Dec 25, 2017 10:49 UTC

Sura ya As-Sabaa, aya ya 42-45 (Darsa ya 771)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 771 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 42 ambayo inasema:

فَالْيَوْمَ لَا يَمْلِكُ بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ نَّفْعًا وَلَا ضَرًّا وَنَقُولُ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذُوقُوا عَذَابَ النَّارِ الَّتِي كُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ

Hii leo hataweza yeyote kumletea nafuu wala madhara mwenzie. Na tutawaambia walio dhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mlio kuwa mkiukanusha.

Tuliona katika darsa iliyopita jinsi Allah SW alivyowahutubu washirikina kwamba: nyinyi mnadai kuwa mnawaabudu malaika na kutaka wakuombeeni na kukushufaieni, ilhali malaika wenyewe watalikana jambo hili Siku ya Kiyama na kuwaambia kwamba nyinyi mlikuwa mkimfuata shetani na kutaka msaada kwa mashetani. Baada ya hayo, aya tuliyosoma inasema: Siku ya Kiyama ghairi ya Allah SW na watu atakaotaka Yeye, hakuna mtu mwengine yeyote atakayeweza kuwanufaisha au kuwasababishia madhara wanadamu wenzake; yaani mathalani kumtoa mtu aliyeko Motoni na kumuingiza Peponi, au aliyeko Peponi kumpeleka Motoni. Mwenye mamlaka ya siku hiyo ni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwa hivyo washirikina, ambao wamezifanyia dhulma kubwa kabisa nafsi zao na dini ya Allah, siku hiyo watafikwa na adhabu ya Moto ambayo walikuwa wakiikana duniani na kuliona ni jambo muhali. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mazingira ya Siku ya Kiyama ni tofauti na ya duniani. Hapa duniani watu wanaweza kuwanufaisha au kuwasababishia madhara wenzao. Lakini Siku ya Kiyama hakuna mtu atakayekuwa na mamlaka ya jambo lolote, seuze atake kuwanufaisha au kuwasababishia madhara watu wengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kumuelekea mwengine ghairi ya Mwenyezi Mungu ni kujidhulumu mtu nafsi yake, isipokuwa kama Yeye Allah mwenyewe atakuwa amemfanya mtu au watu kuwa wasita na kiunganishi baina yake na waja wake, kama walivyo Mitume.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 43 ambayo inasema:

 وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ قَالُوا مَا هَـٰذَا إِلَّا رَجُلٌ يُرِيدُ أَن يَصُدَّكُمْ عَمَّا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُكُمْ وَقَالُوا مَا هَـٰذَا إِلَّا إِفْكٌ مُّفْتَرًى ۚ وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ

Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi wanasema: Huyu si chochote ila ni mtu anaye taka kukuzuieni na waliyo kuwa wakiabudu baba zenu. Na wakasema: Haya si chochote ila ni uwongo ulio zuliwa. Na walio kufuru waliiambia Haki ilipo wajia: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhaahiri. 

Baada ya aya zilizotangulia zilizozungumzia ukanushaji wa Kiyama unaofanywa na washirikina, aya hii inaashiria ukanushaji wa aya za Qur'ani waliokuwa wakiufanya watu hao hapa duniani na kueleza kwamba: kutokana na taasubi zisizo na msingi walizo nazo kuhusu imani za wazee wao waliotangulia, bila ya kuzingatia mantiki ya Qur'ani na Bwana Mtume SAW wanaamua kuyakanusha maneno hayo ya Mwenyezi Mungu na kutokuwa tayari kuyaamini kwa sababu tu mafundisho yake yanakinzana na mafundisho ya wazee wao waliowatangulia. Dai la pili la washirikina kuhusu Qur'ani ni kwamba aya zake si maneno ya Mwenyezi Mungu, ni maneno ya mwanadamu ambaye anazua kwa kumnasibishia nayo Mola. Na tuhuma ya tatu ya washirikina ni kudai kwamba kama wanatokea watu wanaovutiwa na Qur'ani na kuyakubali maneno ya Bwana Mtume, hiyo inatokana na kipaji cha ufasaha wa maneno yake, na si kwamba ayasemayo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni wazi kwamba tuhuma na madai haya matatu ambayo Qur'ani inayanukuu kutoka kwenye vinywa vya washirikina na makafiri ni maneno ambayo yametamkwa na makundi yao mbalimbali katika zama tofauti za historia ambapo baadhi ya wakati wapinzani wa Mitume walitoa dai moja, wakati mwengine mawili au pengine yote matatu ili kukadhibisha wito wa Manabii hao wa Allah. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuhifadhi turathi za wazee na waliotangulia kunahusiana na athari za kale na za kihistoria; si kulinda na kuendeleza fikra, imani na mila zao zisizo sahihi. Kuwafuata kibubusa na bila ya hoja waliotutangulia ni kizuizi kwa maendeleo na kunadumaza na kuifanya jamii isistawi na kupiga hatua mbele. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mitume wanajulikana mbele za watu kwa ukweli, usafi na utakasifu; wala katu hawakuwa wasema uongo na wenye kuwasingizia watu mambo, sembuse wajitungie kitabu kisha wazue na kudai kwamba kinatoka kwa Mwenyezi Mungu.  Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba uchawi na mazingaombwe ni mambo yanayohitaji mafunzo kutoka kwa walimu waliobobea; na tab'an yanaweza kubatilishwa na watu magwiji wa uchawi. Lakini Mitume hawakupata mafunzo kwa mchawi au mtaalumu yeyote yule wa sihiri. Wao wametumwa na Mwenyezi Mungu ili kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu na wanayaakisi maneno ya haki tu ya Mola wao.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 44 na 45 ambazo zinasema:

