Nov 21, 2017 06:44 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (91)

Ni wasaa na wakati mwingine wa kuwa nanyi wapenzi wasikilizaji katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la kuhifadhi na kulinda heshima ya Muumini. Tulisema kuwa, moja ya mafundisho muhimu ya dini tukufu ya Kiislamu ni udharura wa kulidha na kuhifadhi heshima ya watu wengine.

Aidha tulibainisha kwamba, kuhifadhi na kuchunga heshima na itibari ya Muumini ni jambo muhimu kiasi kwamba, hatua ya mtu kuharibu heshima ya wengine inahesabiwa kuwa miongoni mwa madhambi makubwa kabisa na Mwenyezi Mungu ameahidi kumpatia adhabu kali yule anayechafua na kuharibu heshima ya wengine.

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 91 kitazungumzia dhuluma na jinsi suala la kudhulumu lilivyokemewa katika Uislamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.

*******

Dini tukufu ya Kiislamu imewakataza wafuasi wake wasisalimu amri mbele ya dhuluma na inawashajiisha wasimamwe na kupambana na dhalimu kwa nguvu zao zote.

Dhulma na uonevu vimewagawanyika katika sehemu mbalimbali ambapo katika dini ya Kiislamu, dhuluma za aina zote zimekatazwa na kupigwa marufuku.  Moja ya aina ya dhuluma ni mtu kujidhulumu mwenyewe. Dhuluma hii ni ile dhambi na hatua ya mtu kuasi na kukiuka maamrisho ya Mwenyezi Mungu na hivyo mhusika kufanya uzembe katika harakati ya kuelekea katika njia ya ukamilifu.  Dhuluma ya aina hii imezungumziwa katika aya ya kwanza ya Surat Talaq pale Mwenye Mungu aliposema:

Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake.

Dhulma ya aina nyingine ni kuwadhulumu watu. Dhulma hii maana yake ni kumdhuru mtu mwingine na kumuudhi kupitia kumpiga, kumtusi, kummua, kumtuhumu, kumsengenya, kuvamia na kupora mali na kumvunjia heshima na kumuharibia itibari yake; mambo ambayo yana taathira mbaya mno. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anaashiria athari mbaya za dhulma na anawanasihi Waislamu na kuwataka wajiepusha na jambo hilo kwa kusema:

Jitengeni mbali na dhulma; kwani dhulma ni uhalifu mkubwa na ambao ni katika madhambi makubwa kabisa.

Katika hadithi moja Bwana Mtume saw amenukuliwa akizungumzia namna mtu aliyedhulumiwa yaani madhlumu atakavyochukua haki yake kutoka kwa dhalimu. Anasema kuwa: Siku ya Kiyama ataingia mja katika uwanja waliokusanywa watu kwa ajili ya hesabu huku akiwa na furaha kutokana na amali njema alizofanya. Kisha atajitokeza mtu mwingine na kusema: Ewe Mwenyezi Mungu, Bwana huyu alidhulumu mimi. Kisha amali za mtu aliyedhulumu zitachukuliwa na kuongezewa katika fungu la amali njema za mja aliyedhulumiwa. Hivyo hivyo watu waliodhulumiwa na Bwana huyo wataendelea kujitokeza na kila mtu kupatiwa fungu fulani kutoka katika fungu la amali njema za dhalimu yule. Hali itaendelea hivyo hadi kufikia Bwana yule aliyekuwa akidhulumu watu hapa duniani kutobakiwa na amali hata moja njema. Baada ya hapo kila anayetokea na ambaye amedhulumiwa, hupunguziwa katika mabaya yake na kuongezewa dhalimu. Dhalimu yule ataendelea kuwa mdaiwa wa watu mpaka anaingizwa katika moto wa Jahanamu.

 

Wapenzi wasikilizaji, katika mafundisho ya Kiislamu mbali na dhulma kukatazwa, na watu kutakiwa wajiepushe na kutenda dhulma, wanapaswa pia kutomsaidia dhalimu na wala kutoridhia dhulma.

