Mar 25, 2018 07:21 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 776 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 7 ambayo inasema:

الَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ

Wale waliokufuru watakuwa katika adhabu kali; na wale walioamini watapata maghufira na malipo makubwa.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyozungumzia uadui wa shetani kwa mwanadamu na hatari ya mtu kuingia motoni kwa sababu ya kujiingiza kwenye kundi la shetani. Katika muendelezo wa maudhui hiyo, aya tuliyosoma inasema: kukufuru na kuikana haki kunamfungulia njia shetani ya kumghilibu na kumdhibiti mwanadamu na kumfanya mwishowe awe na hatima mbaya. Lakini kama mtu atakuwa muumini na mtenda mema, hata kama atapatwa na wasiwasi wa shetani utakaomfanya ateleze na kufanya kosa, Allah humsamehe dhambi yake na kumrehemu kwa rehma na fadhila zake. Ni wazi kwamba imani ya batini na moyoni tu bila amali na matendo haitoshi wala haimletei mtu jaza na malipo mema. Lakini kukufuru tu peke yake kunatosha kumtenga mtu na kumweka mbali na Pepo. Kwa sababu wakati mtu anapochagua njia isiyo sahihi ya kupita hatoweza katu kufika anakokusudia kwenda hata kama atakuwa ametumia kipando bora kabisa cha kusafiria. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kutafakari kuhusu matokeo na hatima ya lolote analofanya mtu kuna taathira katika malezi na saada yake, kwa sababu maisha ya mwanadamu hayamalizikii kwenye kifo; na mtu mwenye akili huwa anaangalia mbali na kufikiria mustakabali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa bila mtu kusamehewa kwanza dhambi zake hawezi kufungukiwa na njia ya kuingizwa peponi na kulipwa jaza na malipo mema. Mtu hawezi kuingia peponi huku mabegani mwake amebeba mzigo wa madhambi, kwa sababu peponi si mahali pa watu wachafu na waovu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 8 ambayo inasema:

أَفَمَن زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا ۖ فَإِنَّ اللَّـهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ ۖ فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ

Je, yule aliyepambiwa ubaya wa tendo lake akaliona zuri (ni sawa na anayeliona jambo kama lilivyo?); basi hakika Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humwongoa amtakaye. Basi roho yako isitoke kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia iliyozungumzia mwisho na hatima za makundi mawili ya waumini na makafiri na kueleza kwamba: hulka ya kukufuru na kuikana haki humfikisha pahala mtu yale maovu anayoyafanya akayaona mazuri na kunyimwa uwezo wa kuyadiriki mambo vile yalivyo katika uhalisia wake. Zaidi ya hayo, huwa hata hafikirii kujirekebisha na wala hakubali kusikiliza mawaidha au nasaha zozote zile. Kwa kuwa makafiri hawamkubali Mwenyezi Mungu huwa wanakipima kila kitu kwa kutumia mizani ya nafsi zao; na ni kawaida kwamba ili kuzifikia raha na starehe za kupita, nafsi humpambia mtu baadhi ya mambo maovu na machafu ili ayaone mazuri. Lakini waumini, wao wanayapima mambo na matendo yao kwa kuzingatia maamrisho ya Mwenyezi Mungu; na pale yanapokinzana nayo huziweka pembeni hawaa na matashi yao na si kutekwa na yale wanayopambiwa na nafsi zao. Ni wazi kuwa kufru na kufuata matamanio ya nafsi humkosesha mwanadamu neema ya kuukubali uongofu wa Allah na kumuelekeza kwenye dhalala na upotofu. Lakini imani juu ya Allah humwandalia mtu mazingira ya kupokea uongofu wa Mola na kumuelekeza kwenye njia iliyonyooka. Kisha sehemu ya mwisho ya aya inamuusia Bwana Mtume Muhammad SAW na waumini wasisikitike kupita kiasi na kusononeka roho na nafsi zao kwa sababu ya hali za watu wasio tayari hata kusikiliza maneno ya haki, seuze kuyakubali na kuyaamini. Kwa sababu hesabu ya watu hao iko kwa Mwenyezi Mungu; na Yeye Mola ni mjuzi wa dhahiri na batini ya nafsi zao. Historia imeshuhudia jinsi Bwana Mtume SAW alivyokuwa akiumia sana moyo wake kwa kutaka watu waongoke na kuifuata haki. Qur’ani tukufu imeizungumzia hali hiyo katika sehemu aya ya 128 ya Suratu-Tawbah kwa kusema: “yanamhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni sana, kwa waumini ni mpole mwenye huruma”. Kwa hivyo madhumuni ya aya ya 8 ya sura hii ya Fat’ir ni kuwa si kwamba tusisikitishwe na kuumia kutokana na kupotoka watu; bali makusudio yake ni kuwa kusikitishwa na kuumia huko kusituzuie kuendeleza harakati wala kusituvunje moyo na kutukatisha tamaa na kudhani kwamba tablighi na ulinganiaji wetu hauna athari yoyote. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba moja ya hatari za nafsi ni kumpambia mtu mabaya na maovu akayaona mazuri na kumpa hoja za kuhalalisha utendaji wa maovu hayo. Kwa maneno mengine ni kwamba, mwanadamu kwanza hutafuta njia ya kujiridhisha na kuihalalisha dhambi kisha ndipo akaifanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mazuri na mabaya tuyapime kwa kutumia mizani madhubuti ya akili na wahyi si matakwa na matamanio ya nafsi zetu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Mwenyezi Mungu ameifanya dhambi kuwa sababu ya kupotoka mtu; na upotokaji huo unatokana na utendaji wa mtu mwenyewe. Makafiri wanafuata njia ya upotofu kutokana na inadi na ukaidi na matokeo yake ni kuwafanya wapotoke zaidi. Vilevile aya hii inatufunza kuwa ni sawa mtu kuungulika na kusikitishwa na hali ya upotofu wa watu. Lakini kusikitishwa na kuungulika huko inapasa kuwe na kiwango na mpaka. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 776 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata, na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.