Apr 19, 2018 03:05 UTC
  • Alkhamisi tarehe 19 Aprili, 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Shaaban 1439 Hijria sawa na Aprili 19 mwaka 2018.

Miaka 2051 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nadharia za wanahistoria, yaani tarehe 19 Aprili mwaka 33 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (as), kulianzishwa mjini Roma maktaba ya kijamii 'Public Library' kwa ajili ya ulimwengu mzima ambayo kila mwenye elimu alikuwa na haki ya kuingia humo na kusoma vitabu alivyotaka. Kabla ya Waroma, Wasumeri, Waashuri, Wababeli na Wairani walikuwa na maktaba zao ingawa maktaba hizo hazikuwa zikitumika na watu wote, huku maktaba ya Waashuri ikiwa ndio maarufu zaidi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, nchi ya kwanza ambayo ilianzisha asasi za uandishi na tarjama za vitabu duniani, ilikuwa ni Iran, ambapo karne 15 zilizopita zilikuwa zikifanya kazi hizo katika utawala wa Khosrow Anushirvan.

Maktaba ya umma

Siku kama ya leo miaka 1043 iliyopita alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria, Khaja Abdullah Ansari katika mji wa Herat nchini Afganistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi na nudhumu, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mahabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Khaja Abdullah Ansari

Siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, sawa na tarehe 19 Aprili 1807, majeshi ya Uingereza yalilazimika kuondoka katika mji wa bandari ya Alexandria nchini Misri, baada ya kushindwa kukabiliana na jeshi la Misri. Ikiwa ni katika njama za kutanua wigo wake wa utawala wa kikoloni, Uingereza ilichukua uamuzi wa kuishambulia na kuiteka Misri ambayo ilikuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmaniya. Baada ya kuanza mashambulizi hayo na mji wa Alexandria kutekwa na Uingereza, maulamaa na wanazuoni wa nchi hiyo walitoa fatwa ya kuanzishwa vita vitakatifu dhidi ya wavamizi, kwa shabaha ya kuikomboa Misri kutoka kwa wavamizi wa Kiingereza.

Alexandria

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza Charles Darwin. Msomi huyo alifanya utafiti kuhusu manma ya kutokea viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu duniani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kielimu na baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species". Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa. Fikra za Darwin zinapingana na mafundisho ya dini za mbinguni kuhusu namna ya kuumbwa mwanadamu lakini zimetumiwa kama msingi wa mifumo ya kilahidi kama ule wa Umaxi.

Charles Darwin

Tarehe 19 Aprili miaka 25 iliyopita, polisi ya Marekani FBI ilishambulia makao ya wafuasi wa kundi la David na kuua watu 80 miongoni mwao. Wafuasi wa kundi hilo ambao wanapinga vikali siasa za serikali ya Marekani walishambuliwa na kuuawa na askari wa FBI baada ya kuzingirwa katika makao yao kwa siku kadhaa. Mauaji ya wapinzani wa serikali katika nchi kama Marekani inayodai kutetea uhuru wa kusema na kuabudu na haki za binadamu yaliwashangaza watu wengi duniani na kuifedhehesha serikali ya Washington.

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, Kadinali Joseph Ratzinger alikabidhiwa uongozi wa Kanisa Katoliki Duniani baada ya kufariki dunia Papa John Paul wa Pili na kuchagua jina la Papa Benedict wa 16. Ratzinger alizaliwa mwaka 1927 nchini Ujerumani na alipanda daraja na kuwa askofu mwaka 1977 na hatimaye kufikia daraja ya ukadinali. Papa Benedict wa 16 alikabiliwa na matatizo mbalimbali akiwa kiongozi wa kanisa hilo ikiwa ni pamoja na mgogoro wa masuala ya kiroho katika nchi za Magharibi, ufisadi na utovu wa maadili pamoja na vitendo vya ubakaji vinavyofanywa na maaskofu na makasisi dhidi ya watoto wadogo. Papa Benedict wa 16 alilazimika kuachia uongozi wa Kanisa Katoliki Februari mwaka 2013 baada ya kuzongwa na kashfa nyingi za viongozi wa ngazi za juu ndani ya kanisa hilo.

Kadinali Joseph Ratzinger

 

Tags