Dec 11, 2023 05:48 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Dec 11

Matukio muhimu ya SPOTI yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopiita, kitaifa na kimataifa....

Soka Asia; Persepolis yanyolewa na al-Duhail

Klabu ya Persepolis ya Iran imebanduliwa nje ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia baada ya kucharazwa na al-Duhail ya Qatar katika mchuano wa Kundi E wa ligi hiyo ya kibara. Katika mchezo huo uliopigwa Jumanne usiku katika Uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran, vijana wa mjini walishindwa kutumia vizuri fursa ya kuupigia nyumbani mbele ya makumi ya malefu ya mashabiki, na kufanya msemo wa mcheza kwao hutuzwa kukosa maana. Hata hivyo wenyeji hao walianza kwa kasi ya juu, kwa dakika saba baada ya kupulizwa kipyenga cha kuanza ngoma, walitangulia kucheka na nyavu kupitia goli la Shahab Zahedi. Dakika mbili baadaye, Muhammed Muntari aliwasawazishia wageni.

 

Katika kipindi cha pili, licha ya Wekundu wa Tehran kuutandaza mpira na kuumiliki kwa sehemu kubwa, lakini walishindwa kuongeza bao. Kosa kosa hizo zimewanyima tiketi ya kutinga raundi ya 16 ya ligi hiyo ya kieneo. Bao la ushindi wa al-Duhail lilitiwa kimyani kwa guu la kushoto na Mkenya, Michael Olunga aliyeufanya uwanja wa Azadi uzizime.

Maskini Persepolisi walishindwa kufurukuta nyumbani wakati huu mbaya ambapo orodha ya viwango ya Opta Power Rankings imeitangaza Esteghlal kuwa timu bora zaidi ya Iran barani Asia. Klabu bora barani hapa kwa mujibu wa orodha hiyo mpya ni al-Hilal ya Saudi Arabia, ikifutiwa na al-Nassr. Esteqlal na Sepahan zinashikilia nafasi ya sita na saba kwa uswanjari huo, huku Persepolis wakitupwa nje ya kumi bora, hadi nafasi ya 13.

 

Katika hatua nyingine, klabu ya Ittihad ya Saudia ilikwea kileleni mwa Kundi C baada ya kuizaba Sepahan ya Iran mabao 2-1 katika mchuano mwingine wa Ligi ya Klabu Bingwa Asia iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia AFC. Inaelekea kuwa ilikuwa wiki ya mikosi kwani Iran, kwani timu ya mpira wa mikono ya Jamhuri ya Kiislamu ilicharazwa 32-20 na DRC Jumamosi katika mashindano ya Handiboli ya Kombe la Rais.

Soka Barani Afrika; Uganda bingwa Cecafa U18

Timu ya taifa ya soka ya vijana ya Uganda imebuka kidedea baada ya kuichabanga Kenya mabao 2-1 katika fainali ya Mashindano ya Kandanda ya Kanda ya Afrika Mashariki na Kati Cecafa kwa vijana wenye chini ya miaka 18.

 

Katika fainali hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya siku ya Ijumaa, timu hizo mbili zilikabana koo katika kipindi cha kwanza na kushindwa kutikisa nyavu za hasimu. Wenyeji walitangulia kuona lango la wageni katika kipindi cha pili, kupitia goli la Syphas Owuor kunako dakika ya 65 ya mchezo, lakini Uganda wakasawazisha dakika 10 baadaye, kupitia Batiibwe Okello. Hakim Mutebi alivurumisha kombora lililotikisa nyavu za wenyeji, kwenye dakika za nyongeza baada ya dakika 90 za ada kuishia kwa sare ya bao 1-1, na kuifanya Uganda itwae ubingwa wa Kombe la Cecafa kwa vijana wenye chini ya miaka 18 kwa mwaka huu 2023.

Starlets ya Kenya washindwa kufuzu WAFCON

Katika hatua nyingine, timu ya taifa ya Kenya ya wanawake Harambee Starlets Jumanne, Desemba 5 ilishindwa kufuzu Kombe la Wanawake la Mataifa ya Afrika (WAFCON) baada ya kuzabwa bao 1-0 na Botswana katika raundi ya mwisho ya kufuzu kombe hilo. Botswana ilishinda kwa jumla ya magoli 2-1 baada ya sare ya 1-1 jijini Nairobi wiki iliyopita. Botswana sasa imefuzu moja kwa moja kwa WAFCON ambayo itaandaliwa nchini Morocco kwa mara ya pili mtawalia.

