Feb 25, 2018 04:30 UTC
  • Jumapili tarehe 25, Februari, 2018.

Leo ni Jumapili tarehe nane Jamadi th-Thani 1439 Hijiria, sawa na tarehe 25 Februari mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, alizaliwa Benedetto Croce, mmoja wa wanafalsafa wakubwa wa Italia. Akiwa kijana mdogo, alipoteza familia yake katika ajali ya tetemeko la ardhi ambapo naye pia alisalia chini ya kifusi kwa muda wa masaa 12. Tukio hilo lilikuwa na athari kubwa katika maisha ya Croce ambapo hadi mwisho wa umri wake alikuwa akipinga kila aina ya mapinduzi. Mwaka 1893 Miladia Benedetto Croce alitoa Makala yake ya kwanza ya falsafa. Hata hivyo mwaka 1900 alitoa makala yake nyingine ya ukosoaji huku mwaka 1910 akifanikiwa kuwa seneta wa kudumu katika bunge la Italia ingawa pamoja na hayo hakuwa na harakati kubwa za kisiasa. Katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia alikuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo nchini humo. Benedetto Croce alifariki dunia mwaka 1952.

Benedetto Croce

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, alizaliwa mjini Khorasan, moja ya miji ya Iran Sheikh Muhammad Muhaqqiq Bahlul, mmoja wa maulama wakubwa na mahatibu wa zama zake. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi kwa baba yake alielekea mjini Sabzevar kwa ajili ya kujiendeleza kimasomo. Baada ya tukio la kuwalazimisha wanawake wa Iran kuvua hijabu kufuatia amri ya mtawala wa wakati huo, Reza Shah Pahlavi, Sheikh Bahlul alitoa hotuba kali kwa Waislamu wa mji wa Mash'had ndani ya msikiti wa Goharshad dhidi ya utawala huo wa kifalme. Kufuatia hali hiyo utawala huo ulifanya mauaji makubwa dhidi ya wananchi na wafanyaziara katika haramu ya Imam Ridha (as) mjini hapo. Baada ya hapo Sheikh Muhammad Muhaqqiq Bahlul alilazimika kujificha na kukimbilia nchini Afghanistan. Kwa kuzingatia kuwa utawala wa Afghanistan wakati huo ulikuwa na mahusiano mazuri na Iran na kwa kukhofia kuharibika mahusiano ya pande mbili, Kabul ilimtia mbaroni Sheikh Bahlul ambapo alibakia jela nchini humo kwa kipindi cha miaka 30. Baada ya kuachiliwa huru Sheikh Bahlul alirudi kwa muda mfupi nchini  Iran kisha akasafiri Misri, Iraq na baadhi ya nchi za Kiislamu huku akirejea tena Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa mwaka 1979.

Sheikh Muhammad Muhaqqiq Bahlul

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Abd al-Husayn Sharaf al-Din al-Musawi. Al-Musawi Aamili alizaliwa mwaka 1290 Hijiria mjini Kadhimiya, moja ya miji ya Iraq, na baada ya kuhitimu masomo yake ya kidini alielekea mjini Jabal Amel nchini Lebanon ambapo akiwa huko alijishughulisha na harakati za Kiislamu. Alimu huyo wa daraja kubwa alitoa huduma kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa kazi zake muhimu ilikuwa ni kulingania umoja kati ya Waislamu duniani na katika uwanja huo aliandika pia vitabu na makala mbalimbali.

Ayatullah Abd al-Husayn Sharaf al-Din al-Musawi

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, ndege za kijeshi za utawala wa Saddam, ziliishambulia kwa mabomu miji midogo ya Saqqez, Pol-e Dokhtar na Mahabad nchini Iran. Kufuatia jeshi vamizi la Iraq kushindwa vibaya na wanamapambano Waislamu wa lran katika operesheni kadhaa za eneo la kisiwa cha Majnoon, utawala huo wa Baathi uliamua kutekeleza mashambulizi ya kinyama dhidi ya maeneo ya makazi ya raia nchini Iran. Katika mashambulizi hayo miji tofauti ya Khorramabad na Borujerd ililengwa na makombora manne huku miji ya Saqqez, Pol-e Dokhtar na Mahabad nayo ikishambuliwa vibaya. Karibu raia 50 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 400 kujeruhiwa.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, dikteta wa zamani wa Ufilipino aliyekuwa amejitangaza rais wa maisha, Ferdinand Marcos, alikimbia nchi hiyo akiwa pamoja na familia yake. Marcos alichukua hatamu za uongozi mwaka 1965. Alidumisha utawala wake wa kidikteta na ukandamizaji nchini Ufilipino kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwaka 1973 Ferdinand Marcos alijitangaza kuwa rais wa maisha wa Ufilipino. Wakati huo wananchi katika maeneo mbalimbali walikuwa tayari wameanzisha harakati za mapambano ya kisiasa na kijeshi dhidi ya dikteta huyo. Mapambano hayo yalishika kasi zaidi katikati ya muongo wa 1980, na Februari 25 1986 Marcos akalazimika kuikimbia Ufilipino.

Ferdinand Marcos

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi Waislamu 29 miongoni mwao. Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru katili huyo kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani!

Mji wa al-Khalil

Tags