Sura ya As-Sabaa, aya ya 25-30 (Darsa ya 767)
Sura ya As-Sabaa, aya ya 25-30 (Darsa ya 767)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 767 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 25, 26 na 27 ambazo zinasema:
قُل لَّا تُسْأَلُونَ عَمَّا أَجْرَمْنَا وَلَا نُسْأَلُ عَمَّا تَعْمَلُونَ
Sema: Nyinyi hamtaulizwa kwa makosa tuliyo yafanya, wala sisi hatutaulizwa kwa mnayo yatenda nyinyi.
قُلْ يَجْمَعُ بَيْنَنَا رَبُّنَا ثُمَّ يَفْتَحُ بَيْنَنَا بِالْحَقِّ وَهُوَ الْفَتَّاحُ الْعَلِيمُ
Sema: Mola wetu Mlezi atatukusanya, kisha atatuhukumu kwa haki; Naye ndiye Hakimu, Mjuzi.
قُلْ أَرُونِيَ الَّذِينَ أَلْحَقْتُم بِهِ شُرَكَاءَ ۖ كَلَّا ۚ بَلْ هُوَ اللَّـهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
Sema: Nionyesheni mlio waunganisha Naye kuwa washirika. Hasha! Bali Yeye ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa katika kuwalingania watu wito wa haki, Bwana Mtume Muhammad SAW amewataka wao wenyewe wakae watafakari na kuchagua njia wanayohisi kuwa ndiyo ya haki; na bila shaka kila mtu atawajibika kwa njia aliyojichagulia, na kwa amali na matendo aliyofanya. Baada ya maelezo hayo, aya tulizosoma zinasema: Siku ya Kiyama kila mtu atasailiwa na kuulizwa kulingana na chaguo alilofanya. Bila shaka hakimu na mwamuzi baina ya watu atakuwa ni Allah SW ambaye ni Muumba wa mbingu na ardhi na Mjuzi wa hali zote za waja wake. Yeye Mola atahukumu kwa haki na uadilifu na atamlipa kila mtu jaza na malipo ya amali zake. Hapa duniani, kila mtu huwa anadai kwamba fikra, matendo na njia anayofuata yeye ndio sahihi; hivyo huwa si rahisi wakati mwengine mtu kuweza kupambanua kati ya haki na batili. Lakini akhera hakutokuwa pahala pa mtu kujidai, kwani ni Yeye Allah SW, kulingana na elimu yake mutlaki ya ujuzi wa kila kitu, ndiye atakayeainisha ipi haki na ipi batili na kutenganisha baina ya mawili hayo. Kisha aya inayofuatia inawahutubu tena washirikina ya kwamba: hivyo mnavyovidhani kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu havina ukweli wowote; hizo ni dhana na mawazo yenu tu. Hicho si kitu kinachoweza kuonyeshwa na kuthibitishwa ukweli wake. Ni vipande vya miti na mawe tu visivyo na thamani yoyote ya kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji au wasaidizi katika uendeshaji masuala ya ulimwengu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama kipimo cha mambo yote ni haki na batili; si nasaba na uhusiano wa kifamilia, lugha au asili za watu. Kwa hivyo amali za kila mtu zitapimwa kwa kutumia mizani ya haki tu, si kitu kingine chochote kile. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika kuzungumza na wapinzani tusiwachukulie kuwa ni waovu na wafanya madhambi. Bwana Mtume SAW aliwaambia washirikina: Mwenyezi Mungu atatusaili sisi kwa sababu ya madhambi yetu na nyinyi pia kutokana na amali zenu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba hakuna yeyote kati ya maabudu na miungu waliobuniwa na wanadamu yakiwemo masanamu na malaika, wanaojiitakidi wao wenyewe kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu; ni watu wajinga na majahili ndio wanaowaunganisha wao na Allah na kuwaitakidi kuwa ni washirika wake Mola.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 28 ambayo inasema:
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ
Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui.
