Sep 11, 2017 15:46 UTC
  • Imam Jaafar Swadiq (as) amesema: Ndugu yangu ninayempenda zaidi ni yule ambaye ananizawadia (ananitajia aibu na mapungufu yangu) aibu zangu.
    Imam Jaafar Swadiq (as) amesema: Ndugu yangu ninayempenda zaidi ni yule ambaye ananizawadia (ananitajia aibu na mapungufu yangu) aibu zangu.

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia moja ya maudhui muhimu katika jamii nayo ni ya mkopo usio na riba yaani suna na ada nzuri ya Kiislamu ya kumkopesha mtu fedha.

Tuliashiria jinsi jambo hilo lilivyosisitizwa katika Uislamu na kuona jinsi Mtume saw alivyokuwa akifadhilisha kumkopesha mtu kuliko hata kutoa sadaka. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 88 ya mfululizo huu kitazungumzia ada na tabia nyingine nzuri nayo ni ya kutoa au kumpatia mtu adia na zawadi. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kusikiliza yale niliyokuandalieni kwa wiki hii.

Dini tukufu ya Kiislamu inasisitiza mno juu ya kuweko mahusiano na maingiliano salama baina ya wanadamu na inazingatia na kuyapa muhimu masuala kama kuwatembelea ndugu, jamaa na marafiki na kuwapelekea zawadi. Hii ni kutokana na kuwa, kumpatia mtu zawadi ni moja ya sababu za kuondoa chuki, visasi, vinyongo, adawa na uadui; na badala yake kuleta huba, upendo na kupendana. Katika Uislamu fadhila na daraja ya kutoa zawadi ni zaidi ya fadhila ya kutoa sadaka.

Sadaka yenye kuendelea

 

Adia au zawadi kama itatolewa kwa nia njema, safi na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi huwa na athari nyingi chanya kwa mtoa zawadi na mpokeaji wa zawadi hiyo na matokeo yake ni kupatikana furaha na buraha. Kimsingi ni kuwa, falsafa na siri ya kupeana zawadi ni kujenga mapenzi na kuondosha chuki, vinyongo na uadui. Mtume saw aamenukuliwa akisema: Peaneni zawadi, kwani zawadi huondoa vinyongo na kufutilia mbali chuki na uadui mkongwe.

Tukirejea mafundisho ya Kiislamu tunapata kuwa, miongoni mwa amali na matendo ambayo yametiliwa mkazo ni kuwapa watu zawadi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, madhali watu wanapendana, wanapeana zawadi, wanaheshimu na kutunza amana, basi wataendelea kubakia katika kheri na mambo mema.

Licha ya kuwa Uislamu unatilia mkazo juu ya kutoa zawadi ya kimaada na kuitaja kuwa sababu ya kukidhi mahitaji ya maisha na kupelekea kuweko huba na upendo miongoni mwa wanajamii, lakini zawadi na adia haiishii tu katika masuala ya kimaada.

Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema

 

Kwani zawadi bora kabisa katika Uislamu ni ile zawadi ambayo inakidhi hitajio miongoni mwa mahitaji ya kimaanawi na kiroho ya mwanadamu na kumfanya aliyepewa zawadi hiyo awe katika njia ya hidaya na uongofu.

Imam Jaafar Swadiq (as) amenukuliwa akisema kuwa: Ndugu yangu ninayempenda zaidi ni yule ambaye ananipa zawadi ya kunieleza aibu na mapungufu yangu.

Katika hadithi hii Imam Swadiq (as) hakutumia ibara ya mwenye kunitajia aibu zangu bali ametumia neno mwenye kunizawadia aibu zangu. Hii inaonyesha kwamba, mtu anaekueleza mapungufu yako huwa amekupa zawadi nzuri nayo ni ya uongofu.

Yumkini katika maisha tunayoishi baadhi ya watu wakachukia na kukasirika pale wanapoelezwa aibu na mapungufu yao. Lakini ukweli unabakia pale pale kwamba, anayekutajia aibu na mapungufu yako huwa amekupa zawadi katika njia na harakati ya ukamilifu na jambo hili lina umuhimu mno.

Katika hadithi nyingine Mtume (saw) amenukuliwa akisema kuwa, zawadi bora kabisa ambayo Mwislamu anaweza kumpatia ndugu yake ni maneno ya hekima ambayo kupitia kwayo Mwenyezi Mungu amuongezee hidaya na uongofu au amuokoe kunako kuangamia na kupotea.

