Sura ya As-Sabaa, aya ya 22-24 (Darsa ya 766)
Sura ya As-Sabaa, aya ya 22-24 (Darsa ya 766)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 766 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 22 na 23 ambazo zinasema:
قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ ۖ لَا يَمْلِكُونَ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَمَا لَهُمْ فِيهِمَا مِن شِرْكٍ وَمَا لَهُ مِنْهُم مِّن ظَهِيرٍ
Sema: Waombeni hao mnaodai kuwa ni badala ya Mwenyezi Mungu. Hawamiliki hata chembe mbinguni wala ardhini. Wala hawana ushirika wowote humo. Wala hawana msaidizi miongoni mwao.
وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ ۚ حَتَّىٰ إِذَا فُزِّعَ عَن قُلُوبِهِمْ قَالُوا مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ ۖ قَالُوا الْحَقَّ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ
Wala hautafaa uombezi mbele Yake ila kwa yule aliyempa idhini. Hata itakapoondolewa fazaa kwenye nyoyo zao, watasema: Kasema nini Mola wenu? Watasema: Haki, Naye Ndiye aliye juu, Mkubwa.
Aya hizi zinawahutubu washirikina na waabudu masanamu wa Makka kwa kuwatupia masuali ya kimantiki ili kuzipa changamoto imani na itikadi zao zisizo na msingi wowote. Kwa kuanzia aya zinasema: Nyinyi mnaitakidi kuwa Mwenyezi Mungu ana washirika na kwamba baadhi ya masuala ya uendeshaji ulimwengu yako mikononi mwa washirika hao. Kama muyasemayo ni kweli waombeni wao basi wakutengezeeni mambo yenu na kukutatulieni matatizo yenu. Lazima wao wawe wanamiliki sehemu ya mbingu na ardhi, au wawe washirika wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji na uendeshaji wa ulimwengu; au angalau wawe manaibu na wasaidizi wake katika ufanyaji mambo hata waweze kuwa na nafasi katika masuala ya ulimwengu huu. Kwa kuzingatia kuwa moja ya imani za Waislamu ni kuhusu shufaa na uombezi wa Mitume na mawalii wa Allah, katika kujibu suali kwamba kuna tofauti gani kati ya masanamu na waja wanaoshufaia, aya inayofuatia inasema: Mitume na mawalii mahususi wa Allah nao pia ni viumbe na mahuluku wake Mola; na kama walivyo viumbe wengine, wao wenyewe hawana nguvu wala uwezo wowote. Lakini Mwenyezi Mungu mwenyewe amewapa idhini ya kuwashufaia na kuwaombea baadhi ya watu. Sisi sote tunajua kama Allah SW amewafanya Mitume kuwa wasita na kiunganishi na kuwatuma ili wawaelekeze watu kwenye uongofu na akawafikishia maamrisho yake kwa njia ya wahyi, na wao Mitume wakayafikisha mafundisho hayo kwa watu. Katika suala la shufaa pia wale waumini ambao wamefanya taksiri katika kutekeleza majukumu yao ya kidini wanawaendea Mitume na kuwataka wawe wasita baina yao na Allah ili Yeye Mola awatakabalie toba zao. Kwa hivyo kama ambavyo toba ni njia ya kurejea kwa Mwenyezi Mungu, wao waumini wanawaendea mawalii wake ili kupata ridhaa yao, ambayo huwafungulia njia ya kupata ridhaa yake Yeye Mola. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutasawiri na kufikiria kuwepo mmiliki na muumba ghairi ya Mwenyezi Mungu, ambaye ataweza kuwa maabudu wa mwanadamu ni fikra hewa na ya udhanifu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ujinga na kutokuwa na uwezo mwanadamu wa baadhi ya mambo ndiko kunakomfanya atafute mshirika katika kazi zake au msaada kwa wenzake. Lakini Allah SW, Mola wa ulimwengu ni Muweza wa kila kitu, hivyo hahitaji mshirika wala msaidizi. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kushufaia na kuombea hakumaanishi kwamba wanaoshufaia ni wenye huruma zaidi kuliko Mwenyezi Mungu; kwa sababu ni Yeye Allah ndiye anayewapa idhini mawalii wake mahususi wawashufaie watu. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba iko siku, hatimaye watu makafiri na waovu watakuja kukiri ukweli wa maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na njia ya Mitume wake, lakini kukiri huko hakutokuwa na faida yoyote kwao wao wakati huo.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 24 ambayo inasema:
قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ قُلِ اللَّـهُ ۖوَإِنَّا أَوْ إِيَّاكُمْ لَعَلَىٰ هُدًى أَوْ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ
Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Sema: Mwenyezi Mungu! Na hakika sisi au nyinyi bila ya shaka tuko kwenye uwongofu au upotofu ulio wazi.
