Dec 25, 2017 10:33 UTC

Sura ya As-Sabaa, aya ya 34-37 (Darsa ya 769)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 769 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 34 na 35 ambazo zinasema:

 وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ

Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji, ila walisema wapenda anasa wake: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyo tumwa nayo.

 وَقَالُوا نَحْنُ أَكْثَرُ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ

Na wakasema: Sisi tuna mali mengi zaidi na watoto, wala sisi hatutaadhibiwa.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia majibizano yatakayojiri Siku ya Kiyama kati ya wanyonge na waliotakabari. Aya tulizosoma zinasema: Waliotakabari, ambao ni watu walioleweshwa na neema walizojaaliwa na Allah wakiwa wameghariki kwenye starehe, raha na anasa wanadhani kwamba wao ni wabora na wako juu zaidi kupita watu wengine; na alama ya ubora wao ni wingi wa mali na umaarufu wa koo na nasaba zao. Watu hao walikuwa hawayajali maneno ya Mitume kwa sababu kwa kawaida watu wanyonge na wahitaji ndio waliokuwa wakiwaamini Mitume na kuwa karibu nao wakati matajiri walikuwa wakijihisi si hadhi yao na hailaiki kwa wao kuchanganyika na kukaa mahali pamoja na watu wanyonge na masikini katika jamii. Wao walikuwa wakitamka dhahiri shahiri kwamba sisi hatuko tayari kuwaamini Mitume na vitabu walivyokuja navyo. Na kama tutajaalia kwamba Kiyama pia kitakuja, Mwenyezi Mungu hatotuadhibu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anatupenda sisi na ndiyo maana ametupa mali na watoto wengi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baadhi ya wakati mali na madaraka huyapofua macho na moyo wa mtu mpaka akayapinga mafundisho ya Mitume bila hoja wala mantiki yoyote, na kuyakataa katakata maneno ya haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kujaaliwa neema za dunia si ishara ya mtu kuwa karibu na Mwenyezi Mungu. Ukweli ni kwamba kujaaliwa neema kunambebesha mtu dhima na mas-ulia. Aya hizi aidha zinatuelimisha kuwa ikiwa raha na starehe zitamtia mtu ghururi zinaweza kumfanya awe na inadi na ukaidi wa kuikubali haki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuwa na raha duniani hakuashirii kuwa na raha na neema pia huko akhera. Kwani kuna watu wengi wenye raha ambao wameishi maisha ya raha na starehe duniani lakini akhera watakuwa katika adhabu kali.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 36 ambayo inasema:

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

Sema: Hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki amtakaye na huikunja, lakini watu wengi hawajui.

Baada ya aya zilizotangulia zilizoeleza kwamba: wanaotakabari wanachukulia kwamba kuwa na raha duniani ni ishara ya kupendwa na Mwenyezi Mungu na pia ni kiashiria cha kuwa na raha na starehe huko akhera, aya hii ya 36 inasema: ukunjufu wa riziki au kudhikishiwa si ishara ya kupendwa wala kughadhibikiwa na Allah hata idhaniwe kwamba kila mwenye mali na utajiri ni mtu anayependwa na Mola; na kila masikini na mwenye dhiki ya maisha ni mtu aliyeghadhibikiwa. Kutafautiana huko katika upataji wa riziki kunatokana na hekima na maslaha maalumu, kwa sababu Allah SW ameuumba mfumo wa ulimwengu kwa misingi hiyo ya maslaha na hekima wala hauna uhusiano na mapenzi au ghadhabu zake kwa waja wake. Hata hivyo watu wengi hawalizingatii hilo na hivyo wanahukumu mambo visivyo kwa kutegemea dhana na mawazo yao tu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kupewa na kuondolewa neema kunafanyika kwa maslaha na hekima ya Mwenyezi Mungu; si alama ya kupendwa au kughadhibikiwa na Yeye Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa moja ya majukumu ya Mitume ni kurekebisha fikra na mawazo yasiyo sahihi waliyonayo watu ili wasije wakamnasibishia Mwenyezi Mungu mambo batili na ya upotofu. Kwa mfano wasidhani kwamba kila mara mtu anapojaaliwa kuwa na neema nyingi na raha chungu nzima, hiyo ni ishara ya kupendwa na kuridhiwa na Allah. Aidha aya hii inatutaka tujue kwamba mali na watoto tulionao vinatokana na Mwenyezi Mungu, si sisi wenyewe. Kazi na juhudi tunazofanya pamoja na viunganishi vingine vinavyotuwepesishia kupata riziki visitufanye tukaghafilika na Ar-Razzaq, yaani mtoaji halisi wa kila riziki tuipatayo.

Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 37 ambayo inasema:

وَمَا أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُم بِالَّتِي تُقَرِّبُكُمْ عِندَنَا زُلْفَىٰ إِلَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ جَزَاءُ الضِّعْفِ بِمَا عَمِلُوا وَهُمْ فِي الْغُرُفَاتِ آمِنُونَ

 Na si mali yenu wala watoto wenu watakao kukaribisheni kwetu muwe karibu, isipo kuwa aliye amini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo maradufu kwa waliyo yafanya. Nao watakuwa salama katika maghorofa.

Kwa mujibu wa aya ya 15 ya Suratu-Taghaabun neema zote za Allah zikiwemo mali na watoto ni nyenzo za kutahiniwa na kujaribiwa watu. Na ndiyo maana kuna watu wengi waliojaaliwa utajiri wa mali na satua za madaraka ambao wanazitumia vizuri sana neema hizo za Allah katika njia za kheri kwa kufanya mambo mema na kuwahudumia wanyonge na wahitaji. Watu wa aina hii watapata ujira na thawabu kubwa kwa Mola. Na kinyume chake pia kuna matajiri wengi ambao wanazifanyia uchoyo na ubakhili mali na utajiri waliojaaliwa na hivyo kuwaletea balaa wao wenyewe hapa duniani na kuwa sababu ya kupata adhabu kali huko akhera. Mkabala na hao walioneemeshwa kwa mali na utajiri, kuna watu wanyonge na masikini wengi ambao wanastahamili na kuvumilia hali yao ya umasikini na kutofanya uhalifu na uovu ili tu wawe matajiri kwa gharama yoyote ile. Hao watalipwa na Allah malipo makubwa ya thawabu kwa subira na uvumilivu wao huko akhera. Na tab'an kuna masikini wengi pia wanaotumia kisingizio cha umasikini na matatizo waliyonayo kujihalalishia kufanya vitendo viovu na kuwa tayari kufanya uovu wowote ule alimuradi wapate mali na utajiri. Kisha aya inaendelea kwa kueleza kwamba, kipimo cha kupata mapenzi ya Allah ni imani na amali njema na kufafanua kuwa: badala ya kushughulishwa na nyumba, gari na hali ya maisha ya watu zingatieni amali na matendo yao. Ikiwa amali zao ni njema na wanafanya wayafanyayo kwa ajili ya Allah basi ni watu waliofuzu; wawe matajiri au mafakiri! Lakini kama watakuwa makafiri au wenye kufanya maovu na maasi, hawatofuzu hapa duniani wala huko akhera, iwe wao ni masikini au ni matajiri! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba watu wengi wanazichukulia mali na watoto kuwa ni alama ya saada na kufuzu, ilhali mbele ya Mwenyezi Mungu, imani na amali njema ndio sababu ya kufuzu na kuokoka mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuwa na mali na watoto na suhula zozote zile sio msingi; la msingi na muhimu ni jinsi mtu atakavyozitumia neema hizo. Ikiwa mtu atazitumia neema hizo katika njia sahihi kwa msingi wa imani sahihi na amali njema zitakuwa sababu ya kumjenga na kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiutu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa adhabu za Mwenyezi Mungu zinalingana na dhambi na kosa la mtu, lakini jaza na thawabu zake zinatokana na uraufu na fadhila zake Mola na ni nyingi zaidi maradufu kulinganisha na amali njema aliyofanya mja. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 769 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washukurivu wa kila neema aliyotujaalia, kwa kuitumia kwa namna na katika njia inayomridhisha Yeye Mola. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/