Sura ya Faat'ir, aya ya 3-6 (Darsa ya 775)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.
Hii ni darsa ya 775 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 3 na ya 4 ambazo zinasema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ
Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwengine asiye kuwa Mwenyezi Mungu anaye kupeni riziki kutoka mbinguni na ardhini? Hapana mungu ila Yeye tu. Basi wapi mnako geuzwa?
وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ ۚ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ
Na kama wakikukadhibisha, basi walikwisha kadhibishwa Mitume kabla yako. Na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu.
Katika aya tulizosoma kwenye darsa iliyopita uliashiriwa ukwasi na ueneaji wa rehma za Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Aya hizi tulizosoma zinaashiria upekee wa Allah katika uumbaji na utoaji riziki na kueleza kwamba: neema zote za kimaada na zisizo za kimaada zinazokuteremkieni kutoka mbinguni na ardhini zinatoka kwa Mwenyezi Mungu aliye mmoja tu. Yeye Mungu aliyekuumbeni ndiye anayekuruzukuni; si kwamba uumbaji ni wake Yeye Allah lakini utoaji riziki uko kwa mungu mwengine au kingine chochote kile ambacho ni kiumbe kama nyinyi. Ghairi yake Yeye Allah hakuna muumba wala mtoaji riziki mwengine, kwa hivyo ikiwa matumaini yenu ya kupata chochote kile yatakuwa kwa yeyote yule asiyekuwa Yeye mjue kuwa mko kwenye upotofu. Kisha aya zinaendelea kwa kumliwaza Bwana Mtume Muhammad SAW na Waislamu kwa kuwaambia, ikiwa makafiri na washirikina wanayakadhibisha mafundisho ya Uislamu na hawako tayari kuikubali haki msiingiwe na shaka juu ya njia ya haki mnayofuata, bali kuweni imara na thabiti na jueni kwamba mwisho wa mambo yote unarejea kwa Mwenyezi Mungu. Atawaadhibu wao kwa ukafiri na ukanushaji wao kama ambavyo atakupeni nyinyi pia jaza na malipo mema kwa uthabiti na istiqama yenu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuzingatia neema za Mwenyezi Mungu ni njia ya kutuwezesha kumjua Yeye Mola na kujiweka mbali na kufru na shirki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa japokuwa Yeye Allah ndiye Ar-Razzaq, yaani mwenye kuruzuku lakini anawapatia waja wake riziki hizo kupitia sababu za kimaumbile alizoumba Yeye mwenyewe. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutalii yaliyowasibu waliotutangulia kutatufanya tuwe thabiti na imara katika kushikamana na njia ya haki na kutohofu makeke na nguvu za kidhahiri za batili. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kuzingatia na kukumbuka maadi na kufufuliwa kunamfanya mtu awe imara na thabiti kukabiliana na maadui wa dini na vilevile kuvumilia misukosuko na matukio machungu na mazito.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 5 ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ ۖ فَلَا تَغُرَّنَّكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا ۖ وَلَا يَغُرَّنَّكُم بِاللَّـهِ الْغَرُورُ
Enyi watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Mwenyezi Mungu.
Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia upekee wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji na utoaji riziki na pia maudhi ya Utume, aya hii ya tano inaashiria ahadi za Allah kuhusiana na Kiyama na kueleza kwamba: yale yaliyoahidiwa kuhusu kuhesabiwa amali za waja katika mahakama ya Siku ya Kiyama na wema kulipwa Pepo na wabaya kulipwa Moto, yote hayo ni haki, hakika na kweli. Kwa hivyo jihadharini raha, starehe na mapambo ya dunia yasije yakakughafilisheni akhera na wala ahadi za hadaa anazokupeni shetani kwamba Mwenyezi Mungu ni mrehemevu na mwenye kughufuria madhambi, zisije zikakushajiisheni kufanya madhambi na maovu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba miongoni mwa mbinu na hila za shetani za kumshajiisha mtu kufanya madhambi ni kumpa matumaini ya kupata maghufira na msamaha wa Allah ilhali sharti la kupata msamaha wa Mola ni kutubia na kujutia mtu dhambi aliyofanya sio kushupalia na kuwa na raghaba ya kufanya madhambi mengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa ikiwa shetani anawahadaa makafiri kwa mapambo, starehe na raha za dunia, huwaghilibu pia baadhi ya waumini na kuwafanyisha madhambi kwa kuwapa matumaini ya kupata maghufira na msamaha wa Allah.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 6 ambayo inasema:
إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ
Hakika Shet'ani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa Motoni.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kwa kuwatahadharisha watu wote na hasa waumini kwamba tangu mwanzo wa kuumbwa kwenu Shetani alikufanyieni uadui na hakuwa tayari kusujudu kwa ajili yenu. Kwa kuwa yeye alitolewa na kuwekwa mbali na rehma za Allah kutokana na kuasi kwake huko, ameapa kwamba atafanya kila awezalo ili kuwapotosha wanadamu. Kwa hivyo na nyinyi mfanyeni yeye pia adui na wala msikubali kuhadaiwa na kutekwa na wasiwasi wake anaokutieni. Kisha aya inaendelea kwa kueleza kwamba: si kama shetani ana nguvu juu yenu na uwezo wa kukulazimisheni mfanye madhambi; la hasha; ushawishi wake unafanya kazi kwa watu ambao wao wenyewe wametaka kumfuata yeye na kuwemo kwenye kundi la wafuasi wake. Ni wazi kwamba hatima ya watu wa aina hiyo ni adhabu ya Moto na kuwa pamoja na shetani kwenye makaazi ya Moto wa Jahannam. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba tusifikirie maadui wa mali, roho na heshima ya watu wetu na ardhi yetu tu, japokuwa yote hayo ni muhimu, lakini inapasa tumfikirie pia adui wa imani na akhlaqi zetu. Kwa sababu kama tutaghafilika kidogo tu shetani atatutumbukiza kwenye shimo la madhambi na upotofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa ikiwa tutatoka kwenye Hizbullah kwa maana ya Kundi la Mwenyezi Mungu ambalo katika maana yake pana linajumuisha waumini wote wa kweli, tutaangukia kwenye kundi la shetani na kunasa kwenye mtego ambao itakuwa vigumu kujitoa na kujinasua na hatima yetu itakuwa ni kuishia kwenye adhabu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 775 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na hila na ghilba za shetani na kumfanya adui yetu kama yeye alivyo adui kwetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.