Sep 11, 2017 05:43 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Septemba 11

Ahlan wasahlan wamarhaba mpenzi mwanaspoti wa RT na karibu katika dakika hizi chache tutupie jicho matukio kadhaa ya michezo yaliyotawala vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa. Karibu…

Wanamieleka chipukizi wa Iran waibuka wa 4 Ugiriki

Wanamieleka barobaro wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameibuka katika nafasi ya nne katika Mashindano ya Mabingwa wa Mieleka ya Makadeti mwaka huu 2017 nchini Ugiriki. Siku ya Jumapili, Muirani Mehdi Akhbar Eshghivasoukolaei alituzwa medali ya dhahabu baada ya kumbwaga Mjapani Kanata Yamaguchi kwa alama 6-0 katika mpambano wa fainali ya wanamieleka wenye kilo 54 uliopigwa katika Ukumbi wa Ano Liosia Olympic, katika mji mkuu wa Ugiriki, Athens. Baadaye siku hiyo hiyo, wanamieleka mabarobaro wa Iran ya Kiislamu, Meysam Enayatollah Zaree and Seyyed Mehdi Seyyedabasali walitosheka na medali za shaba kila mmoja katika kategoria za kilo 76 na 100 kwa utaratibu huo. Kadhalika Abbas Ali Foroutanrami nusuru aipe Iran dhahabu nyingine lakini alipelekwa mchakamchaka na Mrusi Alan Bagaev na hivyo kutwaa medali ya fedha. Mohammad Ashghar aliipa Iran medali ya shaba baada ya kumlemea Masaki Sato raia wa Japan katika mpambano wa wanamieleka wenye kilo 69. Russia waliozoa jumla ya pointi 73 walitawazwa washindi wa mashindano hayo yanayofahamika kwa kimombo kama 2017 Cadet World Championships yaliyoanza Septemba 4 na kumalizika Septemba 10, huku Marekani na Azerbaijan zikishikilia nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.

Soka: Iran kuchuana na Togo

Nikudokeze kwamba timu ya taifa ya soka ya Iran inatazamiw kuvaana na Togo katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki baadaye mwezi huu. Mehdi Taj, Mkuu wa Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vijana wa Timu Melli ya Iran watashiriki mechi mbili za kirafiki za kimataifa nchini Russia mwishoni mwa mwezi huu.

Timu ya taifa ya soka ya Iran

Mchuano wa Iran na timu ya Afrika ya Togo utapigwa Septemba 29, na siku sita baadaye, itavaana na Russia katika uwanja wa mji wa St. Petersburg. Iran ambayo ipo katika nafasi ya 24 katika orodha ya mwisho ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA, kadhalika inatazamiwa kuchuana na Sweden katika mchuano mwingine wa kimataifa wa kirafiki, ikiwa ni katika maandalizi ya Kombe la Dunia mwakani nchini Russia. Tayari Iran imejikatia tiketi ya kushiriki fainali hizo za dunia.

Mbio za Kombe la Dunia 2018

Misri imerejea kileleni mwa Kundi E katika michuano ya soka ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia. Hii ni baada ya Mafarao wa Misri kuwafunga vijana wa The Cranes ya Uganda bao 1-0 katika mchuano wa marudiano uliochezwa katika uwanja wa Burg El-Arab mjini Alexandria Jumanne usiku. Bao la mshambuliaji Mohamed Salah katika dakika ya saba ya mchuano huo kipindi cha kwanza, ilitosha kuisaidia Misri kumaliza mechi hiyo kwa ushindi huo mwembamba lakini muhimu. Kabla ya mchuano huo, Uganda waliishinda Misri mabao 2-1 wiki iliyopita jijini Kampala. Ushindi huo umewapa furaha kubwa mashabiki wa Misri ambao mara ya mwisho kutinga Kombe la Dunia ni mwaka 1990.

Kombe la Dunia 2018, nchini Russia

Huku hayo yakirifiwa, Shirikisho la Soka Duniani FIFA, limetangaza kwamba mchezo kati ya Afrika Kusini na Senegal unapaswa kurudiwa kutokana na makosa ya mwamuzi wa mchezo huo. Mchezo Kati ya Bafana Bafana na Senegal ulipigwa Novemba 12 mwaka jana, ambapo vijana wa Bafana Bafana waliibuka washindi. Kwa mujibu wa maafisa wa FIFA, mchezo huo utarudiwa Novemba mwaka huu 2017. Hata hivyo haijatajwa tarehe ambayo itazikutanisha tena timu hizi mbili. FIFA imetoa uamuzi huo baada ya refari wa mchezo Joseph Lamptey kuchezesha ndivyo sivyo na kwamba tayari amekabiliwa na hatua za kiniadhamu.

