Ulimwengu wa Michezo, Feb 26
Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita...
Judoka wa Iran atwaa dhahabu Grand Slam Ujerumani
Bingwa wa mchezo wa judo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametunukiwa medali ya dhahabu baada ya kuonyesha mchezo wa kufana katika mashindano ya kimataifa ya Düsseldorf Grand Slam 2018 nchini Ujerumani. Saeid Mollaei mwenye umri wa miaka 26 aliibuka mshindi katika mpambano wa fainali na hasimu wake Alpha Oumar Djalo raia wa Ufaransa, kwa wachezaji wenye kilo zisizozidi 81. Judoka huyo wa Iran amepongezwa kwa kuonyesha ustadi na ufundi wa hali ya juu katika mpambano huo wa mwisho uliompa dhahabu siku ya Jumamosi.
Mjerumani Dominic Ressel na Aslan Lappinagov wa Russia walilazimika kutuzwa medali ya shaba kwa pamoja. Mashindano hayo ya judo ya Düsseldorf Grand Slam 2018 yalianza Februari 23 na kuunga pazia lake Jumapili Februari 25.
Wanajudoka 446 wa kike na kiume kutoka nchi 65 duniani, zikiwemo Iran, Azerbaijan, Ubelgiji, Bulgaria, Ufaransa, Ujerumani, Uingerea, Japan na Russia walishiriki mashindano hayo ya dunia.
Iran yaishtaki Saudia AFC
Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran FFIRI limeishtaki klabu ya al-Hilal ya Saudi Arabia kwa Shirikisho la Soka barani Asia AFC, baada ya wachezaji wa timu hiyo kukataa kukimya kwa sekunde chache, ishara ya heshima kwa wahanga wa ajali ya ndege ya Iran iliyoua makumi ya watu. Jumanne iliyopita katika uwanja wa Seeb kaskazini mashariki mwa Oman, wakati ambapo wachezaji wa klabu ya Esteqlal ya Iran waliposimama na kunyamaza kimya kwa ajili ya kutoa heshima zao kwa wahanga wa ajali hiyo, wachezaji wa al-Hilal ya Saudia walikataa kusimama mkabala na wachezaji wa Iran kwa ajili ya kuonyesha heshima kwa familia za wahanga wa ajali hiyo.
Ndege ya Shirika la Aseman ya Iran ilianguka katika eneo la Semirom katika mkoa wa Isfahan katikati mwa Iran na watu wote 66 waliokuwemo ndani yake walifariki dunia. Marais, viongozi na shakhsia wa nchi mbalimbali duniani wametoa mkono wao wa rambirambi kufuatia ajali hiyo. Licha ya dharau na majivuno hayo, vijana wa Iran waliwachabanga Wasaudi bao 1-0 katika mchuano wa Kundi B.
Hii sio mara ya kwanza kwa wachezaji wa Saudia kupuuza au kutotoa heshima kwa familia, jamaa na marafiki wa wahanga wa matukio ya majonzi. Juni mwaka 2017, timu ya taifa ya soka ya Saudia ilipuuza kusimama kwa dakika moja wakiwa kimya kwa ajili ya heshimi kwa wahanga wa shambulizi la kigaidi la London, kabla ya mchuano wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Australia katika Uwanja wa Adelaide Oval.
Huku hayo yakirifiwa, Balozi wa Qatar nchini Ujeumani, Sheikh Saoud bin Abdulrahman Al Thani, ameutaja kama uvumi usiokuwa na maana tetesi zilizotolewa na Turki al-Sheikh, Waziri wa Michezo wa Saudia aliyedai kuwa, yumkini Doha ikapokonywa haki ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2022. Ameyataja madai hayo kama propaganda zenye lengo la kuichafua Qatar.
Rais wa FIFA aitembele Tanzania
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino aliwasilia jijini Dar es Salaam Jumatano usiku kwa ajili ya mkutano uliofanyika siku ya Alkhamisi, katika Ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere Mjini Dar es Salaam. Gianni Infantino alifuatana na Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) Ahmad Ahmad. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe aliongoza mapokezi kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Akizungumza baada ya kumpokea kiongozi huyo Waziri Mwakyembe alisema Tanzania iko tayari kutoa ushirikiano kwa mikakati mbalimbali ya Fifa yenye lengo la kuinua soka la Afrika. Aidha alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Agenda kadhaa zilizojadiliwa kwenye mkutano kati ya Infantiono na wakuu wa soka Tanzania ni pamoja na utoaji wa Fedha za FIFA kwa ajili ya maendeleo ya mchezo wa soka, changamoto za usajili wa wachezaji kwa kutumia mtandao yaani Transfer Matching System (TMS) na kalenda ya kimataifa ya FIFA. Hali kadhalika Rais wa FIFA alikutana na waandishi wa habari ambapo aliyatolewa maelezo masuala mazito yanayofungamana na uhusiano wa mpira wa soka wa Tanzania na shirikisho hilo. Kabla ya kuja Tanzania, Rais wa FIFA alizitembelea nchi za Nigeria na Ghana.
