Sura ya As-Sabaa, aya ya 46-47 (Darsa ya 772)
Sura ya As-Sabaa, aya ya 46-47 (Darsa ya 772)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 772 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 46 ambayo inasema:
قُلْ إِنَّمَا أَعِظُكُم بِوَاحِدَةٍ ۖ أَن تَقُومُوا لِلَّـهِ مَثْنَىٰ وَفُرَادَىٰ ثُمَّ تَتَفَكَّرُوا ۚ مَا بِصَاحِبِكُم مِّن جِنَّةٍ ۚإِنْ هُوَ إِلَّا نَذِيرٌ لَّكُم بَيْنَ يَدَيْ عَذَابٍ شَدِيدٍ
Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha mfikiri. Mwenzenu huyu hana wazimu. Hakuwa yeye ila ni Mwonyaji kwenu kabla ya kukufikieni adhabu kali.
Katika aya hii na nyengine zinazofuatia za sura hii ya Sabaa, Allah SW anamtaka Mtume wake awatangazie bayana watu utaratibu wake wa tablighi na ulinganiaji wito wa haki. Nukta ya kwanza inayobainishwa na aya hii ni kwamba: ewe Mtume! waambie watu, lengo la wito wangu ni kutaka nyinyi na jamii yenu mtengenekewe. Kama mnataka muokoke na balaa hilo la maovu, madhambi na maasi na mnusurike na adhabu kali kutokana na matendo yenu, inabidi msimame kivitendo kwa ajili ya kujirekebisha nyinyi wenyewe na jamii yenu; tab'an kusimama kwa msingi wa kumwamini Mwenyezi Mungu na kwa ajili yake Yeye Mola, si kwa ajili ya malengo ya kimaada na kidunia. Ikiwa mko tayari kweli, na nia na dhamira yenu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu inapasa kabla ya hatua yoyote ile mrekebishe na kusahihisha kwanza imani na fikra zenu. Katika hili, mkae mtafakari na kujiuliza, Mwenyezi Mungu amekuumbeni kwa lengo gani na anakutakeni mfanye nini? Jiulizeni, Mwenyezi Mungu amekuleteeni Mtume kwa madhumuni gani? Na vilevile fikirieni vizuri juu ya hatima na mwisho wa amali na matendo yenu. Kama mtatafakari kidogo tu mtabaini kuwa Mwenyezi Mungu amemtuma Mtume wake kwa ajili ya kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu; na yeye Mtume hana lengo jengine ghairi ya kuwaonya na kuwapa indhari watu ya adhabu, kutokana na amali na matendo yao maovu. Kama ni hivyo, inawezekanaje mtu anayewataka watu wafikiri na kutafakari, yeye mwenyewe awe ni majinuni na mwendawazimu kama wanavyomtuhumu wapinzani wake? Hivi kweli kila ataye tutahadharisha mimi na wewe kuhusu hatari kubwa inayotukabili, ambayo sisi hatuna uelewa nayo, atakuwa majinuni na mwendawazimu, wakati yeye ana uelewa kamili wa hatari hiyo? Bila shaka katika harakati za kuirekebisha jamii, tusikae kungojea mpaka wajitokeze wengine kuungana na sisi na kusema mathalani kidole kimoja hakibanji chawa, au kutoa hoja kwamba ikiwa akthari ya watu katika jamii wamepotoka, kitu gani sisi tunachoweza kufanya? Bali inatakiwa hata watu wawili wawili, au kama haikuwa, basi hata mtu mmoja mmoja tufanye juhudi za kujirekebisha sisi wenyewe na jamii kwa ujumla. Na wala kutojali watu wengine kusituzuie sisi kutekeleza jukumu letu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mambo hayaendi na kutengenea kwa kukaa kitako tu na kusema; inapasa kusimama na kufanya harakati, tab'an kwa ajili ya Allah SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, katika kusimama na kufanya harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wingi na idadi ya watu sio msingi; kitu muhimu ni ubora wa hatua tunayochukua na nia safi na ya ikhlasi ya tunalolifanya katika njia ya Allah. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, Bwana Mtume SAW aliishi na watu kwa miaka mingi, na alikuwa akijulikana na wote kwa sifa za ukweli, hekima, urazini na uaminifu na wala hakuonekana kuwa na ila hata ndogo kabisa, lakini pamoja na hayo, wakati aliposimama kuwapa indhari washirikina kuhusu mwisho mbaya wa matendo yao maovu walimtuhumu kuwa ni mzushi na mwendawazimu.
Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 47 ambayo inasema:
قُلْ مَا سَأَلْتُكُم مِّنْ أَجْرٍ فَهُوَ لَكُمْ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ
Sema: Ujira nilio kuombeni ni wenu nyinyi. Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Shahidi juu ya kila kitu.
Aya hii pia inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kwa kumtaka Bwana Mtume Muhammad SAW awaeleze watu kuhusu utaratibu wa ulinganiaji wake kwa kuwaambia: mimi sitarajii wala sitaki kitu chochote cha kimaada kutoka kwenu katika kukuelekezeni kwenye njia ya uongofu ya Allah na kukutahadharisheni juu ya Kiyama. Malipo ya kazi yangu nitayapata kwa Mwenyezi Mungu. Kila nililokutakeni mfanye ni kwa manufaa yenu wenyewe, si yangu mimi! Kama mnadhani kuna kitu chochote ambacho nimekutakeni kwa ajili yangu mimi, basi hicho pia ni kwa manufaa yenu nyinyi! Ikiwa ninataka malipo kwenu, mathalani nikakuambieni muwapende Ahlu-Bayt wangu, ni kwa sababu faida ya kufanya hivyo inarejea kwenu nyinyi wenyewe. Natija ya kuwafuata wao ni kwamba mtaipata njia iliyonyooka ya uongofu na wala hamtapotea na kupotoka. Ni kama mwalimu anapowaambia wanafunzi wake: yasomeni vizuri niliyokusomesheni; na baada yangu mimi wafuateni wale niliowafunza mimi. Manufaa ya kufuata maagizo yote hayo mawili huwa yanawarudia wanafunzi wenyewe si mwalimu wao. Mitume wote katika kila zama za historia walikuwa mithili ya walimu wenye huruma na uchungu na wanafunzi wao, kutokana na kuwafunza na kuwaonyesha watu njia sahihi ya maisha, bila ya kuwataka wawape bakhshishi au ujira wowote ule. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wafanya tablighi ya dini hawatakiwi kuwa na tamaa ya kitu kwa watu. Wanapaswa watangaze wazi kuwa hawategemei chochote kwao, na yote wanayofanya ya kuwaelimisha na kuwaelekeza kwenye uongofu ni kutekeleza jukumu na wajibu wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, tusijihisi tuna ihsani ambayo tumemfanyia Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kufuata dini yake na kutekeleza maamrisho yake, kwa sababu yote tunayoyafanya ni kwa manufaa yetu sisi wenyewe wala hayamnufaishi vyovyote Allah SW na Mtume wake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba ikiwa tunaelewa fika kuwa Mwenyezi Mungu anayashuhudia tunayoyafanya, yanatukera nini manenomaneno na tuhuma za baadhi ya watu mpaka kutufanya turudi nyuma katika kazi ya tablighi na kuwaelimisha watu? Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 772 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atujaalie ikhlasi katika amali zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/