Imam Ali bin Abi Twalib as anasema katika mlango wa kuwasaidia madhalimu kwamba: Anayetenda dhulma, anayemsaidia na anayeridhia dhulma wote watatu ni washirika.

Kupitia hadithi hii tunafahamu kwamba, si kutenda dhulma tu ndio jambo baya na lililokatazwa katika Uislamu, bali hata kumsaidia dhalimu au kuridhia dhulma nako hakuna tofauti na kutenda dhulma.

Imam Jafar Swadiq as anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Kila ambaye anapenda madhalimu wabakie atakuwa amependa kumuasi Mwenyezi Mungu na kukiuka maamrisho yake.

Safwan bin Mihran alikuwa mmoja wa wafuasi na vipenzi wa Imam Mussa Kadhim (as). Safwan alikuwa ana miliki ngamia wengi na alikuwa akiwakodisha ngamia wake kwa watu wengine na kujiingizia kipato. Siku moja alikwenda kwa Imam Mussa bin Jaafar al-Kadhim (as). Imam alipomuona akasema, Ewe Safwan mambo yako yote ni mazuri, isipokuwa jambo moja. Safwan akauliza, ni jambo gani hilo Ewe Imam? Imam Kadhim as akamwambia, kumkodishia ngamia wako Harum Rashid, Khalifa dhalimu wa ukoo wa Bani Abbas. Safwan akasema: Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, mimi sijawakodisha ngamia wangu kwa ajili ya dhambi, kuwinda au kazi isiyo na maana. Harun Rashid amewakodisha ngamia wangu kwa ajili ya kwenda Hija. Isitoshe mimi siambatani nae, bali mfanyakazi wangu ndiye ninayemtuma. Imam Kadhim as akamuuliza Safwan, je unapenda abakie hai ili aendelee kukodisha ngamia wako na wewe upate fedha? Safwan, akasema, ndio. Imam akasema: Kila ambaye anapenda madhalimu wabakie ni katika wao na kila atayekuwa miongoni mwao basi ni mtu wa motoni. Safwan anasimulia kwamba, baada ya kusikia maneno hayo ya Imam Kadhim as aliondoka na kwenda kuuza ngamia wake wote. Baada ya Harun Rashid kusikia habari hiyo alimuuliza sababu ya kufanya hivyo. Safwan anasema: Nikamjibu Harun Rashid kwa kumwambia nimekuwa mzee na wafanyakazi wangu hawafanyi kazi vizuri kama inavyotakiwa. Hata hivyo Harun Radhuid akasema: Hapana, mimi ninafahamu ni nani aliyekupa muongozo na si mwingine bali ni Mussa bin Jaafar al-Kadhim (as). Licha ya Safwan kujitahidi kumuonyesha Harun kwamba, hana uhusiano na Imam Mussa al Kadhim as, Harun Rashid hakukubaliana na utetezi wake huo. Hata hivyo alimwambia Safwan kwamba: Ninaapa kwa Mola, lau kama si wema ninaoufahamu kutoka kwako basi nisingesita kukuua.

 

Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 72 ya Surat al-Anfal:

Na wale walio amini lakini hawakuhama, nyinyi hamna wajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.

Kupitia aya hii tukufu tunafahamu kwamba: Waislamu wanatakiwa kuwasaidia ndugu zao katika dini ambao wamedhulumiwa na kufanya hivyo ni jukumu lao la kidini.

Hii leo kama ambavyo tunashuhudia Waislamu katika maeneo mbalimbali wanakabiliwa na dhulma hasa Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar, ni jukumu la Waislamu popote walipo kuwasaidia wenzao hao kwa hali na mali. Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, mtu ambaye atasikia sauti ya kutaka msaada ikisema, Enyi Waislamu nisaidieni! Na kisha kutoitikia hilo, basi si katika Waislamu.

Aidha katika wosia wake kwa wanawae Hassan na Hussein, Imam Ali bin Abi Twalib anawaambia: Kuweni adui wa dhalimu na na wenye kumsaidia madhlumu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha Hadithi ya Uongofu umefikia tamati kwa leo, tukutane tena wiki ijayo, siku na wakati kama wa leo.