Ligi ya Mabingwa Afrika

Katika hatua nyingine, matokeo ya suluhu iliyoipata Al Ahly ya Misri nyumbani Cairo dhidi ya CR Belouizdad yameifanya klabu ya Yanga ya Tanzania kuwa na matumaini ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga ilipata sare ya bao 1-1 ilipovaana na Medeama ya Ghana kwenye mchezo wa tatu wa kundi D na kufikisha pointi mbili ikisalia nafasi ya mwisho kwenye msimamo. Katika mchezo wao wa Jumamosi, Yanga walisawazisha kupitia kwa Pacome Zouazoua, dakika 36 baada ya wenyeji kutangulia katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Baba Yara mjini Kumasi nchini Ghana.

Wakati huohuo, wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba walitupa karata yao muhimu usiku wa Jumamosi nchini Morocco dhidi ya Wydad Casablanca, ambapo Wekundu wa Msimbazi waliishia kulishwa bao moja la uchungu bila jibu ugenini katika Uwanja wa Marrakech. Bao hilo la vijana wa Kiarabu katika mchuano huo wa Kundi B lilifungwa na Zakaria Draoui, katika dakika za majeruhi.

Simba wamesajili sare katika michezo yote miwili waliocheza, na ushindi katika mchezo wake huo wa wikendi ungehuisha imani na matumaini ya wanamsimbazi.

Israel yaua wanamichezo wa Palestina

Israel imeua shahidi makumi ya wanariadha na wamamichezo wa Palestina tangu utawala huo wa Kizayuni uanzishe mashambulizi ya kutisha dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7. Shirika rasmi la habari la Palestina la WAFA limenukuu ripoti ya Kamati ya Olimpiki ya Palestina iliyosema kuwa “mashine ya maangamizi ya Israel” imeua wanariadha wasiopungua 47 wa timu na michezo mbalimbali tangu ilipoanzisha vita. Aidha kamati hiyo imesema maafisa 17 watendaji na wa mabenchi ya ufundi wameuawa pia katika hujumua hizo za Wazayuni dhidi ya Gaza ndani ya miezi miwili.

Jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza

 

Kwa mujibu wa kamati hiyo, miongoni mwa wanamichezo wa Kipalestina waliouawa shaidi katika hujuma hizo za utawala haramu ni Yasmine Sharaf, mwanakarate wa miaka sita aliyekuwa na azma ya kuiwakilisha Palestina katika katika majukwaa ya kimataifa ya michezo. Taarifa ya Kamati ya Olimpiki ya Palestina imeeleza kuwa, mabomu ya Israel yameshambulia na kuharibu viwanja na taasisi kadhaa za michezo za Palestina, ukiwemo Uwanja wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa UNDP, Uwanja wa Beit Hanoon pamoja na viwanja na kumbi nyingine za michezo.

Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza

Na katika Ligi Kuu ya Uingereza, klabu ya Aston Villa siku ya Jumamosi iliiondoa kileleni Arsenal kwa kuigaraza bao 1-0 na kujiongezea alama 3 muhimu. Villa wanaoneka kuamka sasa, kwani Jumatano waliwapa mabingwa watetezi Man City U kichapo laini kama hicho dhidi ya Gunners katika mchuano mwingine wa EPL.  

Man U pia, licha kuupigia nyumbani, ilipewa kichapo cha mbwa kwa kuchabangwa mabao 3-0 ilipovaana na Bournemouth.

Ilikuwa wiki ya miamba kudhalilishwa, naona pia Chelsea walitandikwa 2-0 na Everton. Liverpool ambayo iliambulia sare ya 1-1 ilipotoa kijasho na City, ipo kileleni mwa jedwali la EPL kwa sasa wakiwa na alama 37. Arsenal kwa sasa wameshushwa hadi nafasi ya pili kwenye jedwali hilo wakiwa na pointi 36, wakifuatiwa na Villa yenye alama 35, City ambao Jumapili iliichapa Laton City mabao 2-1 wanatosheka na alama 33 wakiwa katika nafasi ya nne, huku orodha ya tano bora kwa sasa ikifungwa na Tottenham ambao Jumapili waliinyoa kwa chupa New Castle kwa kuigaragaza mabao 4-1, na sasa wamefikisha alama 30.

………………….MWISHO……………