Jumatano, Oktoba 4, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 13 Muharram 1439 Hijria sawa na 4 Oktoba 2017.
Tarehe 13 Muharram mwaka wa 61 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 1378 iliyopita Abdullah bin Afif aliuawa shahidi na gavana wa Yazid bin Muawiya, Ubaidullah bin Ziad. Afif alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha malalamiko na upinzani wa waziwazi dhidi ya jinai za Ubaidullah bin Ziad za kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as). Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kuwashambulia kwa maneno makali na kuwavunjia heshima mateka wa Karbala waliokuwa wamepelekwa katika majlisi yake, Abdullah bin Afif ambaye alikuwa miongoni mwa wachamungu wakubwa wa mji wa Kufa huko Iraq na wafuasi wa kweli wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as), alikerwa mno na mwenendo huo wa gavana wa Yazidi wa kuwavunjia heshima Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kumjibu mtawala huyo kwa hasira. Ubaidullah ambaye hakutarajia kuona majibu kama hayo baada ya kuua watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alitoa amri ya kukamatwa Afif na kupelekwa kwake. Hata hivyo watu wa kabila lake walizuia kitendo hicho. Askari wa utawala wa Bani Umayyah walivamia nyumba ya Abudullah bin Afifi usiku na kumtoa nje kisha wakamuua shahidi kwa kumkata kwa mapanga.
Siku kama ya leo miaka 187 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru wake. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.
Tarehe 4 Oktoba ya leo miaka 89 iliyopita, tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu nchini Uingereza, alizaliwa tarehe 6 Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa, askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe 4 Oktoba mwaka 1928, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.
Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikaanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputnik 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini.
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Lesotho ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Kabla ya uhuru, Lesotho ilikuwa ikijulikana kwa jina la Basutoland na kuanzia mwaka 1884 ikawa chini ya mkoloni Mwingereza. Uingereza iliendelea kuikalia kwa mabavu Lesotho hadi mwaka 1966 na hatimaye nchi hiyo ikapata uhuru kamili katika siku kama ya leo. Lesotho iko kusini mwa bara la Afrika huku ikiwa imezingirwa na jirani yake Afrika Kusini.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, serikali ya Kuwait ilikataa kumpa Imam Khomein idhini ya kuishi nchini humo na hivyo akalazimika kuelekea nchini Ufaransa. Hatua ya Imam kuelekea Paris ilikuwa sababu ya kuharakisha mwenendo wa mafanikio ya Mapinduzi nchini Iran, kinyume kabisa na matarajio ya dikteta Saddam wa Iraq na Mohammad Reza Pahlavi, mfalme kibaraka wa wakati huo wa Iran ambao waliamini kwamba, kwa kumbaidisha Imam Khomein (MA) wangekuwa wameua harakati zake za kimapinduzi. Akiwa mjini Paris, Imam aliishi katika kijiji cha Neauphle-le-Château, kilometa 50 kutoka mji huo, ambapo aliendeleza harakati zake za kimapinduzi kupitia barua na kanda za sauti kwa wanamapinduzi nchini Iran.