Hadithi ya Uongofu (95)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu, kipindi ambacho hujadili maudhui mbalimbali za kijamii, kidini na kimaadili na kukunukulieni miongozo na hadithi kutoka kwa Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu as kuhusiana na maudhui hizo. Kama mnakumbuka kipindi chetu kilichopita kilijadili maudhui ya hasira na ghadhabu na kubainisha madhara ya jambo hilo.
Tulisema kuwa, hasira inapaswa kuwa na hali ya uwiano; kwani kama itatoka katika hali ya kati na kati na uwiano, basi hugeuka na kuwa moja ya tabia na mienendo mibaya kabisa ya kimaadili. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 95 ya mfululizo huu kitazungumzia namna ya kuzuia na kudhibiti hasira. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache.
*******
Moja ya sifa muhimu za waja waumini ni kudhibiti hasira zao na kusamehe makosa ya wengine. Mafundisho ya Kiislamu yanawataka wafuasi wa dini hii kudhibiti na kuzuia hasira zao. Sifa hii ya kuzuia na kudhibiti hasira imekokotezwa na kutiliwa mkazo katika Suna na hadithi za Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu as. Fauka ya hayo, Mwenyezi Mungu amemuandalia ujira mnono mtu ambaye anaudhiwa na kukasirishwa kisha akadhibiti na kuzuia hasira zake hasa pale anapokuwa na uwezo kurejesha na kulipiza kitendo alichofanyiwa ambacho kilipelekea akasirike iwe ni kubughudhiwa, kutusiwa au kitendo kingine chochote cha maudhi.
Mtume Muhammad saw amenukuliwa katika moja ya hadithi akisema kuwa: Kila mwenye kuzuia na kudhibiti hasira hali ya kuwa ana uwezo wa kulipiza alilotendewa, lakini akawa ni mwenye subira, Mwenyezui Mungu atamlipa ujira wa shahidi.
Moja ya njia na mbinu za kuzuia na kudhibiti hasira ni kujipamba kwa sifa na tabia nzuri ya subira na uvumilivu.
Subira na uvumilivu humpa mtu nguvu ya kuzuia hasira. Ili mtu apate utulivu na afikie sifa ya subira na uvumilifu na hivyo kuweza kuzuia na kudhibiti hasira zake, kumetajwa njia mbalimbali kwa ajili ya jambo hilo. Moja ya mbinu na mkakati wa hilo ni kuonyesha huba na urafiki. Inaelezwa kuwa, unapoona mtu katika watu wako wa karibu ameshikwa na hasira msogelee na umliwaze kwa kumpangusa na kumgusagusa, kwani kugusana mwili na watu wako wa karibu huwa sababu ya kupatikana utulivu.
Wataalamu wanasema kuwa, wakati mtu anaposhikwa na hasira, joto la mwili wake hupanda na hali hiyo hupelekea kuongezeka kasi ya mzunguko wa damu. Katika hali hii, uwezo wa kufikiri mtu hupungua. Katika hatua kama hii, kunywa maji ya baridi au kuosha uso kwa maji ya baridi hupunguza hasira na hufanya kiwango cha joto la mwili kushuka.
Na hapo mtu hupata fursa ya kutafakari kuhusiana na matokeo mabaya ya kufanya chuki na ugomvi au kujihusisha na vitendo vya utumiaji mabavu. Mtume saw anasema kuwa: Mmoja wenu anapopandwa na hasira aoshe uso wake kwa maji ya baridi, kwani hasira inatokana na moto, na moto hauzimishwi isipokuwa kwa maji.
Ukweli ni kuwa, kutokana na mtu kuishi katika jamii ya watu wa aina mbalimbali bila shaka huenda akakumbwa na mambo ambayo yatamchukiza na kumkasirisha kwani miamala ya baadhi ya wanajamii huwa kinyume na utu, insafu na uadilifu. Muhimu ni mtu kutotoa fursa matendo ya wengine yamuudhi na kupandisha hasira. Ukiruhusu matendo ya wengine yakukasirishe, hiyo itamaanisha kwamba wao ndio wanaokuamulia jinsi utakavyohisi.
