Dec 18, 2023 07:04 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Disemba 18

Mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti duniani ndani ya siku zilizopita....

Ligi Kuu ya Soka Iran; Watani wa jadi watoshana nguvu

Siku ya Alkhamisi, Uwanja wa Azadi hapa mjini Tehran ulichimbika na kutifua mavumbi wakati wa mchuano wa watani wa jadi, klabu za Persepolis na Esteqlal ambao uliishia kwa sare ya bao 1-1. Persepolis walitangulia kuona lango la mahasimu wao kupitia bao la mtoka benchi Omid Alishah. Baada ya hapo, Esteqlal iliwaweka Wekundu wa Tehran chini ya mashinikizo, lakini washambuliaji wake walishindwa kucheka na nyavu. Katika dakika za majeraha, kiungo wa kati, Arash Rezavand alichezewa ndivyo sivyo na kuangushwa na beki wa Persepolis Ali Nemati, ambapo muamizi aliamua kuipa Esteqlal penati baada ya kupewa maelekezo tata na Refa Msaidizi wa Video VAR. Ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa mashine ya VAR kutumika katika ligi kuu ya hapa nchini. Kevin Yamga alivurumisha kombora wavuni katika penati hiyo na kufanya mambo kuwa sawa bin sawa.

Image Caption

 

Mapema siku hiyo, Sepahan iliigaragaza Foolad mabao 3-1 mjini Isfahan, wakati ambapo Nassaji ilikuwa ikinyolewa na Shams Azar kwa kuzabwa mabao 2-1 huko Qazvin. Kwa matokeo hayo ya michuano ya Ligi Kuu ya Soka ya Iran (Ligi ya Wataalamu ya Ghuba ya Uajemi), Esteqlal inasalia kileleni mwa jedali, ikiwa na alama 25, pointi moja zaidi ya Sepehan ambao wana mchuano mkononi. Wekundu wa Tehran kwa sasa hawana budi kutosheka na nafasi ya tatu kwa jedwali hilo wakiwa na alama 21.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limepongeza hatua ya Iran kuruhusu wanawake kuingia uwanjani wakati wa debi la Tehran kati ya Persepolis na Esteqlal iliyoishia kwa sare ya bao 1-1. Gianni Infantiono, Rais wa FIFA amesema hatua ya Shirikisho la Soka la Iran kuruhusu wanawake 3,000 kuingia uwanjani kutazama mchuano huo ni mafanikio makubwa katika ulimwengu wa kandanda na kuongeza kuwa, hatua hiyo ni matunda ya mashauriano baina ya pande mbili. Infantino aidha amepongeza nafasi na mchango wa Iran kwa soka la bara Asia.

 

Mbali na hayo, vijana wawili wa kike wa Iran wametwaa medali mbili za dhahabu katika Mashindano ya Upigaji Makasia ya Vijana wa Asia. Kimia Zarei na Fatemeh Majlal walizidi ujuzi mahasimu kutoka Hong Kong, Kazakhstan, na Vietnam na kuibuka kidedea katika mashindano hayo ya vijana wenye chini ya miaka 23 yaliyofanyika mjini Pattaya nchini Thailand.

Na mwanataekwondo wa Kiirani, Mehran Barkhordari alituzwa medali ya dhahabu baada ya kung'ara siku ya Jumapili katika fainali ya mashindano ya Wuxi 2023 World Taekwondo Grand Slam Champions Series. Alimzidi kete hasimu wake kutoka Uzbekistan, Jasurbek Jaysunov katika kategoria ya wanataekwondo wenye kilo zisizozidi 80, na hivyo kujikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.

Riadha: Kenya yang'ara Imarati

Mwanariadha nyota wa Kenya, Brigid Kosgei aliibuka kidedea katika mbio za Abu Dhabi Marathon katika Umoja wa Falme za Kiarabu siku ya Jumamosi. Kosgei ambaye amewahi kuvunja rekodi ya dunia ya marathon, alishinda mbio hizo kwa kutumia saa 2, dakika 19 na sekunde 15, huku akiwatifuliwa mavumbi Waethiopia, Hawa Feysa na Sintayehu Athlemahu waliomaliza wa pili na wa tatu kwa kutumia saa 2, dakika 24 na sekunde 03 na saa 2, dakika 25 na sekunde 36 kwa usanjari huo.

Katika safu ya wanaume, raia wa Eritrea Amare Hailemicael aliibuka mshndi kwa kutumia saa 2, dakika 07 na sekunde 10 huku nafasi za pili na tatu zikitwaliwa na Wakenya Leonard Barsoton na Tanui Ozbilen.