Baada ya maudhui ya uumbaji iliyoashiriwa katika aya zilizotangulia, aya hii inazungumzia maudhui ya utoaji riziki na kueleza kwa njia ya kuhoji: Ni nani aliyekuwekeeni njia na sababu za kupatia riziki? Ni nani anayeleta mawingu na upepo ili mvua inyeshe na kuifanya ardhi kavu na yabisi iwe na utayari kwa ajili ya kilimo na upandaji mazao? Ni nani anayeifanya mbegu ichipue kutoka kwenye udongo na kutoa anuai za mazao kwa ajili yenu? Ni nani anayeliamrisha jua litoe mwangaza na joto mnalohitajia nyinyi pamoja na mimea na wanyama wenu? Ni kwa amri ya nani mbingu na ardhi zimeweza kumtayarishia mwanadamu nyenzo, sababu na suhula kama hizi za maisha? Katika mambo yote haya, nyinyi washirikiana mnamfanyia Mwenyezi Mungu mshirika, wakati sisi tunaamini kuwa neema zote hizi zinatoka kwa Mwenyezi Mungu mmoja asiye na mshirika. Hakuna shaka kuwa itikadi mbili hizi zina mgongano. Kwa hivyo nyinyi kaeni mfikiri, muone kama maneno yetu ni sahihi muyakubali; na kama mtayayona si sahihi basi yakataeni. Ukweli ni kwamba Bwana Mtume SAW hajikatii hukumu yeye mwenyewe kwa kusema sisi tuko kwenye haki na nyinyi mko kwenye batili, bali anatumia njia ya insafu na kusema: moja kati yetu sisi makundi mawili liko kwenye uongofu na kundi jengine liko kwenye dhalala na upotofu. Kwa hivyo kila mmoja kati yetu achunguze kwa kutumia akili na mantiki na kuona imani na itikadi yake inaafikiana na hali ipi: uongofu au upotofu? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika mfumo wa elimu na malezi, tupendelee zaidi kutumia mbinu ya uulizaji masuali badala ya maelezo ya moja kwa moja ili kuweza kuamsha dhamiri za walengwa na kuwafanya wao wenyewe wakae na kutafakari juu ya maudhui wanazoulizwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa ijapokuwa mwanadamu hulima na kuvuna anuai za mazao kwa juhudi na bidii anazofanya lakini sababu za upatikanaji mazao hayo zinatokana na Mwenyezi Mungu. Maji, udongo na hewa ni miongoni mwa vitu vyenye nafasi na mchango muhimu katika kilimo na ufugaji na ni miongoni mwa neema za Allah kwa mwanadamu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba riziki ya mbinguni ni mwangaza, joto, mawingu, upepo na mvua; na riziki ya ardhini ni matunda yote na baraka za ardhini. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hii kuwa tuwe na insafu katika kuzungumza na kujadiliana na wapinzani; na si kuwaambia tu: sisi tuko kwenye haki na nyinyi mko kwenye batili. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 766 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washukurivu wa neema zake kubwa na ndogo, tunazozijua na tusizozijua. Aidha atujaalie kuwa walinganiaji wema wa Uislamu kwa kauli na amali zetu, si wenye kuliharibu jina la dini hii tukufu kwa ndimi na matendo yetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/