Dec 25, 2017 09:49 UTC

Sura ya As-Sabaa, aya ya 6-9 (Darsa ya 762)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 762 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 6 na 7 ambazo zinasema:

وَيَرَى الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ الَّذِي أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ هُوَ الْحَقَّ وَيَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ

Na walio pewa ilimu wanaona ya kuwa uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi ni haki, nayo huongoa kwendea njia ya Mwenye nguvu, Mwenye kusifiwa.

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا هَلْ نَدُلُّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ يُنَبِّئُكُمْ إِذَا مُزِّقْتُمْ كُلَّ مُمَزَّقٍ إِنَّكُمْ لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ

Na walio kufuru walisema: Je! Tukujuulisheni mtu anaye kuambieni kwamba mtakapo chambuliwa mapande mapande mtakuwa katika umbo jipya?

Aya tulizosoma katika darsa iliyopita ziliwazungumzia watu waliokuwa wakikanusha kufufuliwa viumbe, yaani Maadi na wakawa wanajaribu kuwapotosha na watu kwa kuzikadhibisha aya za Mwenyezi Mungu. Aya hizi tulizosoma zinasema: watu wenye ilimu na wenye kufikiri wanazitafakari na kuzizingatia aya ulizoteremshiwa ewe Mtume na kubaini kuwa ni haki. Wao wanafikia kwenye hitimisho kwamba njia sahihi ya kuufikia uongofu wa Allah ni kuziamini na kuzifuata aya za Qur'ani tukufu. Katika zama za Bwana Mtume Muhammad SAW baadhi ya maulamaa wa Ahlul Kitab walioamua kuachana na taasubi na kutohukumu mambo kiupendeleo walisilimu na kumwamini Mtume huyo wa haki. Katika kipindi chote hiki cha historia pia tangu ulipodhihiri Uislamu, kuna wasomi na wanasayansi wengi ambao baada ya kutafiti na kutalii aya za Qur'ani wamekiri juu ya ukweli na adhama yake wakaamua kuwa wafuasi wa Uislamu na waumini wa Kitabu hicho cha mbinguni. Lakini mkabala na watu hao, daima wamekuwepo pia watu ambao huibua mjadala wa kufufuliwa viumbe ili kuikadhibisha Qur'ani na Utume wa Nabii Muhammad SAW. Wao husema kwa kejeli na istihzai: Huyu Muhammad ndiye mtu anayedai kwamba baada ya wanadamu kuoza makaburini na kugeuka udongo watatolewa tena kwenye udongo huo na kuanza maisha mengine mapya. Kwa kuwa watu hao hawawezi kukanusha kuwepo asili ya ulimwengu na asili ya mwanadamu huamua kukadhibisha maadi na ufufuo wa viumbe. Wao wanafanya hivyo ili kuwashawishi watu wasimwamini Bwana Mtume wala wasiyakubali maamrisho ya dini. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kinyume na mtazamo wa watu wanaoamini kuwa dini ni matokeo ya ujinga na ujahili wa watu, wasomi na wataalamu wengi katika kipindi chote cha historia wamekiri na kuukubali ukweli wa dini tukufu ya Uislamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa njia ya Mitume huwapa izza na heshima waumini duniani. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba wapinzani wa njia ya Mitume, badala ya kutegemea akili na mantiki wanajaribu kutumia mbinu ya kudunisha na kukejeli kuchafua shakhsia za Mitume mbele ya macho ya watu ili asitokee mtu akawaamini waja hao wateule.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 8 na ya 9 ambazo zinasema:

أَفْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَم بِهِ جِنَّةٌ ۗ بَلِ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ فِي الْعَذَابِ وَالضَّلَالِ الْبَعِيدِ

Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au ana wazimu? Bali wale wasio amini Akhera wamo adhabuni na upotofu wa mbali kabisa.

أَفَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ إِن نَّشَأْ نَخْسِفْ بِهِمُ الْأَرْضَ أَوْ نُسْقِطْ عَلَيْهِمْ كِسَفًا مِّنَ السَّمَاءِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّكُلِّ عَبْدٍ مُّنِيبٍ

Kwani hawaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao ya mbingu na ardhi? Tungeli penda tungeli wadidimiza ardhini, au tungeli wateremshia juu yao vipande vya mbingu. Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila mja aliye tubia. 

Wapinzani wa Bwana Mtume Muhammad SAW waliokuwa wakikanusha kuwepo uhai tena baada ya kufa walikuwa wakisema: madai haya ni uongo ambao mtu huyu anamnasibishia nao Mwenyezi Mungu; na yeye amepatwa na wendawazimu ndo maana anasema maneno kama haya; kama si hivyo vipi mtu mwenye akili anaweza kudai mambo kama haya?! Mwenyezi Mungu Mtukufu anawajibu watu kama hao kwa kuwaambia: Mtume si muongo wala si mwendawazimu! Bali ni nyinyi ndio mlio kwenye upotofu mkubwa mkawa hamko tayari kuyakubali maneno ya haki huku mkidhani kwamba kwa kukanusha Kiyama mtaweza kuokoka na adhabu anayoizungumzia yeye kuwa itakufikeni. Kisha Allah SW anawaeleza makafiri hao wakaidi na wenye inadi kwamba: Hivi nyinyi hamziangalii mbingu na ardhi mkaona zimeumbwa kwa nguvu na uwezo wa aina gani? Hivi kweli Mwenyezi Mungu aliye Muweza wa kuumba mbingu na ardhi zenye adhama kama hii atashindwa kukuumbeni nyinyi tena mara ya pili? Ni kweli hasa kwamba nyinyi mna shaka juu ya uwezo wake hata mnakadhibisha kama hivyo? Mnadhani Yeye hawezi kuleta tetemeko kubwa la ardhi likakudidimizeni nyote chini ya ardhi? Au akateremsha mawe kutoka mbinguni yakakuangamizeni nyinyi pamoja na nyumba zenu? Mtu yeyote mwenye akili timamu anajua kama hayo ni mambo yenye kuyumkinika na anazo taarifa za kutokea kwake katika pembe mbalimbali za dunia. Kama ni hivyo, vipi baadhi ya watu hawafikirii nyuma na mbele yao bali wanatosheka na wanayoyaona kwenye leo yao tu na kukikanusha Kiyama? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baadhi ya watu wanamkubali Mwenyezi Mungu kuwa ndiye Muumbaji na ndiye asili ya ulimwengu, lakini hawako tayari kuamini kufufuliwa kwa viumbe ili wasije wakalazimika kufuata maamrisho ya Mola na kubeba mas-ulia yanayotokana na maamrisho hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kutoamini akhera ni chimbuko la anuai za dhalala na upotofu na huwa sababu ya mtu kuzama zaidi kwenye lindi la upotofu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutafakari juu ya adhama ya uumbaji huifanya imani ya mtu juu ya asili ya ulimwengu iwe madhubuti na vilevile ni chemchemu ya imani juu ya ufufuo. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa mwanadamu ambaye hawezi kuyakabili matukio ya kimaumbile kama zilzala, vipi anaweza kuiepuka adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuiokoa nafsi yake na hilo? Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba kutafakari juu ya ulimwengu wa maumbile kunamfanya mtu awe na unyenyekevu wa kumtii na kumwabudu Mola wake Muumba; humuondolea utegemezi kwa watu na vitu vingine na huwa chemchemi ya kumwezesha kudhihirisha uja na kujielekeza kwa Mola wake. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 762 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/