Jumapili, Disemba 31, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1439 Hijria, mwafaka na tarehe 31 Disemba 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1307 iliyopita aliingia madarakani Abul-Abbas Abdullah Ibn Muhammad, maarufu kwa jina ‘Saffah’ khalifa wa kwanza wa utawala wa Bani Abbas. Ni vyema kukumbusha kwamba watawala wa Bani Abbasi kwa kushirikiana na Abu Muslim Khurasan na jeshi lake, walimuua mtawala wa mwisho wa Bani Umayyah Marwan wa Pili, na huo ndio ukawa mwisho wa utawala wa Bani Umayyah. Hata hivyo Bani Abbas kama walivyokuwa Bani Umayyah nao kwa miaka kadhaa walitawala kwa dhulma na ukandamizaji sambamba na kupora mali za watu wa mataifa ya Kiislamu. Utawala wao uliendelea hadi mwaka 656 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 503 iliyopita alizaliwa katika mji mkuu wa Ubegiji Brussels, Andrea Vesalius tabibu na daktari mpasuaji mashuhuri wa nchi hiyo. Umashuhuri wa daktari huyo ulitokana zaidi na juhudi zake alizofanya za kufahamu utendaji wa viungo mbali mbali vya mwili. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Andrea Vesalius akajulikana kwa jina la baba wa elimu ya anatomia yaani sayansi inayohusu mwili na viungo vyake. Tabibu huyo aliaga dunia mwaka 1564.

Siku kama ya leo miaka 326 iliyopita, alifariki dunia Robert Boyle mwanafizikia na mwanakemia wa Ireland. Alizaliwa mwaka 1627 na kuwa chini ya ungalizi na usimamizi wa baba yake ambaye alikuwa akihesabiwa kuwa mmoja wa wanafizikia mashuhuri wa Uingereza. Robert Boyle alisoma masomo yake na kufanikiwa kubobea katika taaluma ya fizikia. Mtaalmu huyo pia alifanya utafiti mwingi katika uga wa kemia.

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita alizaliwa Henri Émile Benoît Matisse, mchoraji maarufu wa Ufaransa. Baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari na kwa pendekezo la baba yake alielekea mjini Paris kwa ajili ya kusomea sheria. Hata hivyo badala ya sheria, Matisse alijifunza uchoraji. Baada ya kuchora vibao kadhaa alifungua maonyesho ya athari zake akiwa na umri wa miaka 27 ambapo moja ya athari zake ilinunuliwa na serikali ya Ufaransa. Ndoto yake ilikuwa ni kuanzisha mfumo mpya wa tasnia ya uchoraji, ambapo katika uwanja huo alifanya tafiti mbalimbali katika fani hiyo na kufanikiwa kukamilisha athari ya Henri Matisse, ambapo mwaka 1905 akishirikiana na wachoraji wengine walianzisha mfumo wa uchoraji kwa jina la Fauvism au ‘Fauves’. Henri Émile Benoît Matisse alifariki dunia tarehe 3 Novemba 1945 akiwa na umri wa miaka 85.

Katika siku kama ya leo miaka 142 iliyopita, Arthur Christensen Mtaalamu wa mambo ya nchi za Mashariki wa Denmark alizaliwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Copenhagen. Katika kipindi cha masomo yake, Christensen alikuwa na mapenzi makubwa na masuala ya nchi za Mashariki hususan Iran. Baadaye alifanya utafiti kuhusiana na historia na fasihi ya Iran. Mtaalamu huyo wa nchi za Mashariki alikuwa akiifahamu vizuri lugha ya kifarsi na aliandika kitabu alichokipa jina la “Iran Katika Zama za Wasasani”. Arthur Christensen aliaga dunia mwaka 1945.

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ‘Redio Tehran’ ilianza kurusha matangazo yake kwa ajili ya wasikilizaji wa maeneo ya mashariki na katikati mwa Afrika. Redio Tehran imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za uandishi zikiwemo za kuandaa taarifa za habari, vipindi vya kiuchumi, kisiasa, kidini na kijamii. Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanasikika katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi.

Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, Rais Boris Yeltsin wa Russia alijiuzulu na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin. Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi. Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa zake kushindwa. Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia
