akawaambia: Nisalieni kwa kusema hivi:
اللهم صل علی محمد و علی آل محمد کما صلیت علی ابراهیم انک حمید مجید. اللهم بارک علی محمد و آل محمد کما بارکت علی ابراهیم و آل ابراهیم انک حمید مجید»
Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mahali ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu na malaika wake wanamsalia Mtume kuenzi kazi aliyofanya kwa tabu, usumbufu na misukosuko, sisi ambao ni wafuasi wa mtukufu huyo tunapaswa kuthamini jihadi na kujitolea kusio na kifani kwa mja huyo mteule wa Allah, kwa kutekeleza wajibu wetu kwa kumsalia kwa ndimi zetu na kumtii kwa matendo yetu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mapenzi na mahaba ya moyoni tu hayatoshi. Tunapaswa kudhihirisha na kubainisha wazi katika jamii mapenzi yetu kwa shakhsia watukufu na wazee waliotangulia.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 57 na 58 ambazo zinasema:
إِنَّ الَّذِينَ يُؤْذُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا مُّهِينًا
Hakika wanao muudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehesha.
وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا
Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na waumini wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio dhaahiri.
Baada ya aya iliyotangulia kuwausia waumini kuienzi kazi kubwa iliyofanywa na Mtume wa Allah kwa kumsalia na kumtakia rehma mtukufu huyo, aya tulizosoma zinasema: Lakini wale ambao kwa maneno na mwenendo wao wanamuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu atawapa adhabu kali duniani na akhera, wala hawatopata rehma zake Mola. Maana ya kumuudhi Mwenyezi Mungu ni mtu kufanya jambo kinyume na analotaka na analoliridhia yeye Mola, ambapo badala ya kupata rehma za Allah huandamwa na laana na ghadhabu za Mola. Kwa mujibu wa Hadithi, kitendo chochote cha kuwaudhi na kuwabughudhi waja wa Mwenyezi Mungu ni sawa na kumuudhi yeye Allah SW. Kama ambavyo ndani ya Qur'ani imeelezwa kuwa, kuwakopesha na kuwasaidia waja wa Allah ni sawa na kumkopesha Yeye Mola. Na mtu ambaye hayakubali maneno ya Bwana Mtume Muhammad SAW akayakana na kuyakadhibisha au akamzulia tuhuma mtukufu huyo au akaamiliana naye kwa utovu wa adabu atakuwa amemghadhibisha Mwenyezi Mungu na kumuudhi Mtume wake. Bila shaka yoyote kuwaudhi Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW pia ni sawa na kumuudhi mtukufu huyo, na hilo ni jambo lililosisitizwa katika Hadithi. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba si Mtume wa Allah peke yake, lakini waumini wote pia wanawake na wanaume inapasa waheshimiwe; na mtu yeyote yule hana haki ya kumtuhumu muumini na kumvunjia heshima yake bila ya hoja na ushahidi kwa sababu ya dhana tu au kumtizama kwa jicho baya. Kitendo hicho ni dhambi kubwa na nzito mbele ya Mwenyezi Mungu na matokeo yake ni mtu kufikwa na adhabu kali. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusiwaudhi na kuwabughudhi watu kwa maneno na tabia zetu; kufanya hivyo kutatukosesha rehma za Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kumtusi mtu, kumdhalilisha na kumfanyia istihzai kuna matokeo mabaya, ambayo baadhi yake mtu atayaona na yatamdhihirikia papa hapa duniani. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atulinde na kauli na matendo ya kumuudhi Yeye Mola, Mtume wetu pamoja na Waislamu wenzetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.