Soka yapigwa usiku Mogadishu

Maelfu ya mashabiki wa soka walijimwaya uwanjani kutazama mchuano wa kwanza kupigwa usiku katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, baada ya kupita karibu miongo mitatu bila kushuhudiwa mechi za usiku nchini humo. Mchuano huo uliochezwa katika Uwanja wa Konis siku ya Ijumaa, ulikuwa fainali ya mechi za klabu za vijana wenye umri kati ya miaka 16 hadi 18. Mchuano huo wa aina yake ulishuhudia timu ya Waberi ikiichabanga Hodon mabao 3-0. Meya wa Mogadishu, Tabit Abdi Mohamed ameutaja mchuano huo kuwa wa kihistoria na kwamba tukio la namna hiyo limesubiriwa na Wasomali kwa zaidi ya miaka 30.

Ramani ya Somalia

Naye Omar Ibrahim Abdisalam, Msemaji wa Shirikisho la Soka Somalia amesema mechi kama ya Ijumaa usiku mara ya mwisho ilishuhudiwa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwaka 1988. Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwezi uliopita, refa maarufu katika mchezo wa kandanda nchini Somalia alipigwa risasi na kuuawa karibu na nyumbani kwake mjini Mogadishu wakati akirejea nyumbani kwake mtaa wa Wardhigley akitokea msikitini. Osman Jama Dirah, ambaye alisimamia mechi za kanda na kimataifa aliuawa na wanaume wawili waliomfyatulia risasi kadhaa pasipo kugundulika chanzo cha watu hao kufanya hivyo.

Ligi ya Premier

Na tunatamatisha kwa kutupia jicho baadhi ya mechi muhimu za hivi karibuni za Ligi Kuu ya Soka Uingereza. Timu ya Manchester City imeibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 baada ya kuifumua bila huruma Liverpool katika mchezo wa EPL uliochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Etihad. Mabao ya Liverpool yaliwekwa kimiani na wachezaji Sergio Aguero (1), Gabriel Jesus (2) na Leroy Sane (2) ikiwa ni kipigo kikubwa kutolewa na klabu hiyo kwenye msimu huu mpya. Kipigo hicho kinahesabiwa kuwa kikubwa kwa Liverpool jijini Manchester baada ya miaka 70. Timu ya mkufunzi mkongwe Arsene Wenger pia ilijitosa uwanjani Jumamosi kwenye mbio za ushindi na kuhuisha hadhi yake kisoka. Mabao mawili ya Danny Welbeck na moja kutoka kwa Mfaransa Alexandre Lacazette yaliwawezesha kutwaa pointi tatu muhimu katika mechi yao ya nyumbani uwanjani Emirates dhidi ya Bournemouth. Matokeo hayo yameiwezesha Arsenal ambayo ilikosa huduma za kiungo Santi Cazorla kukwea hadi katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi ya Uingereza ikiwa na alama 6. Ushindi kama huu wa Gunners wa mabao 3-0 ulitwaliwa na Tottenham waliposhuka dimbani kucheza na Everton.

Liverpool iliyonyolewa kwa chupa

Katika mechi nyingine zilizopigwa Jumamosi kwenye ligi ya EPL, Manchester United walilazimishwa sare ya mabao 2-2 na Stoke City, wakati ambapo Southampon ilikuwa inapokea kichapo cha mbwa cha mabao 2-0 kutoka Watford. Burnley na New Castle zilizitandika Crystal Palace na Swansea bao 1-0 kwa usanjari huo. Man U licha ya kupigwa stop na Stoke wanasalia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa sasa, wakiwa na pointi 10, alama sawa na Man City iliyopo katika nafasi ya 2 ingawaje zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa. The Blues wanafunga orodha ya tatu bora ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza angalau kwa sasa, wakiwa na alama 9. 

………………………..TAMATI……………………

 

 

 

 

 

Tags