Sep 23, 2017 02:33 UTC
  • Jumamosi, Septemba 23, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe Pili Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria mwafaka na tarehe 23 Septemba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita, yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia yake waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo. Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka baada ya kukataa kutoa kiapo cha utii kwa utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq. Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini walibadilisha msimamo na wakaaacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya. ***

Harakati ya Imam Hussein (as)

Miaka 342 iliyopita katika siku kama ya leo, Valentin Conrart mwandishi na mwanafasihi wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 72. Alizaliwa mwaka 1603 katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na fasihi ya lugha na kwa msingi huo ndio maana alipokuwa katika rika la ujana, Valentin Conrart akawa na mapenzi na taaluma ya fasihi ya lugha na taratibu akaanza kujihusisha na fani ya uandishi.***

Valentin Conrart

Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita sawa na tarehe Mosi Mehr 1281 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Imam Ruhulllah Khomeini (MA)

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, Saudi Arabia iliasisiwa, na Abdulaziz bin Saud akawa mfalme wa nchi hiyo. Nchi hiyo ina miji mitakatifu ya Makka na Madina na Mtume wa Uislamu Muhammad SAW alizaliwa katika mji wa Makka. Tangu mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria, Saudi Arabia iliondoka chini ya himaya ya utawala wa Bani Abbas na hali ya mambo ya nchi hiyo haikuwa shwari kwa karne kadhaa. Serikali ya Othmania iliivamia Saudi katika karne ya 16 Miladia na kuanzia katikati mwa karne ya 17 ukoo wa Aal Saud ulianza kufanya juhudi za kuiongoza nchi hiyo na jitihada hizo ziliendelea hadi mwanzoni mwa karne ya 20.***

Bendera ya Saudi Arabia

Na miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili raia wa Austria. Sigmund alizaliwa mwaka 1856. Daktari huyo alifanya utafiti na kuchunguza matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kwa sababu hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis. ***

Sigmund Freud

 

Tags