Sura ya Al-Ahzab, aya ya 59-62 (Darsa ya 758)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 59-62 (Darsa ya 758)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 758 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 59 ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗوَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Katika darsa kadhaa zilizopita tumeashiria maudhui ya mavazi na hijabu kwa mujibu wa aya za Qur’ani tukufu. Aya hii ya 59 ya Suratul Ahzab inaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Kuvaa buibui au mtandio mrefu hakutoshi, lakini inavyotakiwa wasichana na wanawake waumini wavae mavazi yao kwa namna ambayo yataweza kufunika mwili wote pamoja na nywele; na si kufunika baadhi ya sehemu tu za mwili au nywele zao. Kisha aya inaendelea kusisistiza kwamba vazi hilo kamili na lenye kusitiri sehemu zote litakufanyeni nyinyi wanawake Waislamu mjulikane kuwa ni watu wenye kujistahi na kujiheshimu na hivyo msiwe mnaudhiwa na kuvunjiwa heshimu na watu wachafu; yawe maudhi hayo ni ya maneno au ya milahaka isiyofaa ambayo itakusababishieni machungu na mateso ya kiroho. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba falsafa na hekima ya kufaradhishwa hijabu ni kuwalinda wanawake na macho ya utamanifu, maneno machafu na milahaka miovu ya watu. Kwa hivyo hijabu kwa mwanamke ni kinga na ngao japokuwa imewekewa pia vizuizi na mipaka yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kulindwa staha na heshima ya jamii ya Kiislamu ni jambo lililotiliwa mkazo na Qur’ani na Mtume wa Allah; na sehemu mojawapo ya uchungaji heshima hiyo inawahusu wanawake ambao wanatakiwa wanapokuwa kwenye harakati za nje ya nyumba zao wawe wanavaa mavazi ya heshima. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Uislamu haujapanga kuwatawisha na kuwafungia wanawake majumbani; kwa hivyo hakuna kizuizi wala pingamizi kwa wanawake Waislamu kushiriki kwenye shughuli za kijamii ikiwa tu watajistahi, wakachunga murua wao na kujisitiri kwa vazi la heshima la hijabu.
Darsa ya 758 ya Qur’ani inahitimishwa na aya ya 60, 61 na 62 ambazo zinasema:
لَّئِن لَّمْ يَنتَهِ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْمُرْجِفُونَ فِي الْمَدِينَةِ لَنُغْرِيَنَّكَ بِهِمْ ثُمَّ لَا يُجَاوِرُونَكَ فِيهَا إِلَّا قَلِيلًا
Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitna Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.
مَّلْعُونِينَ ۖ أَيْنَمَا ثُقِفُوا أُخِذُوا وَقُتِّلُوا تَقْتِيلًا
Wamelaaniwa! Popote waonekanapo wakamatwe na wauliwe kabisa.
سُنَّةَ اللَّـهِ فِي الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلُ ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا
Hii ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyo kuwa kwa wale walio pita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.
Aya hizi zinawahusu watu waliokuwa wakiishi Madina katika zama za Bwana Mtume Muhammad SAW, lakini kwa namna mbalimbali wakawa wanafanya mambo yaliyosababisha kuvurugika amani ndani ya jamii. Wale waliokuwa na maradhi ya nafsi walikuwa wakiwasumbua wasichana na wanawake wa Madina. Kwa upande mwingine wanafiki nao, ambao walikuwa wakitumia visingizio tofauti kukwepa kwenda vitani kupigana jihadi na maadui wa Uislamu, walikuwa wakieneza uvumi kwa watu ili kuzusha wahaka na hofu. Walikuwa wakiwavunja moyo watu na kudhoofisha hamasa ya wapiganaji kwa kuukuza uwezo wa adui au hata kueneza habari za uvumi za kudhoofika na kushindwa jeshi la Waislamu. Kwa kuzingatia kwamba katika jamii yoyote ile kuwepo amani na usalama ni muhimu zaidi kuliko jambo jengine lolote ikiwemo hata uchumi na maisha ya watu Mwenyezi Mungu SW anamwambia Mtume wake: Wachukulie hatua kali kabisa watu wa aina hii wanaowafanya watu wakose amani na usalama wa kiroho na kinafsi. Baadhi yao wafukuze waondoke kabisa Madina na wengine wapige vita uwatokomeze ili liwe somo na funzo kwa wengine, asitokee tena mtu yeyote akathubutu kuvuruga amani na usalama wa watu kwa kisingizio chochote kile. Kwa kumalizia, aya hizi zinaashiria kaida na utaratibu usiobadilika aliouweka Allah na kueleza kwamba: Kuing’oa na kuitokomeza mzizi ya ufisadi na uvurugaji amani na usalama ni miongoni mwa ada na kaida alizoweka Allah SW na kuwataka Mitume wake wazifanyie kazi katika zama zao wenyewe na kuendelezwa katika zama za baada yao na watawala wa Kiislamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusijilegeze na kuonyesha udhaifu mbele ya watu wanaovuruga usalama na kusababisha amani kukosekana katika jamii; kwa sababu kuchafuka kwa amani ni mithili ya ugonjwa thakili unaohatarisha uzima wa jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wasababishaji wa fitna na ukosefu wa amani na usalama katika jamii inapasa waandamwe na kuwafanya wajihisi hawana usalama popote walipo. Watu wa aina hiyo inapasa wakamatwe na kupewa adhabu kali kulingana na mtazamo wa mtawala wa Kiislamu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kueneza uvumi ni moja ya njia na mbinu zinazotumiwa na adui kujipenyeza na kuwa na ushawishi ndani ya jamii ya Kiislamu. Viongozi kwa upande wao wana wajibu wa kubainisha ukweli na uhakika wa mambo ili kujenga imani kwa watu; na watu nao wanatakiwa wasiwe wanakiamini na kukipa umuhimu kila wanachosikia ikawa wao wenyewe ndio wasababishaji wa kuenea uvumi ndani ya jamii. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa haifai kuzingatia maslahi au tahafifu yoyote katika kutekeleza hukumu kwa watu wanaovuruga amani na usalama wa jamii; inatakiwa mtawala wa Kiislamu atekeleze hukumu ya Allah kama inavyostahiki. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaalie jamii za mataifa yote ya Waislamu ziishi katika amani na usalama na azinusuru na shari za maadui zao wa ndani na nje ya nchi zao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.