Kiptum akipaisha Kiswahili kimataifa

 

Katika hatua nyingine, mwanariadha wa Kenya, Kelvin Kiptum amejizolea sifa kemkem kutoka kwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili kwa kuamua kuitumia katika kutoa hotuba yake baada ya kutawazwa kuwa mwanariadha bora zaidi wa mwaka 2023. Jijini Monaco Jumatatu iliyopita, Kiptum aliibuka na uzalendo wa kipekee kwa taifa lake la Kenya ambalo hutumia Kiswahili kama lugha ya Taifa na pia Afrika Mashariki ambako lugha hii inazidi kujipa makali.

Kiptum aliingia katika kumbukumbu za ujasiri, ueledi na ubabe baada ya kuvunja rekodi ya mbio za nyika Mjini Chicago. Hadi sasa, Kiptum anashikilia ubabe wa kuwa mwenye kasi zaidi katika mbio tatu kati ya saba ambazo ameshiriki hadi sasa. Mwanariadha nyota wa Kenya Faith Kipyegon aliitwaa taji la Mwanariadha Bora wa Kike Duniani katika tuzo hizo. 

Dondoo za Hapa na Pale Mchezaji wa kriketi wa Australia Usman Khawaja ameahidi "kupambana" na uamuzi wa bodi ya usimamizi wa mchezo huo ambayo anasema imemzuia kuonyesha ujumbe wa kuunga mkono "wale ambao hawana sauti". Akizungumza kwa hisia nzito katika mkanda wa video alioweka kwenye mtandao wake wa kijamii, Khawaja amefafanua kuwa ujumbe wake wa kuonyesha mshikamano na Wapalestina "sio wa kisiasa" na kwamba "tatizo kubwa" ni watu wanaompigia simu kumsuta kwa msimamo wake huo. Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Kriketi ya Australia alionekana akiwa amevalia buti za kriketi zenye jumbe "maisha ya watu wote ni sawa" na "uhuru ni haki ya binadamu" zilizoandikwa juu yake kwa rangi za bendera ya Palestina wakati wa mazoezi ya timu yake kabla ya mechi za mfululizo za majaribio dhidi ya Pakistan.

Sheria za Baraza la Kimataifa la Kriketi (ICC) haziruhusu wachezaji kuonyesha maneno "yasiyofuata kanuni" au nembo kwenye nguo au vifaa vinavyovaliwa wakati wa mechi za kimataifa. Hii inamaanisha kuwa Khawaja hataweza kuvaa buti hizo wakati wa mechi ya kwanza ya majaribio ya Australia dhidi ya Pakistan, iliyoanza Disemba 14. "Nitaheshimu maoni na uamuzi wao, lakini nitapambana nao na kutafuta kibali," amesema Khawaja na kuongeza kuwa, anachofanya ni kuwasemea wale wasio na sauti. Usman Khawaja amesisitiza katika mkanda huo wa video kwamba, hatua yake ni ya kuwazungumzia maelfu ya watoto wanaouawa Gaza bila kufikiriwa athari zake wala kujutiwa na kuhurumiwa na kwamba ujumbe wake haukuwa wa kisiasa kama inavyoonekana na ICC.

Takriban watoto 8,000 wameshauawa hadi sasa huko Gaza tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha mashambulio ya kinyama Oktoba 7 dhidi ya Ukanda huo uliozingirwa.

Na kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Arsenal iliicharaza Brighton mabao 2-0 na kurejea kileleni mwa msimamo wa EPL wikendi. Mara hii, risasi za Gunners ziligonga ndipo wakiupigia nyumbani Emirates Jumapili. Mabao ya Wabeba Bunduki kwenye mchuano huo yalifungwa na Gabriel Jesus katika dakika ya 53 ya mchezo kabla ya Kai Havertz kulizamisha kabisa jahazi la wageni kwa bao lake la dakika za lala salama. Kwa ushindi huo, Arsenali imerejea kileleni mwa jedwali ikiwa na lama 39, pointi moja zaidiya Liverpool ambayo wikendi ililazimishwa sare na Manchester United. Naona Mashetani Wekundu wanachekelea sare hiyo tasa na Liverpool ya Mo Salah, kwa kuzingatia kuwa, wamekuwa na msimu mbaya kwa kulishwa vichapo vya fedheha hata wanapoupigia nyumbani. Aston Villa pia ilipata ushindi laini wa mabao 2-1 iliposhuka dimbani kuvaana na Brentford, na kwa sasa inaridhika na nafasi ya tatu ikiwa na alama 38 kama Liverpool.   City kwa sasa ipo katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 34, huku mduara wa tano bora ukifungwa na Tottenham wenye alama 33.

…………………..TAMATI………………