Mafundisho ya Kiislamu sambamba na kusisitiza juu ya thamani ya zawadi na kutoa zawadi yanatilia mkazo pia juu ya kupokea zawadi hata kama itakuwa ndogo kiasi gani. Mtume (saw) anaitambua na kuihesabu zawadi kuwa ni riziki ya Mwenyezi Mungu na alikuwa akipokea kwa moyo mkunjufu kila zawadi aliyokuwa akipatiwa na alikuwa akisema: Miongoni mwa ishara za mtu kumheshimu ndugu yake ni kuipokea zawadi anayompatia. Katika hadithi nyingine Mtume (saw) amenukuliwa akisema maneno ambayo yanaonyesha adhama na heshima yake kubwa kwa mtoa zawadi pamoja na kuthamani zawadi. Anasema kuwa: Hata kama nitapatiwa zawadi ya miguu ya ng'ombe au kondoo nitaipokea.

 

Baadhi ya wafasiri wanasema kuwa zawadi ya miguu ya kondoo haikuwa imezoeleka katika zama hizo. Hivyo wanasema kwamba, Mtume (saw) ameitaja miguu ya kondoo ili kusisitiza umuhimu wa kutoa na kupokea zawadi.

Kutokana na hadith hizo, tunaona kuwa, kupeana zawadi ni jambo linalohamasishwa sana bila kuangalia ukubwa au thamani ya zawadi husika. Kwa sababu mabadilishano ya zawadi huongeza upendo, huondosha wasiwasi na kuimarisha hali ya ukaribu miongoni mwa watu.

Zawadi ndogo ni ushahidi wa upendo wa dhati, kwa kuwa sio mzigo kwa mtoaji, haina gharama kubwa na ni rahisi kwa mtoaji.

Inasimuliwa kwamba, siku moja mwanamke mmoja masikini alimletea zawadi Bi Aisha mke wa Bwana Mtume (saw). Hata hivyo Bibi Aisha aliikataa zawadi hiyo kwa kumuonea huruma mwanamke yule. Baada ya Bwana Mtume (saw) kunukuliwa kisa hicho alihuzunuika sana na kumwambia mkewe, kwa nini hukuipokea zawadi yake? Je unajua kwamba, hatua yako hiyo ya kuikataa zawadi yake umemdunisha na kumdhalilisha?

Kwa hakika kuwapa zawadi ndugu na jamaa ni miongoni mwa mifano ya wazi ya kuunga udugu jambo ambalo limeashiriwa katika Kitabu cha Qur'ani. Mtu kwa kumpa zawadi ndugu yake anaweza kwa urahisi kabisa kuwafanya watu wampende na hivyo kuujaza moyo wake joto la huba, huruma na mapenzi. Hata hivyo adia au zawadi sio maalumu kwa ndugu na jamaa au watu wa karibu tu, bali mtu anaweza kumpatia zawadi rafiki yake bali hata kuwatumia zawadi maadui zake.

Nukta nyingine ambayo ni lazima kuizingatia katika utoaji zawadi ni mtu kufanya hivyo na kutokuwa na matarajio kutoka kwa aliyempatia zawadi. Hapana shaka kuwa, mtu anayepokea zawadi ana jukumu la kulipa wema na hisani hiyo kadiri anavyoweza ili kwa njia hiyo aweze kudumisha urafiki na ndugu yake huyo; lakini jambo la msingi ni kwamba, tunapotoa zawadi hatupaswi kuwa na matarajio kwamba, madhali tumempatia zawadi mtu fulani basi lazima na yeye atupatie adia na hiba kama tulivyofanya sisi.

 

Imam Ali bin Abi Twalib as amenukuliwa akisema maneno yenye hekima kubwa kwamba: Nenda ukamtembelee mtu ambaye yeye hakutembelei na mpatie zawadi mtu ambaye yeye hakupatii zawadi.

Kupitia maneno haya tunafahamu kwamba, hupaswi kuacha kumpatia zawadi mtu fulani eti kwa sababu umeshampatia zawadi mara kadhaa lakini yeye hajafanya hivyo. Katika jamii tunazoishi kuna watu huwa hawako tayari kumpa mtu zawadi au kumtendea wema fulani isipokuwa na yeye anataraji kufanyiwa kama alivyofanya yeye. Mafundisho ya Uislamu hayaamrishi mwenendo kama huu.

Aidha zawadi ziko za aina mbalimbali na ni jambo ambalo lipo katika tamaduni na ada za kila kaumu na jamii. Kadhalika thamani na aina ya zawadi inatofautiana kulingana na jamii na utamaduni wa watu fulani.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nakomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu. Bila shaka mmenufaika vya kutosha ninakuageni nikitaraji kukutana nanyi tena wiki ijayo panapo majaaliwa Yake Mungu. Kwaherini.