Mkenya aibuka kidedea Tokyo Marathon
Mwanariadha nyota wa Kenya, Dickson Chumba ameibuka kidedea katika mbio za Tokyo Marathon nchini Japan siku ya Jumapili. Chumba ambaye ni mshindi wa mashindano haya ya mwaka 2014 ameibuka mshindi kwa kutumia saa mbili, dakika tano na sekunde 30. Licha ya kuibuka wa pili kwa kutumia sekunde 41 zaidi ya Mkenya Dickson Chumba, Yuta Shitara wa Japan amevunja rekodi ya nchi hiyo.
Mkenya mwingine Amos Kipruto amefunga orodha ya tatu bora kwa kutumia saa mbili, dakika sita na sekunde 33. Ushindi mwenyeji Mjapani wa saa mbili, dakika 6 na sekunde 11 ndio bora zaidi katika historia ya mbio za nyika nchini humo, ikizingatiwa kuwa amevunja rekodi ya mwanariadha mkongwe Toshinari Takaoka aliyetumia saa mbili, dakika 6 na sekunde 16 katika mbio za Chichago Marathon mwaka 2002.
Katika safu ya wanawake, Waethiopia Birhame Dibaba na Ruti Aga wameibuka wa kwanza na wa pili kwa usanjari huo, huku Mmarekani Amy Cragg akiibuka wa tatu.
Ligi ya EPL
Tututupie jicho matokeo ya baadhi ya mechi zilizopigwa kwenye Ligi Kuu ya Soka Uingereza. Manchester United siku ya Jumapili ilirudi katika nafasi ya pili baada ya kiungo wake Jesse Lingard kuwapa ushindi kwenye mchuano wa aina yake dhidi ya Chelsea nyumbani Old Trafford. Iliwalazimu Man U kufanya kazi ya ziada baada ya Chelsea kupata goli wa kwanza na kuwa kifua mbele kwenye kipindi cha kwanza. Baada ya mapumziko, United walijipapatua na kujikusanya upya, ambapo Romelu Lukaku alimtangulia Marcos Alonso na kuisawazishia Man U na kuwa bao lake la kwanza dhidi ya klabu yake ya zamani. Lukaku alimpa Lingard pasi nsafi zikiwa zimesalia dakika 15 mechi ikamilie na bila kuchelewa akapachika wavuni.
Chelsea watabaki katika nafasi ya tano baada ya Tottenham kuwashinda Crystal Palace bao 1-0 siku hiyo hiyo. Awali klabu ya Liverpool ilikuwa imewaondoa kwa muda Mashetani Wekunduu katika nafasi ya pili baada ya kuikandamiza West Ham United kwa mabao 4-1 katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Uingereza. Kocha wa timu hiyo Jurgen Klopp amesema kuwa amefurahishwa sana na matokeo hayo, kwani yanazidi kuiweka Liverpool katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo. Washambuliaji wao, Mohamed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane wote walizifumania nyavu katika kipindi cha pili katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Anfield. Emre Can aliipatia Liverpoo bao la kuongoza akifungwa kwa mpira wa kona baada ya lile la Salah ya kushindwa kuingia wavuni baada ya kugonga mwamba. Salah aliifanya Liverpool kuwa mbele kwa mabao 2-0 baada ya kupiga shuti hafifu baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Alex Oxlade-Chamberlain, kabla Firmino hajaongeza baada ya kosa la kipa Adrian. Mtoka benchi Michail Antonio, aliifungia West Ham na kuirejeshea matumaini, lakini Mane, aliyegonga mwamba muda mfupi kabla, alikamilisha ushindi kwa Liverpool.
Man City yatwaa Kombe la Carabao
Kwengineko, klabu ya Manchester City imetwaa Kombe la Carabao baada ya kuigeuza kichwa cha mwendawazimu Arsenal katika fainali ya kukata na shoka iliyotimua mavumbi kwenye uwanja wa Wembley siku ya Jumapili.
Man City wameshinda taji hilo kwa kuigaragaza Gunners magoli 3-0 katika mchezo ambao City ilitawala kwa kiasi kikubwa. Magoli ya City yalipachikwa na Sergio Aguero, Vincent Kompany na David Silva.
.................................TAMATI...........................