Kwa nini usijitahidi kuonyesha kwamba, wewe ni mkomavu kwa kumsamehe aliyekukosea? ” Ukifanya hivyo, utakuwa umefaulu kudhibiti hasira yako badala ya kuiruhusu hasira ikudhibiti. Njia ya nyingine ya kudhibiti na kukabiliana na hasira ni kama ilivyokuja katika baadhi ya hadithi zinaoeleza kuwa, wakati mtu anaposhikwa na hasira ambapo shetani huwa karibu nae, anapaswa kujikinga na Mwenyezi Mungu na akithithirishe kusema:
اَعُوْذُ بِاللّهِ مِنَ الشَّیْطانِ الرَّجِیْمِ
Yaani, najikinga kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya shetani mlaaniwa aliyetengwa mbali.
Aidha katika baadhi ya hadithi nyingine inaelezwa kuwa, mtu anaposhikwa na hasira atamke maneno haya:
لا حَولَ وَ لا قُوَّةَ اِلاّ بِاللّهِ الْعَلِىَّ الْعَظِیمِ
Yaani, hapana uwezo wala nguvu ila za Mwenyezi Mungu". Kutamka maneno haya husaidia kuondoa hasira.
Njia nyingine ya kudhibiti na kukabiliana na hasira ni mtu kufanya mabadiliko ya kimwili yaani kama alikuwa amesimama akae na kama alikuwa amekaa alale. Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa:
Mmoja wenu anaposhikwa na hasira kama amesimama na akae, na kama amekaa basi alale na kama hasira zake hazitashuka basi na atie udhu kwa maji ya baridi au aoshe mwili wake.
Kuhusiana na jambo hilo, Imam Muhammad Baqir as pia amesema: Wakati mtu anaposhikwa na hasira kama amesimama basi akae mara moja na kama amekaa basi na aamke haraka, ili uchafu na ushawishi wa shetani ujitenge na yeye.
Kwa hakika watu wenye hasira na waliopandwa na ghadhabu wanapaswa kufikiria athari mbaya za jambo hilo kabla ya moto wa hasira kuwaka na kukolea na hivyo kuzingira nyoyo zao. Hali hiyo inapaswa kuwakumbusha daima kwamba, kukasirika na kughadhibika kusiko na maana ni moto ambao yumkini ukaunguza imani na saada zao. Kwa hakika kukasirika huongeza moto wa ghadhabu za Mwenyezi Mungu duniani na akhera. Hasira pia humuweka mbali mtu na marafiki na kuwafurahisha maadui. Aidha hasira na ghadhabu zinapunguza umri wa mtu na kuhatarisha usalama wa afya yake.
Kwa hakika kimsingi tatizo hujitokeza pale mtu anaposhindwa kuzuia hasira zake na kuchukua hatua ya kuingia katika ugomvi na watu pasina sababu hasa ya msingi. Bila shaka hasira isiyo na mipaka au hasira iliyojaa taasubi na ujahili hupelekea kutokea vurugu na ugomvi wenye madhara na majuto ndani yake. Kutozuia hasira ni sawa na ugonjwa, usipouzuia na kuutibu unaweza kuwa na madhara. Kwa hakika njia bora ya kuondoa hasira ni msamaha. Kuwa tayari kusamehe na kusahau.
Tunahitimisha kipindi chetu cha leo kwa kukunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na ghadhabu na hasira.
Imam Jafar Swadiq as amesema: Jiepusheni na ghadhabu, kwani huleta mashaka.”
Imam Ali as amesema: Tuliza ghadhabu zako na kumsamehe mtu aliyekukosea wakati wewe ukiwa na uwezo au cheo chako.
Imam Jafar Swadiq as: Ghadhabu ni kitu kinachoteketeza moyo wa mwenye hekima; kwani yeyote yule asiyeweza kudhibiti vyema ghadhabu zake basi kamwe hawezi kuitumia busara yake.
Aidha Imam Swadiq as amesema:
Ghadhabu ni ufunguo wa kila aina ya shari.
Na hadi hapa ndio tunafuikia mwisho wa kipindi chetu kwa juma hili. Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa yake Mola.