Baada ya maudhui ya tauhidi na shirki, aya hii ya 28 inazungumzia sifa ya wito na risala ya Utume wa Nabii Muhammad al-Mustafa SAW ya kuwa kwake kwa ajili ya ulimwengu mzima. Ijapokuwa wahutubiwa wake wa mwanzo walikuwa wazungumzaji wa lugha ya Kiarabu wa eneo la Hijaz; na Kitabu alichopewa yeye kiliteremshwa kwa lugha ya Kiarabu, lakini ujumbe uliomo ndani yake hauihusu kaumu na wazungumzaji wa lugha maalumu na kwa ajili ya zama za mtukufu huyo tu. Ni ujumbe unaojumuisha watu wa ulimwengu mzima wa kila asili, kabila na rangi hadi mwisho wa dunia. Kama ambavyo aya ya mwanzo ya Suratul Furqan pia inautaja wito wa Utume wa nabii huyo wa rehma kuwa ni kwa ajili ya walimwengu wote. Katika aya hii imeashiriwa pia mbinu na utaratibu wa uelimishaji wa mtukufu huyo katika kutekeleza jukumu lake la Utume na kueleza kwamba: yeye anawapa bishara njema ya saada ya dunaini na akhera wanaoikubali haki na kuifuata; na kwa wale wanaofanya ukaidi na inadi na kuipa mgongo haki anawapa indhari na maonyo ya kufikwa na adhabu kali. Kwa masikitiko makubwa ni kwamba, watu wengi wameghafilika na nafasi ya imani na kukufuru katika saada na kufuzu kwao na wala hawazingatii bishara na indhari wanazopewa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Utume wa Nabii Muhammad SAW ni wa ulimwengu mzima; na kutoa kisingizio kwamba yeye hakutokana na kaumu na watu wa asili yetu ni sawa na mtu aseme: watu wa Sham na Palestina peke yao ndio wanaopaswa kuwa Wakristo, kwa sababu Nabii Isa (as) alizaliwa katika ardhi hiyo na alifikisha ujumbe wa Utume wake katika eneo hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mitume walipewa kazi ya tablighi na kufikisha wito wa Mwenyezi Mungu, si kuwalazimisha watu waiamini na kuifuata dini ya haki; kwa hivyo mbinu ya ulinganiaji wao imesimama juu ya msingi wa utoaji bishara na indhari si kuwalazimisha watu na kuwateza nguvu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 29 na 30 ambazo zinasema:
وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ
Na wanasema: Ahadi hii itakuwa lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
قُل لَّكُم مِّيعَادُ يَوْمٍ لَّا تَسْتَأْخِرُونَ عَنْهُ سَاعَةً وَلَا تَسْتَقْدِمُونَ
Sema: Nyinyi mna miadi ya Siku ambayo hamtaakhirika nayo kwa saa moja, wala hamtaitangulia.
Baada ya aya zilizotangulia kugusia maudhui za Tauhidi na Utume, aya hizi zinaashiria maudhui ya Maadi yaani kufufuliwa viumbe na kueleza kwamba: wakanushaji wa Maadi hawana hoja ya kupinga uwezekano wa kujiri tukio hilo, bali kisingizio kikubwa wanachotoa ni kutojulikana wakati hasa wa kutokea kwake na hivyo wanaamua kukana na kukadhibisha. Ni kama ambavyo watu wote wana yakini kuwa watakufa, lakini hakuna yeyote ajuaye atafikwa na mauti wakati gani. Katika aya hizi tulizosoma Qur'ani tukufu inasema: kujiri kwa Kiyama ni jambo la hakika kabisa ambalo litathibiti katika wakati uleule kama alivyolipanga na kulikadiria Allah SW pasi na kuharakishwa wala kucheleweshwa hata kwa sekunde moja. Na wakati mtakapoziona ishara zake hamtoweza kukikwepa au kuchelewesha kujiri kwake. Kwa hivyo badala ya kufikiria namna ya kukadhibisha, kaeni mtafakari mkijua kwamba siku hiyo mtapaswa kuja kuwajibika kwa amali zenu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ni Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake ndiye aujuaye wakati hasa wa kutokea Kiyama. Hata Mitume pia hawana ilimu juu ya jambo hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa badala ya kutoa visingizio kuhusu wakati wa kujiri tukio la Kiyama au jinsi mtu atakavyolipwa malipo ya thawabu au adhabu, tufikirie namna ya kurekebisha fikra na mienendo yetu ili wakati huo tusije tukafika kwenye uwanja wa Kiyama tukiwa mikono mitupu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 767 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atakabalie toba zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/