Sura ya Al-Ahzab, aya ya 63-68 (Darsa ya 759)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 63-68 (Darsa ya 759)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 759 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 63 ambayo inasema:
يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ ۚ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا
Watu wanakuuliza khabari ya Saa (ya Kiyama). Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu. Na nini kitakujuvya? Pengine hiyo Saa iko karibu.
Makafiri na wanafiki, ambao hawakuwa na hoja ya kukana uwezekano wa kujiri Kiyama, ili kuzusha shaka ndani ya nyoyo za watu na kudhoofisha imani zao walikuwa wakimuuliza Bwana Mtume Muhammad SAW suali hili, kwamba kama uyasemayo ni kweli, tuambie basi hicho Kiyama kitatokea lini hasa? Inapasa tukumbushe hapa kwamba kutojua wakati hasa wa kutokea jambo si hoja ya kukana kujiri kwake. Sisi wanadamu wote tunajua kwamba iko siku kila mmoja wetu atakufa, lakini hakuna yeyote ajuaye mauti yatamfika siku na saa gani hasa. Sasa ikiwa hatujui tutakufa lini, hiyo itakuwa hoja ya kuthibitisha kwamba hatutokufa? Isitoshe, kama Bwana Mtume SAW angewaambia watu hao kwamba Kiyama kitatokea miaka elfu moja ijayo, je wao wangebaki hai mpaka miaka elfu moja mingine ili kuja kubaini ukweli wa maneno ya Bwana Mtume kisha wasilimu? Aya tuliyosoma inaendelea kueleza kwamba: Wakati wa kutokea Kiyama anaujua Allah SW peke yake, na si kwamba Bwana Mtume naye analijua hilo ila anaficha tu kulieleza. Muhimu ni kwamba kila mtu muumini aitakidi kuwa muda wa kujiri tukio la Kiyama uko karibu, hivyo achunge mwenendo na matendo yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kutojua wakati wa kutokea Kiyama hakuathiri asili ya kujiri kwake; na waumini, wao wana yakini juu ya hilo kutokana na imani yao kwa sifa ya ukweli wa Nabii wao wa rehma Muhammad SAW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tunatakiwa muda wote tujiweke tayari kuyakabili mauti na kusimamishwa mbele ya mahakama ya Mwenyezi Mungu. Si muhimu mtu kuujua wakati wake wa kufikwa na mauti; muhimu ni kujiandaa na kuwa na utayari wa kulikabili tukio hilo zito.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 64, 65 na 66 ambazo zinasema:
إِنَّ اللَّـهَ لَعَنَ الْكَافِرِينَ وَأَعَدَّ لَهُمْ سَعِيرًا
Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto unao waka kwa nguvu.
خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ لَّا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا
Watadumu humo milele. Hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru.
يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا
Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungeli mt'ii Mwenyezi Mungu, na tungeli mt'ii Mtume!
Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia ambayo ilizungumzia masuali ya makafiri ya kuibua shaka kuhusu Kiyama, kwa kueleza kwamba: Watu wanaotaka kudhoofisha imani na mafundisho ya dini na kuvuruga mawasiliano ya watu na Mtume wa Allah watakosa rehma za Mola hapa duniani, na huko akhera watafikwa na adhabu kali. Na adhabu yenyewe itakuwa ya namna ambayo itawafanya watamani wasingekuwa wakiamiliana na dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kama walivyofanya walipokuwa hapa duniani. Lakini wapi! Ya laiti haileti; kwa sababu hakutokuwa na fursa tena ya kufidia waliyoyatenda huko nyuma, wala uwezekano wa kurudi tena duniani kwa ajili ya kutubia, wala pia kuwepo mtu yeyote wa kuweza kuwaokoa au kuwapunguzia adhabu inayowangojea. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kukufuru na kukadhibisha, ambako kunatokana na inadi na ukaidi dhidi ya haki hatima yake ni kupatwa na laana ya Allah hapa duniani na huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kinyume na mfumo wa kijamii uliopo hapa duniani, huko akhera hakuna mtu atakayekuwa na uwezo wa kumsaidia mwenzake na kumuepusha na adhabu ya Allah. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba njia pekee ya kuokoka na kufuzu duniani na akhera ni kumtii Mwenyezi Mungu SW na Mtume wake SAW. Kughafilika na jambo hilo kutatuletea majuto huko tunakoelekea.
Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya za 67 na 68 ambazo zinasema:
وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا
Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwat'ii mabwana zetu na wakubwa wetu; nao ndio walio tupoteza njia.
رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا
Mola wetu Mlezi! Wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana kubwa.
Wakati waovu watakapoiona adhabu Siku ya Kiyama ndimi zao zitafunguka na kuanza kuwalaani na kuwaapiza watu waliosababisha wao kupotoka. Lakini maneno na maapizo yao hayo hayatokuwa utetezi wa kuhalalisha maovu yao, kwa sababu wao wangeliweza kumtii Mtume na waja wema badala ya kuwatii wakubwa zao na wazee wao waliotangulia waliokuwa wakifuata upotofu, ili na wao wasije wakapotoka. Isitoshe, hao wakubwa wa kaumu zao hawakuwalazimisha wawafuate na kuwatii kwa nguvu, bali wangeweza kuzikataa itikadi zao. Bila ya shaka watu waovu waliokusudiwa hapa miongoni mwa wakubwa wa kaumu, ni watu wenye nguvu za utawala na madaraka na mali na utajiri. Watu hao hawawezi kuwa kipimo cha kutumia mtu kupambanua na kutambua haki na batili; na lau kama wale waliowafuata watu hao wangewaendea na kuwafuata watu wenye elimu na hekima, wangeweza kuwa na matumaini ya kuokoka. Ajabu ni kwamba watu hao waovu ambao wao wenyewe wamelaaniwa na Allah wanaomba wakubwa na mabwana zao wapewe adhabu maradufu na kupata laana kubwa zaidi, ilhali endapo ombi lao hilo litakubaliwa litawafanya wao pia wapate adhabu maradufu. Ni kama inavyoeleza sehemu aya ya 38 ya Suratul-A’raf pale Allah SW atakapowajibu watu watakaomwomba awazidishie wakubwa wao adhabu maradufu kwa kuwaambia: Itakuwa kwenu nyote maradufu. Kwa wale viongozi wa ukafiri ni kutokana na kuwapoteza watu; na kwa wale wafuasi wao ni kutokana na kuwasaidia viongozi wao hao madhalimu. Kwa sababu lau kama wao wasingeliwafuata wakubwa hao wa dhulma na ukafiri wasingeweza peke yao kuendeleza dhulma zao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama watu waovu watatafuta visingizio vya kutetea na kuhalalisha makosa yao na kutaka kuwabebesha dhima watu wengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kutii na kuwafuata kibubusa wakubwa wa jamii ni jambo lisilokubalika kiakili na kidini na ni jambo litakalomletea majuto mtu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba watu wanaoanzisha mambo potofu yanayosababisha watu kufuata dhalala na upotofu wanabeba dhima na mas-ulia ya kupotoka watu hao na athari zitakazotokana na upotokaji huo hata kama itakuwa ni baada ya wao kufa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 759 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na ufuataji mambo kibubusa kwa hoja na kisingizio cha kuwatii watawala na wenye mamlaka juu yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.