Sura ya As-Sabaa, aya ya 31-33 (Darsa ya 768)
Sura ya As-Sabaa, aya ya 31-33 (Darsa ya 768)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aal zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 768 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 31 ambayo inasema:
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَن نُّؤْمِنَ بِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَلَا بِالَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ ۗ وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ مَوْقُوفُونَ عِندَ رَبِّهِمْ يَرْجِعُ بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ الْقَوْلَ يَقُولُ الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا لَوْلَا أَنتُمْ لَكُنَّا مُؤْمِنِينَ
Na walisema walio kufuru: Hatutaiamini Qur'ani hii, wala yaliyo kuwa kabla yake. Na ungeli waona madhaalimu watapo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, wakirudishiana maneno wao kwa wao! Wanyonge wakiwaambia walio takabari: Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa Waumini sisi.
Aya hii ya 31 inaendelea kuzungumzia yale yaliyoashiriwa katika darsa zilizopita kuhusu nafasi na hali za waumini na makafiri zitakavyokuwa Siku ya Kiyama na kueleza kwamba: makafiri wanayakufuru na kuyakanusha yale yaliyotajwa ndani ya Vitabu vya mbinguni kuhusu Tauhidi na Maadi na hawako tayari kuyakubali. Kwa hakika watu hao wameshajikatia kwamba wasiikubali haki, sawa kabisa na mtu anayejifanya amelala, ambaye vyovyote utakavyomuita na kumtikisa hatoamka na kuinuka. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba: pamoja na hayo wakanushaji hawa hawa ambao hapa duniani wanaipa mgongo haki kwa sababu ya inadi, taasubi na ukaidi usio na msingi, Siku ya Kiyama watatafuta visingizio vya kutetea ukanushaji wao kwa kujaribu kuwabebesha watu wengine mzigo wa madhambi yao. Kwa hivyo watawaambia wakubwa wa jamii zao, ambao nao wenyewe pia watakuwa watu wa Motoni ya kwamba: nyinyi ndio mliotupotosha, vinginevyo sisi tungeamini haki na leo tusingefikwa na adhabu.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba inadi, ukaidi na taasubi dhidi ya haki humsukuma mtu kwenye ukafiri na ukanushaji. Mtu anayefikia hali hiyo hawi tayari katu kuiamini haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa vitabu vyote vya mbinguni vina lengo moja na muelekeo mmoja. Kwa hivyo makafiri hawakiamini chochote kile kati ya vitabu hivyo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kufru, shirki na kutoifuata dini ni dhulma kubwa ambayo mtu anaifanyia nafsi yake pamoja na Mitume wa Allah. Wa aidha aya hii inatufunza kuwa katika utamaduni na mafundisho ya dini kuidhulumu mtu nafsi yake nako pia ni katika vielelezo vya dhulma. Vile vile aya hii inatutaka tuelewe kwamba imani ndicho kitu kitakachomnusuru na kumfanya mtu afuzu Siku ya Kiyama.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 32 na 33 ambazo zinasema:
قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا أَنَحْنُ صَدَدْنَاكُمْ عَنِ الْهُدَىٰ بَعْدَ إِذْ جَاءَكُم ۖ بَلْ كُنتُم مُّجْرِمِينَ
Walio takabari watawaambia wanyonge: Kwani sisi ndio tulio kuzuieni na uwongofu baada ya kukujieni? Bali nyinyi wenyewe mlikuwa waovu.
وَقَالَ الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا بَلْ مَكْرُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ إِذْ تَأْمُرُونَنَا أَن نَّكْفُرَ بِاللَّـهِ وَنَجْعَلَ لَهُ أَندَادًا ۚ وَأَسَرُّوا النَّدَامَةَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ وَجَعَلْنَا الْأَغْلَالَ فِي أَعْنَاقِ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
Na wanyonge watawaambia walio takabari: Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi Mungu, na tumfanyie washirika. Nao wataficha majuto watakapo iona adhabu. Na tutaweka makongwa shingoni mwa walio kufuru. Kwani wanalipwa ila kwa waliyo kuwa wakiyatenda?
