Sura ya As-Sabaa, aya ya 38-41 (Darsa ya 770)
Sura ya As-Sabaa, aya ya 38-41 (Darsa ya 770)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 770 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 38 ambayo inasema:
وَالَّذِينَ يَسْعَوْنَ فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ فِي الْعَذَابِ مُحْضَرُونَ
Na wale ambao wana jitahidi kuzipinga Ishara zetu, wakaona watashinda, hao watahudhurishwa kwenye adhabu.
Aya ya mwisho tuliyosoma katika darsa iliyopita ilibainisha nukta moja, nayo ni kwamba, kwa dhati yake, mali na watoto si vitu vinavyomfanya mtu afuzu na kupata saada. Ni imani na amali njema, ndivyo vinavyomfanya afaulu na kupata saada ya duniani na akhera na kuwa miongoni mwa watakaoingizwa kwenye Pepo ya Allah SW. Baada ya hayo, aya tuliyosoma inaashiria kundi linalokabiliana na wale walioamini na kueleza kwamba: watu hao badala ya kujitahidi kuitambua haki na kuifuata, wao daima huwa wanaikana na kuipiga vita wakidhani kwamba kwa sababu ya kuwa na nguvu za madaraka, utajiri wa mali na kila suhula wataweza kutoka nje ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu Jalla Jalaaluh na kuikwepa adhabu yake. Watu hao inawapasa wajue kwamba dhana yao hiyo ni batili, na wao bila shaka yoyote watahudhurishwa Siku ya Kiyama na kufikwa na adhabu kwa matendo yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wenye nguvu za utajiri na madaraka, ambao wanazitumia suhula zao kuipiga vita na kuiangusha haki ili kuifuta na kutaka ionekane kuwa kitu dhaifu, wao wenyewe ndio watakaoanguka na wala hawatoweza kuishinda irada ya Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa maadui wa Uislamu wanatumia kila hila kuidhoofisha hadhi ya Qur'ani mbele ya macho ya watu. Kwa hivyo Waislamu wote hususan maulamaa wa dini wana wajibu wa kupanga mkakati kamili wa kuzuia maadui wasiweze kufikia lengo lao.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 39 ambayo inasema:
قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ
Sema: Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakacho kitoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanao ruzuku.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia ambayo iliwalaumu na kuwakemea watu wanaojivuna na kujifaharisha kwa wenzao kwa mali na watoto waliojaaliwa na hivyo kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa riziki kwa waja wake na kumzidishia huyu na kumpunguzia yule kulingana na maslaha na hekima yake. Kwa hivyo kukunjuliwa riziki kusikutieni ghururi na kiburi wala kudhikishiwa kusikuvunjeni moyo na kukukatisheni tamaa. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba: mtu anapaswa ajitahidi kutoa alichoruzukiwa kuwasaidia wahitaji kulingana na uwezo wake kwa sababu riziki za waja ziko mikononi mwa Allah, na Yeye Mola amemwahidi kila mwenye kutoa kuwapa wahitaji, kwamba atamfidia kwa alichotoa pasi na kupungukiwa katika riziki yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kutofautiana watu katika riziki kunatokana na hekima yake Mola kama wanavyotofautiana katika vipawa, akili na uwezo wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mola anayewapa riziki watu na viumbe wengine, ametoa hakikisho la kumfidia kwa namna mwafaka mja kile alichotoa kwa ajili yake kuwapa wenzake walio wahitaji.
Darsa ya 770 ya Qur'ani inahitimishwa na aya ya 40 na 41 ambazo zinasema:
وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ
Na siku atakayo wakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je! Hawa walikuwa wakikuabuduni?
قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ
Waseme: Subhanak, Umetakasika. Wewe ndiye walii wetu si hao. Bali wao walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao.
Moja ya itikadi za kikhurafa walizokuwa nazo washirikina ilikuwa ni kuamini kwamba watapata shufaa na uombezi wa malaika Siku ya Kiyama. Kwa hivyo kwa namna fulani, wakawa wanawaabudu malaika na kuwapa hadhi na utukufu maalumu. Ilhali malaika, wao wenyewe hawakuwa wakijiitakidi wala kujidai kuwa na hadhi hiyo. Qur'ani tukufu inatoa taswira ya mahakama ya Siku ya Kiyama kwa kueleza kwamba: malaika siku hiyo watajitetea dhidi ya dhana batili walizokuwa nazo washirikina juu yao kwa kusema: wao walikuwa wametingwa na fikra za kishetani wakawa wanawafuata wao, na kwa hakika walikuwa watiifu kwa mashetani. Shetani aliwapambia ibada ya kuabudu masanamu na akaifanya ionekane nzuri na ya kupendeza mbele yao na akawashughulisha kufuata imani batili na matendo potofu. Ikawa kama kwamba badala ya kumwamini Mungu mmoja wa haki, wakawa watumwa wa shetani na wenye kumwamini yeye. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba washirikina walikuwa wakiwapa malaika hadhi na cheo maalumu. Walikuwa wakiitakidi kwamba malaika watawashufaia na kuwaombea wao Siku ya Kiyama. Kwa sababu hiyo wakawa wanaawabudu kwa namna mbalimbali ili waweze kupata uombezi huo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tujihadhari tusije tukahadaiwa na vitimbi na hila za shetani wala kughilibiwa na dhana zake potofu badala ya kufuata itikadi sahihi za uongofu. Kwani si hasha akayafanya machafu na maovu yaonekane mazuri na ya kupendeza mbele ya macho yetu. Wapenzi waskilizaji kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atulinde na kila vishawishi, ghilba na wasiwasi wa mashetani, miongoni mwa majini na watu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/