Nov 05, 2017 09:09 UTC
  • Jumapili, Novemba 5, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 16 Mfunguo Tano Safar 1439 Hijria, sawa na tarehe tano Novemba, 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita alifariki dunia James Clerk Maxwell, mwanafizikia maarufu na mwasisi wa kanuni ya mwanga na umeme. Maxwell alizaliwa Scotland tarehe 13 Novemba mwaka 1831 Miladia. Mwaka 1871 Miladia, alitoa kitabu chake kwa jina la 'Umeme na mvuto wa sumakuu 'Magnetism'. Haukupita muda mrefu mara akateuliwa kuwa muhadhiri wa elimu ya fizikia katika chuo kikuu cha Cambridge, nchini Uingereza. Katika kitabu chake aliweza kubainisha kwa namna nzuri radiamali na taathira nne mkabala na upeo wa kielektroniki na nguvu ya sumakuu sambamba na kufanikiwa kugundua kanuni ya mwanga na umeme na hivyo kumfanya aitwe lakabu ya elimu hizo.

James Clerk Maxwell

Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita, alizaliwa Will Durant, mwandishi, mwanafalsafa na mtaalamu wa historia wa jimbo la Massachusetts, nchini Marekani. Baada ya kuhitimu hatua kadhaa za kielimu, alifanikiwa kuchukua shahada ya PHD katika uga wa falsafa huku akiteuliwa pia kuwa muhadhiri. Mwaka 1914 Miladia, aliasisi shule moja mjini New York ambayo aliiongoza kwa karibu miaka 13. Mwaka 1926 Miladia Will Durant alitoa kitabu cha masuala ya historia ya falsafa ambapo mafanikio makubwa ya kitabu hicho yalimfanya aweze kukubalika sana kuhusiana na masuala ya historia. Ni kwa ajili hiyo ndio maana ili kuandaa nyaraka za kihistoria na kufanya utafiti zaidi alilazimika kufanya safari tatu kuizunguka dunia. Hatimaye aliandika kitabu kingine cha juzuu kumi ambapo humo aliashiria masuala muhimu na hivyo kuwavutia wengi. Kitabu hicho kilitarjumiwa kwa lugha 12 za dunia. Will Durant alifariki dunia tarehe 9 Novemba 1981, akiwa na umri wa miaka 96.

Will Durant

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, yaani tarehe 5 Novemba mwaka 1944, Dakta Alexis Carrel, mwanabiolojia na mwanafalsafa wa Kifaransa aliaga dunia. Alizaliwa Juni 28 mwaka 1873 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwaka 1912 Dakta Carrel alitunukiwa tuzo ya heshima ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa katika uwanja wa tiba. Alitumia kipindi fulani katika maisha yake kutalii na kuzitembelea nchi mbalimbali zikiwemo za Kiislamu na kushuhudia kwa karibu mila na tamaduni za nchi hizo. Kwa sababu hiyo Dakta Alexis Carrel amesisitiza mno katika maandishi na vitabu vyake juu ya umuhimu na nafasi ya dini na masuala ya kiroho katika maisha ya mwanadamu. Nadharia nyingi za msomi huyo zimo katika kitabu mashuhuri alichokipa jina la "Mwanadamu, Kiumbe Asiyefahamika," ambamo ndani yake anapinga demokrasia ya Kimagharibi.

Dakta Alexis Carrel

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, wakati wa kuendelea harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala dhalimu wa Shah, serikali ya Sharif Emami ililazimika kujiuzulu. Jafar Sharif Emami alikuwa kibaraka wa ukoloni wakati wa kupamba moto harakati za wananchi Waislamu na alikuwa akitoa ahadi za uongo kwa lengo la kupotosha mwelekeo wa Mapinduzi ya Kiislamu. Baada ya Sharif Imami, Jenerali Azhari aliunda serikali ya kijeshi. Hata hivyo Imam Khomeini aling'amua njama na hila za kiongozi huyo na kutangaza kwamba, mawaziri wakuu wanaobadilishwa ni vibaraka wa Shah na ubeberu na akawataka wananchi wasihadaike na hila za viongozi hao bali waendeleze harakati za mapambano za kutaka kuangusha utawala dhalimu wa Shah.

Sharif Emami

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, kulifunguliwa maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya vitabu mjini Tehran. Maonyesho hayo yalishirikisha makampuni na taasisi 196 za uchapishaji vitabu za kigeni kutoka nchi 32 duniani yaliyokuwa na vitabu zaidi ya elfu 16. Vilevile taasisi 215 za uchapisha za ndani ya Iran zilishiriki katika maonyesho hayo. Tangu mwaka huo maonyesho ya kimataifa ya vitabu ya Tehran yamekuwa yakifanyika kila mwaka hapa nchini.

Maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya vitabu mjini Tehran

Na siku kama ya leo miaka mitatu iliyopita, alifariki dunia George Jordac, mwandishi na malenga mkubwa wa Kikristo aliyeandika kitabu cha 'Imamu Ali Sauti ya Uadilifu wa Mwanadamu'. Jordac alizaliwa mwaka 1926 Miladia mjini Marjayoun, Lebanon. Alikuwa muhadhiri katika elimu ya fasihi na falsafa ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Bairut. Aliandika vitabu 30, muhimu zaidi kikiwa ni kitabu hicho cha 'Imamu Ali Sauti ya Uadilifu wa Mwanadamu' chenye juzuu tano. Akielezea sababu ya yeye kuandika juu ya shakhsia ya Imam Ali (as) na si mtu mwingine yeyote yule anasema: "Watu wengi wa nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi na Misri walinipa mapendekezo ya kwa mfano, niandike kuhusu maisha ya makhalifa wengine wa Kiislamu. Lakini mimi sikukubali. Sisemi kwa sababu hao wengine walikuwa ni wabaya, la hasha! Bali ni kwamba sikuona mtu mwingine bora na aliyefaa kuzungumziwa kama Imamu Ali-as-. Hii ni kwa kuwa mapinduzi ya mtukufu huyo yalikuwa mapinduzi ya kibinaadamu, kijamii, kifikra na kiutamaduni….."

George Jordac

Tags