Dec 25, 2023 06:07 UTC
  • Ulimwengu wa Soka, Disemba 25

Hujambo mpenzi msikilizaji, natumai u bukheri wa afya. Karibu katika kipindi chako hiki ambacho hutupia jicho baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyoshuhudiwa ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia....

Unyanyuaji uzani: Iran ya 2 Asia

Timu ya taifa ya kunyanyua uzani mzito ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili katika mashindano ya mabingwa wa Asia kwenye mchezo huo yaliyofanyika nchini Malaysia. Iran imeibuka ya pili katika mashindano hayo yaliyozishirikisha nchi 20 za Asia, kwa kuzoa medali 14 za dhahabu, fedha 12 na shaba 10. Singapore imeibuka kidedea kwenye mashindano hayo yaliyofanyika mjini Johr Bahru baina ya Disemba 10-18, huku orodha ya tatu bora ikifungwa na mwenyeji Malaysia.

Sataranji; vijana wa Iran wazoa medali lukuki

Wanasataranji wa Iran wamezoa medali sita katika Duru ya 25 ya Mashindano ya Ubingwa wa Sataranji ya Vijana ya Asia. Mashindano hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Chesi wa Al-Ain katika Umoja wa Falme za Kiarabu, baina ya Disemba 12 na 22. Ramtin Kakavand ametwaa medali 2 za dhahabu katika kategoria ya Standard na Blitz kwa vijana wa kiume wenye chini ya miaka 10. Rosha Akbari ametia kibindoni medali ya fedha katika safu ya wanasataranji wa kike wenye chini ya miaka 12 mtindo wa Blitz.

 

Fedha nyingine za Iran zimetwaliwa na MohammadTaha Arkak wa kitengo cha wenye chini ya miaka 8 na Kanaan Pourmousavi safu ya vijana wa kiume wenye miaka isiyozidi 12. Kadhalika Niyousha Mohammadi ameondoka na medali ya shaba kwenya katogoria ya wanasataranjia wa kike wenye chini ya miaka 14.

Soka ya Ufkweni; Iran yakubali kichapo kutoka Senegal

Timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya wanaume ya Iran imekubali kupokea wimbi la vichapo kutoka Senegal, katika michuano ya kujinoa na kupasha misuli moto kwa ajili ya Kombe la Dunia la FIFA kwenye mchezo huo mwakani. Siku ya Ijumaa, Wairani walizabwa mabao 3-2 na vijana hao wa Kiafrika, siku mbili baada ya kuchapwa mabao 5-4. Nuksi ya vichapo kwa vijana hao wanaotiwa makali na Ali Naderi ilianza Jumanne kwa kugaragazwa maba 2-1.

 

Kombe la Dunia kwa Klabu: City bingwa

Manchester City ya Uingereza imeibuka kidedea na kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa Klabu kwa mara ya kwanza, na hivyo kuidhihirishia dunia kwa mara nyingine tena kuwa ndiyo klabu bora zaidi duniani. Man City imeifunga klabu ya Fluminense (Flu) ya Brazil mabao 4-0 katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo ambayo kila bara linawakilishwa na timu moja iliyotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa kwa bara husika. Mabao ya City Katika mchezo huo wa Ijumaa uliopigwa katika Uwanja wa Mwanamfalme Abdullah Al-Faisal uliopo mjini Jeddah nchini Saudi Arabia, yalifungwa na Phil Foden, Julian Alvarez mawili na moja la kujifunga. Msimu uliopita City ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza EPL, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA, UEFA Super Cup, na sasa FIFA Club World Cup.

 

Wakati huohuo, wapinzani wa klabu ya Yanga ya Tanzania kwenye Kundi D kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu ya Al Ahly ya Misri, imemaliza nafasi ya tatu kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwa klabu baada ya kuifunga Urawa Red Diamonds ya Japan kwa mabao 4-2. Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Mwanamfalme Abdullah Al-Faisal uliopo mjini Jeddah, mabao ya Al Ahly yalifungwa na Yasser Ibrahim 19', Perce Tau 25', Yasser Ibrahim akijifunga katika dakika ya 60, na Ali Maaloul akifunga akaunti ya mabao dakika ya 90+. Mabao mawili ya kufutia machozi ya Urawa Red Diamonds yalifungwa na wachezaji José Kante dakika ya 43 na Alexander Scholz akifunga dakika ya 54.

Ligi ya Mabingwa Afrika

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu ya Al Ahly ya Misri inaongoza Kundi D kwa pointi 5 ikicheza mechi tatu huku Yanga ya Tanzania ikishika nafasi ya pili na pointi 5 baada ya kucheza mechi 4, na hivyo kufufua matumaini ya kutinga robo fainali. Kwenye mchezo wa kwanza Ahly ikiwa ugenini ilipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga, huku ikitarajiwa kucheza mchezo wa marudiano Machi 1, 2024 na Yanga itakuwa ugenini, Cairo, Misri. Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Medeama, umeisogeza Yanga nafasi ya pili katika msimamo wa kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika, huku wakisubiri matokeo ya Al-Ahly dhidi ya CR Belouizdad. Katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, mabao ya Yanga yalifungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 33, Bakari Mwamnyeto dakika ya 61 na Mudathir Yahya dakika ya 70.  

Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza

Tunatamatisha kipindi kwa kuangazia Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, ambapo mzunguko wa kwanza wa EPL umekamilika kwa namna yake huku Arsenal ikiwa juu ya msimamo wa ligi hiyo kwa pointi 40. Raundi hiyo imekamilika kwa michezo 18, ambapo raundi ya pili itachezwa michezo yenye idadi hiyo pia. Gunners siku ya Jumapili waliilazimisha Liverpool sare ya kufungana bao 1-1 ugenini Anfield. Wabeba Bunduki walikuwa wa kwanza kufyatua risasi kupitia askari wake, Gabriel Magalhaes. Hata hivyo Mohamed Salah aliwasawazishia wenyeji katika mchuano huo wa aina yake. Liverpool inafuata nafasi ya pili ikiwa na pointi 39, sawa na Aston Villa wakiwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mohammed Salah

 

Manchester United siku ya Jumapili walichabangwa mabao 2 bila jibu ugenini waliposhuka katika Dimba la London kuvaana na West Ham, na hivyo kuzidisha masaibu ya mkufunzi Ten Hag. Mabao ya Jarred Bowen na Mohammed Kudus yalitosha kuwashusha Mashetani Wekundu hadi nafasi ya nane wakitosheka na alama 28 kwa sasa. Tottenham iliichapa Everton mabao 2-1 wikendi, huku mchuano baina ya City na Brentford ukiakhirishwa.

Chelsea siku ya Jumapili walipokezwa kichapo cha 3 mfululizo katika Uwanja wa Moleneux, mikononi mwa Wolverhampton. Mabao ya Mario Lemina na Matt Doherty yalitosha kuwapa Wolves alama tatu safi, na kuwazidishia kisunzi Chelsea. Katika Uwanja wa Craven Cottage, Rebecca Welch aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa refa katika Ligi ya EPL, katika mchuano ambao Fulham ilipokea kichapo cha maba 2-0 kutoka Burnley.  Ligi hiyo ya EPL itandelea kuroroma Jumanne hii.

……………………MWISHO……………