 وَمَا آتَيْنَاهُم مِّن كُتُبٍ يَدْرُسُونَهَا ۖ وَمَا أَرْسَلْنَا إِلَيْهِمْ قَبْلَكَ مِن نَّذِيرٍ

Wala hatukuwapa Vitabu wavisome, wala hatukuwatumia Mwonyaji kabla yako wewe.

 وَكَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَمَا بَلَغُوا مِعْشَارَ مَا آتَيْنَاهُمْ فَكَذَّبُوا رُسُلِي ۖفَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ

Na walikadhibisha walio kuwa kabla yao. Na hawakufikilia hata sehemu moja katika kumi ya tulivyo wapa hao. Nao waliwakadhibisha Mitume wangu. Basi kuangamiza kwangu kulikuwa namna gani!

Katika kujibu tuhuma za washirikina dhidi ya Bwana Mtume SAW na kitabu cha mbinguni alichokuja nacho, aya tulizosoma zinasema: kabla ya hapo hakuna Mtume yeyote aliyewahi kutumwa kwa kaumu ya Makureishi wala kitabu walichowahi kuteremshiwa watu hao, hata kwa kutegemea hayo waielezee Qur'ani kuwa ni batili na kumwita aliyekuja nacho kitabu hicho kuwa ni mchawi na muongo. Laiti kama kabla ya hapo wangekuwa wamekujieni Mitume wenye vitabu na nyinyi mkaona kuna migongano kati ya mafundisho ya Nabii Muhammad SAW na Kitabu chake cha Qur'ani na mafundisho ya Mitume hao waliotangulia na vitabu walivyokuja navyo, hapo mngeweza kusema kitabu alichokuja nacho yeye cha Qur'ani ni batili. Sasa ikiwa nyinyi hamna uelewa wowote kuhusu wahyi wa Mwenyezi Mungu, mnaweza kwa msingi gani kudai kwamba Qur'ani ameitunga Mtume SAW na kumtuhumu yeye kwa jambo hilo? Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: washirikina wa Makka wanawezaje kusimama dhidi ya Bwana Mtume SAW hali ya kuwa nguvu na uwezo wao ni mithili ya sehemu moja tu ya kumi ya nguvu walizokuwa nazo watu wa kaumu ambazo tuliziangamiza huko nyuma! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ukanaji na uthibitishaji wa masuala ya kidini inapasa ufanywe kwa ushahidi unaotoka kwenye maandiko ya kidini na sunna za Mitume; haiwezekani kuyapima kwa kutumia elimu na akili ya mwanadamu na kuyakataa au kuyakubali kwa kutegemea vitu hivyo tu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa nguvu na utajiri wa maadui wa dini si lolote si chochote mbele ya nguvu za Allah SW. Kwa hivyo visitutie hofu na kiwewe vitu hivyo bali tushikamane na njia ya Allah na kusimama imara kwa kutakawali na kumtegemea Yeye Mola. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba historia ya waliotangulia ni kioo cha kuangalia watu wa zama hizi na zijazo ili kupata ibra kwamba wasiingiwe na ghururi kwa nguvu zao na kutaka kusimama kukabiliana na Mwenyezi Mungu. Kuna uma na staarabu kadha wa kadha kubwa zimefutwa na kuangamizwa kwa sababu ya kuikana haki. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 771 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atutakabalie amali zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/