Sura ya As-Sabaa, aya ya 10-13 (Darsa ya 763)
Sura ya As-Sabaa, aya ya 10-13 (Darsa ya 763)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 763 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 10 na 11 ambazo zinasema:
وَلَقَدْ آتَيْنَا دَاوُودَ مِنَّا فَضْلًا ۖ يَا جِبَالُ أَوِّبِي مَعَهُ وَالطَّيْرَ ۖ وَأَلَنَّا لَهُ الْحَدِيدَ
Na kwa hakika tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu, (tukasema): Enyi milima! Karirini kumtakasa Mwenyezi Mungu pamoja naye! Na ndege pia. Na tukamlainishia chuma.
أَنِ اعْمَلْ سَابِغَاتٍ وَقَدِّرْ فِي السَّرْدِ ۖوَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ
(Tukamwambia:) Tengeneza nguo za chuma pana, na kadiria sawa katika kuunganisha. Na tendeni mema. Hakika Mimi nayaona vyema mnayo yatenda.
Katika darsa iliyopita tulisoma katika sehemu ya mwisho ya aya ya tisa ya sura hii kuhusu «عبد مُنیب» yaani mja mwenye kutubia na kumuelekea Mola wake. Katika aya ya 24 ya Suratu-Sad pia imeashiriwa nukta hii, kwamba Nabii Daud (as) alitubia na kumuelekea Mola wake. Aya hizi tulizosoma zinaashiria sehemu moja ya maisha ya Nabii Daud na mwanawe, yaani Nabii Suleiman (as). Kwa kuanzia aya zinasema, Allah SW alimpa Nabii Daud atia na fadhila maalumu. Ni fadhila za kimaanawi na kimaada ambazo zimeashiriwa pia kwa ufupi katika aya za Suratu-Naml. Ya kwanza kati ya hizo ni ya vitu kama milima na viumbe kama ndege kuungana na kushirikiana na Mtume huyo wa Allah katika dua na munajati aliokuwa akifanya, kiasi kwamba kila pale Nabii Daud (as) alipokuwa akishughulika kumdhukuru Mwenyezi Mungu, vitu na viumbe vingine vilivyomzunguka vilikuwa navyo pia vikifanya hivyo, kiasi kwamba sauti za minong'ono ya dhikri zao ilizagaa kwenye anga yote. Imepokelewa katika Hadithi kuhusiana na Bwana Mtume Muhammad SAW pia, kwamba masahaba walikuwa wakisikia sauti za tasbihi za changarawe zilizokuwa mikononi mwa mtukufu huyo. Kisha aya zinaendelea kwa kuashiria moja ya uwezo maalumu aliokuwa nao Nabii Daud na kueleza kwamba: Sisi tulimlainishia chuma Daud ili atengezee nguo za chuma zitakazomkinga na maadui yeye na wafuasi wake. Inavyoonyesha, kabla ya Nabii Daud (as) wapiganaji vita walikuwa wakitumia mabamba ya vyuma kujikinga na mishale, mikuki na panga za maadui zao. Lakini mabamba hayo yalikuwa mazito, hivyo yakiwasababishia adha na udhia mkubwa. Lakini kwa irada ya Allah SW, Nabii Daud aliweza kukifanya chuma mithili ya nyuzi nyembamba kisha akazifinyanga katika umbo la mviringo na kuzisuka pamoja zikawa kama nguo, ambazo wapiganaji wake walizivaa zikaweza kuwakinga na mishale na panga za maadui. Aya hizi zimemalizia kwa kumhutubu Nabii Daud na kaumu yake ya kwamba: Zitumieni nyenzo hizo katika njia sahihi na inayofaa mkijua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wale wanaotubia na kurejea kikweli kweli kwa Allah SW, huneemeshwa kwa rehma na fadhila maalumu za Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa viumbe vyote vya ulimwengu wa maumbile, kuanzia vile visivyo na roho, mimea na wanyama vina hisi na vinatii amri ya Allah SW (kama tulivyoona aya hizi zilivyoihutubu milima na ndege). Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuyatumia na kufaidika nayo madini ya chini ya ardhi na maliasili za juu ya ardhi kwa ajili ya manufaa ya watu ni jambo lililousiwa na Allah SW. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kazi ya ufundi inapasa ifanyike kwa umakini na kuwa na kiwango cha ubora; na itumike kwa manufaa na maslahi ya wanadamu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 12 na 13 ambazo zinasema:
وَلِسُلَيْمَانَ الرِّيحَ غُدُوُّهَا شَهْرٌ وَرَوَاحُهَا شَهْرٌ ۖ وَأَسَلْنَا لَهُ عَيْنَ الْقِطْرِ ۖ وَمِنَ الْجِنِّ مَن يَعْمَلُ بَيْنَ يَدَيْهِ بِإِذْنِ رَبِّهِ ۖ وَمَن يَزِغْ مِنْهُمْ عَنْ أَمْرِنَا نُذِقْهُ مِنْ عَذَابِ السَّعِيرِ
Na kwa Suleiman tuliufanya upepo umtumikie. Safari yake ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja, na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja. Na tukamtiririshia chemchem ya shaba. Na katika majini walikuwako walio kuwa wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na kila anaye jitenga na amri yetu katika wao, tunamwonjesha adhabu ya Moto unao waka.
يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِن مَّحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَّاسِيَاتٍ ۚ اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ
Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu, na masanamu, na madeste makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyo ondolewa mahala pake. Enyi watu wa Daudi! Fanyeni amali kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanao shukuru.
Baada ya aya zilizotangulia kuashiria neema na fadhila alizojaaliwa Nabii Daud (as), aya hizi zinataja neema tatu miongoni mwa neema ambazo Allah alimjaalia Nabii Suleiman mwana wa Nabii Daud (as). Neema ya kwanza ni kipando cha angani (ambacho kilikuwa kinafanya kazi kama yalivyo maputo au mabaluni katika zama hizi). Baada ya kipando hicho kufika angani, kilikuwa kikisukumwa na upepo kuelekea kokote kule ambako Nabii Suleiman alitaka kielekee. Kwa kutumia kipando hicho, Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu aliweza kutumia muda wa kutwa moja kukata masafa ya kwenda na kurudi mahali ambako katika zama hizo ilichukua muda wa mwezi mmoja kufika. Neema ya pili ilikuwa ya kuyeyusha shaba kwa ajili ya kutengenezea anuai za vitu na nyenzo zilizohitajika, kama vyombo vidogo vidogo, vikubwa pamoja na majungu makubwa makubwa. Kama chuma kililainika mkononi mwa Nabii Daud, shaba nayo iliyeyuka ilipoingia kwenye mikono ya Nabii Suleiman. Na neema ya tatu aliyopewa Mtume huyo wa Allah ilikuwa ni ya kutiishiwa kundi la majini kwa ajili ya kumtumikia yeye na vyombo vya utawala wake; majini ambayo yalikuwa yakifanya kazi ngumu na nzito kwa amri ya Nabii Suleiman (as), na pale yalipokhalifu na kukaidi kufanya hivyo yalipewa adhabu kali. Kuhusiana na neema ya pili ni wazi kwamba mwanadamu amefikia uwezo wa kuyeyusha shaba, lakini kuhusu neema ya kwanza na ya tatu, hayo ni katika mambo ambayo hayafahamiki katika elimu ya mwanadamu, hivyo si hasha watu wa kimaada wakayachukulia kama mambo ya khurafa na uzushi. Lakini watu waumini, ambao wana itikadi juu ya nguvu na visababishi vya ghaibu na visivyo vya kimaada vya mambo, wao wanakubali kwamba mbali na visababishi vya kimaada vinavyojulikana, kuna visababishi pia vya kimaada na visivyo vya kimaada katika ulimwengu huu ambavyo havijatambuliwa bado na wanadamu ambavyo mawalii wa Mwenyezi Mungu wamevifikia kwa idhini yake Mola na kuweza kufaidika na kuneemeka navyo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata na aya hizi ni kwamba Mitume na mawalii wa Allah wamepewa uwezo wa kufanya mambo yaliyo nje ya uwezo wa kawaida wa mtu katika ulimwengu huu wa maumbile. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mwanadamu anaweza kumtiisha jini afanye atakalo, hata hivyo haijausiwa kufanya hivyo isipokuwa katika mambo ayatakayo Allah SW. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba uundaji vitu vya ufundi na sanaa na kuyatumia madini na vyuma ni miongoni mwa mafunzo ambayo Allah SW aliwapa baadhi ya Mitume ili kuwawepesishia wanadamu njia ya ustawi na maendeleo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa uyeyushaji shaba na kumimina kwenye kalibu ili kutengeza vitu, kuna historia ndefu inayorejea kwenye zama za Nabii Suleiman (as); ambapo katika zama za Mtume huyo, walikuwa wakitumia shaba iliyoyeyushwa na kutiwa kwenye kalibu za vitu kutengenezea vyombo vidogo vidogo na vikubwa vya shaba. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 763 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuutumia ujuzi na elimu anazotuelimisha kwenye mambo ya kheri na yenye manufaa kwetu, si madhara juu yetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/