Dec 25, 2017 10:57 UTC

Sura ya As-Sabaa, aya ya 48-54 (Darsa ya 773)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 773 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 48 na 49 ambazo zinasema:

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَقْذِفُ بِالْحَقِّ عَلَّامُ الْغُيُوبِ

Sema: Hakika Mola wangu Mlezi hutoa Haki, Mjuzi mno wa ghaibu.

قُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَمَا يُبْدِئُ الْبَاطِلُ وَمَا يُعِيدُ 

Sema: Haki imefika, na batili haijitokezi, wala hairudi.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia katika kubainisha ukweli wa Utume wa Nabii Muhammad SAW na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu, ambaye ni mjuzi na mwelewa wa batini na ya ndani ya nafsi za wanadamu wote anajua ni nani mstahiki wa kupokea wahyi wake. Kwa sababu hiyo amemteua Mtume kuwa mjumbe wake na kumteremshia kwenye moyo wake aya zake ambazo, zote zimeshuka kwa msingi wa ukweli na haki ili awafikishie watu. Kwa kuja Mtume huyo na kufikisha ujumbe wa Allah, haki inawafikia watu na kudhihirika kuwa ghairi ya wito wa kumuelekea Yeye Mola, miito mingine yote ni batili, na yeyote au chochote kingine kinachotangazwa kwa watu badala ya Mwenyezi Mungu, hakina uwezo wa kuumba kitu au kukirejesha kile kilichotoweka. Ukafiri na shirki ni njia za batili ambazo hazina nguvu na uwezo wa kudumu wa kukabiliana na haki. Bila shaka ni wazi kwamba kabla ya watu kudhihirikiwa na haki, batili hutamba na kujifaragua na kutaka kujionyesha kuwa ni yenye nguvu na ya kudumu, lakini kipindi cha kudumu batili ni kifupi na hutoweka haraka kuliko inavyoweza kufikiriwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu ni haki, na kila kinachotoka kwake Yeye ni ukweli na haki. Kipimo cha haki na batili ni kauli na matendo yanayofuata njia ya Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, haki ni yenye kushinda dhidi ya batili na kiujumla batili haina uwezo wowote wa kukabiliana na haki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba mwanzo na mwisho wa dunia uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, lakini katikati yake zinashuhudiwa harakati za batili ambazo kama lilivyo povu linaloelea juu ya maji, mwishowe hutoweka tu.

Ifuatayo sasa ni aya ya 50 ambayo inasema:

قُلْ إِن ضَلَلْتُ فَإِنَّمَا أَضِلُّ عَلَىٰ نَفْسِي ۖ وَإِنِ اهْتَدَيْتُ فَبِمَا يُوحِي إِلَيَّ رَبِّي ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ

Sema: Ikiwa mimi nimepotea, basi nimepotea kwa kuidhuru nafsi yangu mwenyewe. Na ikiwa nimeongoka, basi ni kwa sababu ya kuniletea wahyi Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu. 

Katika aya hii, Allah SW anamtaka Mtume wake awatangazie watu kwamba hata mimi ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu nimeufikia uongofu kupitia wahyi wake Mola; na lau kama usingekuwa wahyi wa Allah, mimi pia kama walivyo watu wengine ningekuwa nimepotea. Ni wazi kwamba akili nayo pia ni wenzo wa muongozo wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Lakini bila ya kuwepo nuru ya wahyi, si hasha kutokana na kuwepo njia kadha wa kadha, akili nayo ikafanya makosa katika kupambanua baina ya haki na batili na kumfanya mtu aishie kwenye njia ya upotofu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kabla ya kuwaathiri watu wengine, athari na matokeo ya kupotoka au kuongoka mtu humrejea zaidi yeye mwenyewe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanadamu, ni mjuzi na mwelewa wa hali na mahitaji yake, wala hakuna mpaka na kizuizi chochote baina yake na viumbe wake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 51 na 52 ambazo zinasema:

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ فَزِعُوا فَلَا فَوْتَ وَأُخِذُوا مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ

Na lau ungeli ona watapo fazaika, basi hapana pa kukimbilia! Na watakamatwa mahala pa karibu.

 وَقَالُوا آمَنَّا بِهِ وَأَنَّىٰ لَهُمُ التَّنَاوُشُ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ

Na watasema: Tunaiamini! Lakini watapata wapi kutoka huko mahali mbali?

