Ijumaa tarehe Pili Machi, 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 13 Jamadithani 1439 Hijria sawa na Pili Machi 2018.
Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, mwafaka na tarehe Pili Machi mwaka 2004, mamia ya watu wasio na hatia waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika miripuko kadhaa mikubwa iliyotokea katika maadhimisho ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) huko katika miji mitukufu ya Karbala na Kadhimein nchini Iraq. Katika mwaka huo wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maadhimisho hayo kwa hamasa kubwa baada ya utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani, kupiga marufuku kwa miaka kadhaa shughuli zote za aina hiyo. Miripuko hiyo ya kigaidi ya Karbala na Khadhimein ilitokea ikiwa ni muendelezo wa machafuko yaliyoikumba Iraq tangu nchi hiyo ivamiwe kijeshi na kukaliwa kwa mabavu na Marekani na Uingereza mwaka 2003.

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, nchi ya Morocco ilipata uhuru. Morocco iko kaskazini mwa Afrika katika Ukingo wa Bahari ya Mediterranean na Bahari ya Atlantic na inapakana na Algeria na Sahara Magharibi. Ukoloni wa madola ya Ulaya dhidi ya nchi hiyo, ulianza tangu karne ya 15 Miladia. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Morocco dhidi ya wakoloni wa Uhispania na Ufaransa yalipelekea nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka 1956.

Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, mwanafizikia wa Kifaransa Henri Becquerel alivumbua mionzi ya nunurishi yaani radioactive. Henri alifikia mafanikio hayo baada ya kufanya tafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo. Becquerel alikuwa akichunguza urani ndipo alipogundua mionzi hiyo. Utafiti wa mwanafizikia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tunzo ya amani ya Nobel mwaka 1903 na miaka mitano baadae aliaga dunia.

Siku kama ya leo miaka 1009 iliyopita alifariki dunia Ibn Haytham, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Cairo. Ibn Haytham alizaliwa mwaka 354 Hijiria katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Alibobea katika elimu za fizikia, tiba, falsafa na unajimu. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya hisabati, nujumu na tiba. Moja ya vitabu vyake muhimu ni al-Manadhir ambacho kimetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na kinatumika katika elimu ya nujumu.
