Sura ya Faat'ir, aya ya 1-2 (Darsa ya 774)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 774.
Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya 34 ya Sabaa, katika darsa hii ya 774 tutaanza kuizungumzia sura ya 35 ya Faat'ir. Sura hii imeteremshwa Makka na ina aya 45. Katika aya ya mwanzo ya sura hii Mwenyezi Mungu SW ametajwa kwa sifa ya Faat'ir, yaani Muumbaji, na jina la sura hii limetokana na aya hii. Tunaianza sasa darsa yetu kwa aya yake ya kwanza ambayo inasema:
الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۚ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ
Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi, aliye wafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili, na tatu- tatu, na nne-nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
Sura hii kama zilivyo baadhi ya sura nyengine za Qur'ani kama Suratul Faatiha inaanza kwa kumhimidi, kumshukuru na kumsifu Allah SW. Kumhimidi kwa sababu ulimwengu wote wa maumbile pamoja na adhama yake yote mbinguni na ardhini, vyote hivyo vimeumbwa kwa nguvu na uwezo wake Yeye. Bila ya shaka tadbiri na uendeshaji wa mambo yote ya vitu hivyo unafanywa na Malaika ambao nao pia wameumbwa na Yeye Allah SW. Kwa kuzingatia kwamba kila Malaika ana kazi na jukumu lake maalumu, na uwezo na mamlaka ya kila Malaika yanatafautiana na ya mwenzake, Qur'ani imewapambanua kwa kutumia msamiati wa mbawa mbili mbili, tatu tatu na nne nne, ambazo inavyoonekana umefanyika kwa madhumuni ya kubainisha uwezo na daraja tofauti walizonazo viumbe hao. Ni wazi kuwa Malaika si viumbe wa kimaada na haiwezekani kutasawari mbawa za ndege na kuwanasibishia nazo Malaika. Fasili hii ina maana ya kitu kisicho cha kimaada iliyotumiwa kuikurubisha akili kwenye uelewa wa kitu kwa kutumia msamiati wa kimaada, sawa kabisa na yalivyotumika ndani ya Qur'ani maneno kama Arshi, Kursiy, Loho na Kalamu. Baada ya aya kuwaashiria Malaika inatilia mkazo nukta hii, kwamba isidhaniwe Mwenyezi Mungu aliuumba ulimwengu huko nyuma kisha akauacha kama ulivyo. Hasha! Uumbwaji wa ulimwengu ni wa uendelevu; Yeye Mola anaumba chochote kile atakacho katika wakati wowote ule atakao, na uumbaji wake Yeye Allah hauna kikomo, kwa sababu nguvu na uwezo wake ni wa kudumu, daima dawamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu ameufanya mfumo wa ulimwengu wa maumbile ufanye kazi kwa kuwepo sababu na visababishi. Japokuwa Yeye Allah ni Muweza Mutlaki wa kufanya kila kitu, lakini amepanga tadbiri na uendeshaji wa masuala ya ulimwengu ufanywe na Malaika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mkono wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji uko wazi muda wote; hivyo ulimwengu umo kwenye hali ya kupanuka na kustawi. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kazi na majukumu ya Malaika yanatafautiana. Majukumu yao yanajumuisha upande wa umaanawi na wa sharia za dini na pia upande wa masuala ya uendeshaji ulimwengu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya pili ambayo inasema:
مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hapana wa kuizuia. Na anayo izuia hapana wa kuiachia isipo kuwa Yeye. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Baada ya aya iliyotangulia kuzungumzia uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, aya hii inaashiria rehema zake Mola zisizo na ukomo; rehma ambazo ndio msingi na asili ya uumbaji na ambazo baada ya uumbaji pia kila kiumbe kinazihitajia. Uhai na riziki ambavyo ni vitu vya lazima kwa ajili ya kuendelea kuishi kila kiumbe zinatolewa kwa msingi wa rehema za Allah, na hakuna mtu yeyote awezaye kuzizuia. Kama ambavyo ikiwa Yeye Mola ataziondoa rehema zake kwa mja, hakuna yeyote awezaye kuzirejesha na kuzifidia. Bila ya shaka maana ya neno rehema haikomei kwenye huruma na upendo tu ambayo ni hali ya kihisia lakini inajumuisha atiya na neema zote za Mola kwa mja wake. Chochote kile apatacho mwandamu ni rehma ya Mwenyezi Mungu, kiwe ni cha kimaada au cha kimaanawi, cha upande wa vitu vya uumbwaji au kinachohusu hukumu na sharia za Allah! Sehemu ya mwisho ya aya hii inatilia mkazo sifa mbili za Mwenyezi Mungu; moja ni nguvu na uwezo mutlaki wa Mola na usioshindika; na nyengine ni hekima yake isiyo na kikomo; kwa sababu mambo yote anayofanya Allah yanatokana na nguvu na uwezo wake mutlaki na kwa msingi wa hekima na maslaha. Popote pale Mwenyezi Mungu anapoona inahitajika, huumba na kutoa kwa uwezo wake; na asipoona haja ya kufanywa hivyo, hata kama dunia nzima itaungana pamoja haitoweza kufanya chochote dhidi ya irada yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba rehema za Allah zinatangulia ghadhabu zake. Asili ya kuamiliana kwake na waja wake ni kwa rehema, isipokuwa kama mja ataifunga kwa mkono wake mwenyewe njia ya kupatia rehema za Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa nguvu na irada ya Mwenyezi Mungu imefungamana na hekima yake. Ikiwa tunaona Allah hachukui hatua au hafanyi jambo fulani, si kwa sababu ya kutokuwa na uwezo nalo ila ni kutokana na kuona kwa hekima yake kuwa si maslaha kufanya jambo hilo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 774 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aturehemu kwa rehema zake wala asiamiliane nasi kwa uadilifu wake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.