Mar 25, 2018 07:30 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 777 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 35 ya Fat'ir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 9 ambayo inasema:

وَاللَّـهُ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ فَتُثِيرُ سَحَابًا فَسُقْنَاهُ إِلَىٰ بَلَدٍ مَّيِّتٍ فَأَحْيَيْنَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا ۚ كَذَٰلِكَ النُّشُورُ

Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma Pepo ziyatimue mawingu, nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyo kufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Ndivyo kama hivyo kutakavyo kuwa kufufuliwa.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoashiria hali za waumini na makafiri Siku ya Kiyama. Aya hii inatoa jibu kwa watu wenye shaka ya kufufuliwa viumbe na kudhani hilo ni jambo lisilowezekana kwa kuwaeleza kwamba: hapa duniani pia katika msimu wa baridi, Mwenyezi Mungu SW huifisha miti kwa kuifanya mikavu na kuifufua tena kwa kuinawirisha wakati wa msimu wa machipuo. Kufufuliwa kwenu nyinyi wanadamu, nako pia kutakuwa vivyo hivyo. Hivi mnadhani Mungu anayeutumia upepo na mvua kuirutubisha ardhi kavu na yabisi na kuifanya iwe hai tena na kuwezesha kuota tena miti na mimea juu yake, si muweza wa kukufufueni nyinyi tena na kukutoeni kutoka kwenye ardhi baada ya kufa? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuvuma kwa upepo unaosukuma mawingu yaliyotuama juu ya anga ya bahari na kuyapeleka hadi kwenye ardhi kavu na yabisi; na kunyesha mvua inayoirutubisha na kuipa uhai mpya ardhi hiyo iliyokufa na vitu vingine vya maumbile si mambo yanayotokea kwa sadfa na bahati tu, bali yote hayo yanafanyika kwa irada ya Allah SW, Mola Muumba wa ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mfumo wa ulimwengu wa maumbile unafanya kazi kwa kufuata ratiba, nidhamu na utaratibu maalumu na unaendeshwa na Mwenyezi Mungu kupitia malaika ambao ni watendaji wake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 10 ambayo inasema:

 مَن كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ۚ إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ وَالَّذِينَ يَمْكُرُونَ السَّيِّئَاتِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَمَكْرُ أُولَـٰئِكَ هُوَ يَبُورُ

Mwenye kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye hupanda neno zuri, na a'mali njema Yeye huitukuza. Na wanao panga vitimbi vya maovu watapata adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaondokea patupu. 

Watu wapenda dunia huwa wanadhani kwamba izza na utukufu unapatikana kwa kuwa na madaraka na utajiri au kwa kujikumbatisha kwa wenye mamlaka ya utawala; hivyo hufanya bidii na kutumia nguvu zao zote ili kuipata izza kwa njia hiyo. Lakini Qur'ani tukufu inasema: izza na utukufu wa kweli unapatikana kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, kumwamini Yeye Mola na kuwa mja wake halisi. Kwa sababu maana ya izza ni kutodunishika na kutodhalilishika; na sifa hizo hawezi kupambika nazo mtu isipokuwa kwa kushikamana na chanzo na asili ya uumbaji na Muweza mutlaqi, ambaye ni Yeye Allah SW. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba njia ya kuifikia izza na utukufu ni kuwa na imani sahihi na kufanya amali njema na stahiki na kuongeza kwamba: kinachopanda juu kuelekea kwa Allah na kumuinua mtu kwa daraja ni imani na amali njema, si ghairi ya hivyo. Bila ya shaka kuna baadhi ya watu wanaodhani kwamba wanaweza kuipata izza na utukufu kwa hila, ujanja na hadaa, ilhali hata kama wataweza kuyapata matakwa yao yasiyostahiki kwa kipindi kifupi tu mwishowe wataharibikiwa katika hila na hadaa zao na kuwafanya wadhalilike na kufedheheka. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba izza na utukufu wa kweli unapatikana kwa Mwenyezi Mungu si kwa binadamu! Kuna watu wangapi na wangapi ambao leo wanaonekana mbele za watu watukufu na wenye izza lakini kesho yake wanakuwa duni na dhalili. Lakini mtu muumini hata anapokuwa kwenye dhiki na matatizo makubwa kabisa anabaki kuwa na izza na utukufu! Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, imani na amali ni vitu vyenye uhusiano wa pande mbili na vyenye kuathiriana. Kila kimoja kinamtia nguvu au kumdhoofisha mwenzake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kuipata izza na utukufu wa kudumu kwa hila na hadaa.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 11 ambayo inasema:

 وَاللَّـهُ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ جَعَلَكُمْ أَزْوَاجًا ۚ وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ ۚ وَمَا يُعَمَّرُ مِن مُّعَمَّرٍ وَلَا يُنقَصُ مِنْ عُمُرِهِ إِلَّا فِي كِتَابٍ ۚإِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ 

Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kisha kwa tone la manii. Kisha akakufanyeni mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote hachukui mimba, wala hazai, ila kwa ilimu yake. Na wala hapewi umri mwenye umri mrefu, wala hapunguziwi katika umri wake, ila yamo hayo katika Kitabu. Hakika hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu.

Wakanushaji wa Maadi yaani kufufuliwa viumbe hawana hoja yoyote ya kielimu ya kuthibitishia ukanushaji wao isipokuwa kila mara huibua masuali haya na yale ili kutilia shaka tu uwezekano wa kujiri kwake. Kutokana na hayo aya tuliyosoma inasema: ikiwa mna shaka na uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kuumba tena, inawezekanaje Yeye Mola awe na uwezo wa kukuumbeni nyinyi mara ya kwanza kwa udongo, lakini ashindwe kufanya hivyo tena mara ya pili Siku ya Kiyama? Yeye ambaye amezipanga awamu zote za kuumbwa kwenu kuanzia kutunga mimba kwa tone la manii, kipindi cha kulelewa kwake hadi kuzaliwa kwenu akiwa na uelewa nazo kamili, atashindwa kweli na kupoteza uwezo wa kufanya hivyo Siku ya Kiyama? Na hata baada ya kuzaliwa pia muda wa kuishi kwenu duniani, uwe mfupi au mrefu hautoki nje ya mipaka ya mamlaka ya Allah SW na kila kitu chake kinarekodiwa na kuhifadhiwa katika elimu yake mutlaki Yeye Mola. Baada ya yote hayo mngali mnadhani kwamba kukuumbeni tena ni jambo gumu kwake?! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kutafakari juu ya asili ya kuumbwa mwanadamu humfanya mtu aelewe adhama ya uwezo wa Mwenyezi Mungu na kutopatwa na mghafala au kuingiwa na ghururi na takaburi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa wanadamu wote, iwe ni baba yetu Adam au sisi tuliopo hivi sasa, tumetokana na udongo na tutarejea kwenye udongo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba umri wa mwanadamu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu; na kwa elimu yake Yeye Mola umri wa baadhi ya watu unakuwa mfupi na wa baadhi ya wengine unakuwa mrefu. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kwamba kila saa, dakika na sekunde ya maisha ya mwanadamu inarekodiwa na kuhifadhiwa kwenye daftari maalumu; na Siku ya Kiyama itakuwa ni hati ya ushahidi wenye kumletea faida au hasara kwake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 777 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atusamehe madhambi yetu, atakabalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.