Katika aya hizi na zitakazofuatia ambazo ni aya za mwisho za sura hii ya Sabaa Mwenyezi Mungu SW anampa habari Mtume wake na waumini kwamba wakanushaji wa Qur’ani na Kiyama, ambao hawako tayari kuikubali haki, kuna siku watakuja kupiga mayowe makubwa na kuingiwa na fazaa kubwa, lakini yote hayo hayatokuwa na faida yoyote kwao. Siku hiyo watatangaza kuiamini haki, lakini imani bila ya amali haina thamani. Kama ambavyo imani hiyo itakayodhihirishwa baada ya kuiona adhabu ya Siku ya Kiyama haitomfalia mtu kitu. Kwa sababu mtu anatakiwa aamini kwa hiari na kwa uelewa, si kwa sababu ya hofu na kulazimika. Si hapa duniani wala huko akhera ambako mtu mwovu yeyote yule atakuwa na uwezo wa kuzikwepa nguvu na mamlaka ya Mwenyezi Mungu; kama ambavyo Yeye Mola mwenyewe yu karibu mno na waja wake, rehma na ghadhabu zake pia ziko karibu mno na waja wake walio wema au waovu;  uwe ni ukaribu wa mahali, zama au nafasi na hadhi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutubia kutokana na fikra na amali potofu kunawezekana hapa duniani tu, lakini fursa ya kufanya hivyo haitopatikana katu huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ni jambo la kutarajiwa kwa kila kafiri kuamini pale aionapo adhabu na hatari; lakini imani yenye thamani ni ile inayotokana na hiari na uelewa, si ya kulazimika na kwa sababu ya woga na hofu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba adhabu na ghadhabu za Allah haziko mbali; atakapo Yeye Mola, zinaweza kumfika mtu mahali popote pale na wakati wowote ule.

Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 53 na 54 ambazo zinasema:

وَقَدْ كَفَرُوا بِهِ مِن قَبْلُ ۖ وَيَقْذِفُونَ بِالْغَيْبِ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ 

Na hapo kabla yake waliikataa, na wakiyatupilia mbali maneno ya ghaibu kutoka mahali mbali. 

وَحِيلَ بَيْنَهُمْ وَبَيْنَ مَا يَشْتَهُونَ كَمَا فُعِلَ بِأَشْيَاعِهِم مِّن قَبْلُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا فِي شَكٍّ مُّرِيبٍ

Na watawekewa kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani, kama walivyo fanyiwa wenzao zamani. Hakika hao walikuwa na shaka ya kutia wasiwasi. 

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia na kueleza kwamba: wale ambao leo akhera wanaiamini haki baada ya kuiona adhabu ya Mwenyezi Mungu, walipokuwa duniani waliikanusha Qur’ani na Utume wa Nabii Muhammad SAW. Bila ya hoja yoyote waliupinga ukweli kuhusu ulimwengu wa ghaibu unaojumuisha asili ya uumbaji na marejeo ya viumbe, yaani kufufuliwa kwao Siku ya Kiyama. Wakamtuhumu pia Bwana Mtume SAW kuwa ni mchawi au mwendawazimu na hawakuwa tayari kuyatafakari maneno na mwenendo wake. Ni kawaida kwamba wakanushaji wa Kiyama huwa siku zote wanafikiria raha na starehe zao tu, na kwa sababu hiyo huwa hawayakubali maneno ya Mitume. Lakini raha na starehe zao hizo hazidumu, bali mauti huwatenganisha na matarajio na matamanio yao hayo, kama ambavyo makafiri na wakanushaji haki wa kabla yao pia waliondoka duniani bila ya kuyafikia mengi waliyoyataka na waliyoyatarajia. Katika aya ya mwisho ya sura hii ya Sabaa, Allah SW anatueleza kwamba chanzo cha matatizo yote haya ni shaka zisizo na msingi. Ni kawaida kwa watu wote kuwa na shaka juu ya mambo mbalimbali, lakini inapasa mtu aondokane na shaka hizo kwa kutafakari na kufanya utafiti mpaka afikie kwenye yakini na hakika ya jambo. Kusema tu kwamba mimi nilikuwa na shaka kama mtu huyu kweli ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kama maneno yake ni wahyi wa mbinguni, si hoja itakayokubalika mbele ya Mola. Kwa sababu ungeliweza kufikia kwenye natija kwa kutafakari na kutumia akili na kuondokana na hali hiyo ya dhana, shaka na hatihati. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kukufuru na kukanusha asili na marejeo ya viumbe hakuna mashiko ya kielimu na kimantiki isipokuwa ni dhana na makisio tu yasiyo na msingi, sawa na kutia mkono gizani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa raha na starehe za dunia zina mwisho; tufikirie raha na starehe za kudumu na za milele za huko akhera. Aidha aya hizi zinatutaka tuamue moja kuhusu msimamo wetu juu ya ukweli wa Qur’ani na Siku ya Kiyama ili tusiendelee kubaki na shaka hadi mwisho wa umri wetu, kwani madhara ya hali hiyo ni makubwa mno. Kwa maelezo haya wapenzi wasikilizaji, tunahitimisha tarjumi na maelezo ya Suratu Sabaa. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kufaidika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/