Katika aya hizi yametumiwa mara kadhaa maneno "mustadh-af" na "mustakbir". Inavyoonyesha, madhumuni ya mustadh-afun, yaani wanyonge ni watu wanaoridhia kuwafuata wenzao kibubusa bila ya kutumia akili na fikra zao; na mustakbirun yaani waliotakabari ni watu wanaoyatumia vibaya madaraka na utajiri wao ili kuwanyongesha wenzao na kujikweza juu yao. Ni wazi kwamba mustakbirina hawawalazimishi watu wawatii na kuwafuata. Wao hutumia mbinu mbalimbali za kipropaganda na nyenzo tofauti za kiutamaduni ili kueneza na kutangaza fikra zao za kishirki, ambapo baadhi ya watu huamua kuyaweka pembeni mafundisho ya Mitume na Vitabu vya mbinguni na kufuata propaganda za marembo na mapambo za watu hao. Na kwa bahati ni kwamba yale yanayoenezwa na kutangazwa na mustakbirina katika propaganda zao yanaendana na kuvutia zaidi matashi, hawaa na matamanio ya nafsi ya watu wengi, kwa sababu kama watawafuata mustakbirina hawawi na haja ya kudhibiti masikio, macho na ndimi zao. Yale yanayonakiliwa na aya tulizosoma kuhusu mazungumzo yatakayojiri baina ya makundi hayo mawili Siku ya Kiyama ni ishara kwamba hila na hadaa zinazofanywa na wenye nguvu za madaraka na utajiri wa mali hazimpi uhalali mtu wa kukwepa mas-ulia na kujivua na dhima ya kufuata upotofu wa watu hao. Kila mtu, hata mwenye elimu na utambuzi finyu wa mambo, badala ya kufuata hawaa na matamanio ya nafsi yake anapaswa afuate akili, fitra na maumbile yake safi ambayo ametunukiwa na Allah. Bila shaka mustakbirina wataadhibiwa kulingana na kiwango cha upotoshaji waliofanya kuwapotosha watu; lakini mustadh-afina pia, hawawezi kutetea kuhadaiwa na kughilibiwa kwao kuwa ni kisingizio cha wao kufanya madhambi na kujivua na dhima ya madhambi hayo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, japokuwa jamii chafu na iliyofisidika ina taathira hasi na zenye madhara kwa watu lakini haiwalazimishi kupotoka na kufanya maovu na ufasiki. Kwa hivyo mtu hawezi kuibebesha jamii yake mzigo wa madhambi na makosa anayofanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Siku ya Kiyama haitowezekana mtu kumbebesha dhambi zake mtu mwengine. Kwa maneno mengine, hakuna mtu atakayebeba mzigo wa dhambi za mwenzake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mtu yeyote atakayefikiwa na wito wa Mitume na Vitabu vya mbinguni lakini akaukataa atalazimika kwenda kujieleza na kuwajibika Siku ya Kiyama. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mustakbirina wenye nguvu za madaraka na utajiri wa mali wanapanga usiku na mchana namna ya kueneza fikra zao kwa watu, kuwahodhi na kuwadhibiti na kutowapa fursa ya kufikiri. Kwa kutumia mbinu hiyo, wanawazuilia watu njia ya Mwenyezi Mungu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba watu waliopotoka wanawashawishi na kuwaita watu wengine pia kwenye upotofu; na badala ya kuwakataza mabaya wanawahamasisha kufanya maasi na maovu; na kwa njia hiyo kuielekeza jamii kule walikoelekea wao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 768 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na kufuata mambo kibubusa kwa sababu ya kuyarithi kwa wazee wetu au kwa kuzoeleka katika jamii zetu, mambo ambayo yatazikhasirisha nafsi zetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/