Apr 29, 2018 03:02 UTC
  • Jumapili, 29 Aprili, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 12 Sha'aban 1439 Hijria, sawa na tarehe 29 Aprili, 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 941 iliyopita aliaga dunia Hassan bin Hafiz Ghassani Andalusi, mpokeaji hadithi na tabibu mashuhuri wa Andalusia, sehemu ya Uhispania ya leo. Ghassani alikuwa mwanafasihi mahiri na tabibu mweledi. Aidha alikuwa na hati za kuvutia sana na mwenye kipaji kikubwa cha kutunga mashairi. Kitabu cha 'Tamjiidul-Muhmal' ni moja ya athari za thamani za Hassan bin Hafiz Ghassani na ambacho kinazungumzia na kufafanua maisha ya wapokezi wa hadithi.

Hassan bin Hafiz Ghassani Andalusi

Siku kama hii ya leo miaka 336 iliyopita Peter the Great alichukua madaraka ya nchi huko Russia akiwa na umri wa miaka 10. Peter alikuwa ndugu wa Feodor katika kizazi cha tatu cha Tzar katika ukoo wa Romanov. Baada ya kuchukua madaraka Peter alivuliwa uongozi na dada yake na kubaidishwa katika kijiji kimoja karibu na mji wa Moscow. Baada ya muda Peter aliandaa jeshi kubwa na kwenda kupambana na dada yake. Katika vita hivyo Peter alishinda na kutawala nchi hiyo kwa mara nyingine. Kadhalika Peter alifanya marekebisho makubwa ndani ya Russia. Peter the Great alifariki dunia mwaka 1725.

Peter the Great

Siku kama ya leo miaka 271 iliyopita, jeshi la Ufaransa lililokuwa na wapiganaji wapatao elfu 90, lilianzisha mashambulizi dhidi ya nchi ya Uholanzi. Jeshi hilo ambalo lilikuwa limejizatiti kikamilifu, lilifanikiwa kuvuka kwa haraka mto wa Esco licha ya kuwepo vizingiti vingi na kuingia Uholanzi.

Askari wa Ufaransa

Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, alizaliwa Henri Poincaré, mtaalamu wa sayansi na hisabati wa Ufaransa katika mji wa Nancy nchini humo. Poincare alikuwa mahiri katika somo la hisabati na alianza kufanya utafiti katika uwanja huo. Chunguzi mbalimbali zilizofanywa na mwanahisabati huyo wa Kifaransa kuhusiana na masuala ya uchanganuzi wa kimahesabu, mwangaza, umeme n.k zimetajwa kuwa muhimu na sahihi.

Henri Poincaré

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita sawa na tarehe 29 mwezi Aprili mwaka 1928 Miladia, nchini Uturuki herufi za Kilatini zilitambuliwa rasmi na kuchukua nafasi ya zile za Kiarabu. Hatua hiyo ilichukuliwa katika njama za kuipiga vita dini ya Kiislamu na badala yake kuingizwa tamaduni za Kimagharibi katika jamii ya wananchi Waislamu wa Uturuki. Mchakato huo ulianzishwa na Mustafa Kamal maarufu kama Ataturk kuanzia mwaka 1923. Mfumo wa Jamhuri ulishika hatamu za uongozi huko Uturuki chini ya Ataturk kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1923 baada ya kuanguka kwa utawala wa Othmania uliodumu kwa miaka 623 nchini humo. 

Mustafa Kamal maarufu kama Ataturk

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita majeshi ya waitifaki yalipata pigo kubwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Vikosi vya nchi waitifaki wa Ulaya vilifanya shambulizi la pamoja dhidi ya Italia baada ya kusambaratishwa safu ya ulinzi ya Ujerumani. Italia ilikuwa muitifaki wa Ujerumani chini ya uongozi wa Musolini.

Hitler akiwa amekata tamaa kushinda kwenye vita

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, alifariki dunia Ludwig Wittgenstein, mwanafalsafa mashuhuri wa Austria. Alizaliwa mwaka 1889 Miladia mjini Vienna, mji mkuu wa nchi hiyo na baada ya kuhitimu masomo ya msingi aliendelea na masomo nchini Uingereza katika fani ya uhandisi. Kukutana kwake na Bertrand Russell, mwanafalsafa mkubwa wa Uingereza kulimvutia sana Ludwig Wittgenstein na kumfanya ajiunge na fani hiyo. Baada ya kusoma kitabu cha Russell alidai kwamba masuala yote ya falsafa yametatuliwa, hata hivyo baada ya miaka kadhaa alitambua kosa lake na mwaka 1929 alifikia daraja ya PHD katika falsafa na kufanikiwa kuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Cambridge. Ameacha athari kadhaa katika fani hiyo na moja ya athari hizo ni kitabu cha 'Tafiti za Kifalsafa'.

Ludwig Wittgenstein,

Tags