Jan 22, 2018 06:42 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jan 22

Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu katika dakika hizi chache zilizotengwa kwa ajili ya kuangazia matukio mawili matatu ya michezo yaliyogonga vichwa vya habari kitaifa na kimataifa. Usibanduke kando ya radio yako hadi tamati ya kipindi……..Karibu…..

Handiboli: Iran yaanza vyema Korea Kusini

Timu ya taifa ya handiboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza vyema mashindano ya mabingwa wa mchezo huo barani Asia yanayofanyika nchini Korea Kusini. Siku ya Jumamosi, vijana wa Iran waliwabamiza wenzao wa Japan magoli 37-32, katika mchuano wa mwisho wa hatua ya makundi, uliopigwa katika Ukumbi wa Seo-Suwon Chilbo, mjini Suwon, yapata kilomita 30 kusini mwa mji mkuu Seoul.

Timu ya taifa ya handiboli ya Iran

Kabla ya hapo, Iran iliichabanga Uzbekistan mabao 37-18 katika mechi ya ufunguzi. Timu hiyo ya mpira wa mkono ya Iran itatoana udhia na mwenyeji Korea Kusinin siku ya Jumanne. Iran ipo katika Kundi A pamoja na Iraq na Japan, huku Kundi B likizijumuisha Australia, Bahrain, Oman na Uzbekistan. Mwenyeji Korea Kusini ipo katika Kundi C pamoja na Bangladesh, Imarati na India huku Kundi D likizileta pamoja China, New Zealand, Qatar na Saudi Arabia. Duru ya 18 ya mashindano hayo ya kikanda inapigwa mjini Suwon, huko Korea Kusini kati ya Januari 18 na 28, na mabingwa wataliwakilisha bara Asia katika mashindano ya dunia mwaka ujao 2019.

Muirani atwaa medali katika ukweaji theluji

Mohammad Reza Safdarian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka katika nafasi ya tatu na kutwaa medali ya fedha katika mashindano ya kimataifa ya kukwea theluji yaliyofanyika nchini Uswisi. Muirani huyo aliibuka wa tatu katika siku ya mwisho ya mashindano hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Saas-Fee. Raia wa Russia, Alexey Dengin ndiye aliyeibuka kidedea na kutwaa medali ya dhahabu huku mwenzake Maxim Tomilov akiibuka wa pili na kutia kibindoni medali ya fedha. Mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kwa Kiingereza kama 2018 UIAA Ice Climbing World Tour yalianza Januari 19 na kufunga pazia lake siku iliyofuatia. Wanamichezo zaidi ya 300 kutoka nchi 20 duniani ikiwemo Iran, Marekani na Korea Kusini wameshiriki mashindano hayo.

Michuano ya CHAN

Timu ya taifa ya Uganda na Ivory Coast zimeondolewa katika fainali ya michuano ya mataifa bingwa barani Afrika CHAN, kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani. Michuano hii inaendelea nchini Morocco na mataifa haya mawili, yamelazimika kuondoka katika michuano hii mapema baada ya kupoteza michuano yao ya pili katika kundi B. Matokeo haya mabaya, yameyaacha Zambia na Namibia kufuzu katika hatua ya robo fainali kuwania taji hili la tano. Zambia ilipata ushindi wake wa pili, baada ya kuifunga Ivory Coast mabao 2-1 huku Namibia ikiifunga Uganda bao 1-0 katika dakika za lala salama kwenye mchuano ulipigwa katika uwanja wa Marrakech. Uganda Cranes watachuana na Ivory Coast katika mechi ya kujaribu kupata ushindi angalau katika mashindano haya kabla ya marudio jijini Kampala.

Morocco, mwenyeji wa CHAN 2018

Uganda imekuwa na bahati mbaya katika mashindano haya tangu mwaka 2011, 2014 na 2016 na kipindi chote hicho, imeondolewa katika hatua ya makundi. Morocco na Sudan tayari zimefuzu katika hatua ya robo fainali baada ya kufanya vema katika mechi mbili zilizopita. Wenyeji Morocco imefuzu katika hatua ya robo fainali kuwania taji la CHAN kwa wachezaji wanocheza soka katika ligi za nchi zao. Hatua hii ilikuja baada ya timu hiyo kushinda mechi yake ya pili dhidi ya Guinea kwa kuifunga mabao 3-1. Ayoub El Kaabi alikuwa kinara wa mchuano kwa kufunga mabao yote matatu katika dakika ya 27, 65 na 68. Morocco ipo kileleni mwa Kundi A licha ya kutoa sare ya 0-0 na Sudan katika mechi ya aina yake iliyopigwa katika uwanja wa Casablanca Jumapili. Sudan nayo ilijikatia tiketi kutoka kundi hilo baada ya kuishinda Mauritania bao 1-0 katika mechi yake ya pili. Morocco inaongoza kundi la A kwa alama 9 huku Sudan ikiwa na alama 6. Guinea wamemaliza kampeni zao kwenye michuano hii kwa ushindi wa bao 1-0 waliposhika dimbani kuvaana na Mauritania. Cameroon wameyaaga mashindano hayo baada ya kuzabwa bao 1-0 na Angola.

Ligi ya Premier

Mabao ya hat-trick ya Sergio Aguero yaliipaisha Manchester City na kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 ilipochuana na Newcastle katika mchuano wa kukata na shoka wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Huku wakiupiga nyumbani, vijana wa City walionyesha mchezo wa kufaana na kutamalaki mpira kwa kiasi kikubwa. Aguero alifunga bao lake la kwanza katika dakika ya 34, huku akifung la pili kwa mkwaju wa panati dakika ya 63 kabla ya kupiga msumari wa mwisho kwenye jeneza za Newcastle katika dakika ya 83.

Bao la kufutia machozi la Newcastle lilitiwa kimyani na Jacob Murphy katika dakika ya 67. Man City inasalia kileleni mwa jedwali la Ligi ya EPL ikiwa na alama 65, ikifuatiwa na Manchester United ambayo iliizima Burnley kwa bao 1-0. Mchuano mwingine uliobua gumzo kwenye ligi ya Premier ni ule kati ya Arsenal na Crystal Palace. Gunners waliponyoka na alama tatu muhimu kwa kuizaba Palace mabao 4-1. Mabao ya Wabeba Bunduki wa Uingereza yalifungwa na Nacho Monreal, Alex Iwobi, Laurent Koscielny na Alexndre Lacazette. Arsenal kwa sasa wanalazimia kuridhika na nafasi ya sita wakiwa na pointi 42, nyuma ya Tottenham yenye alama 45. Chelsea wanafunga orodha ya tatu bora wakiwa na alama 50. The Blues wamejiongezea alama tatu nyeti kwa kuisasambua Albion mabao 4-0.

 

Tags