May 14, 2018 03:03 UTC
  • Jumatatu, Mei 14, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Shaaban 1439 Hijria mwafaka na tarehe 14 Mei 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 613 iliyopita kkulingana na kalenda ya Hijria, Ibn Araqi fakihi na kadhi wa Kiislamu wa Misri aliaga dunia katika mji wa Makka. Alizaliwa mwaka 762 na alihudhuria darsa na masomo ya wanazuoni mashuhuri wa zama hizo katika elimu ya hadithi. Ibn Araqi baada ya kunufaika na elimu ya walimu wa zama hizo alifanikiwa kuingia katika faharasa ya maulama mashuhuri na kuanza kufundisha elimu za fikihi na hadithi.  Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu.***

Ibn Araqi

 

Miaka 443 iliyopita katika siku kama ya leo, ardhi ya Angola ilikaliwa kwa mabavu na mkoloni Mreno. Kabla ya Wareno kuwasili Angola, ardhi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Kiafrika wa Guinea. Baada ya Wareno kuidhibiti nchi hiyo walianzisha vituo vya biashara katika maeneo yake yote ya pwani. Baada ya kumalizika vita vya Pili vya Dunia, harakati kadhaa zilianzishwa nchini Angola kwa lengo la kuipatia uhuru nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1975 harakati za wapigania uhuru zilizaa matunda baada ya nchi yao kupata uhuru. ***

Ardhi ya Angola

 

Katika siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, kwa mara ya kwanza ilifanyiwa majaribio nchini Uingereza chanjo ya ugonjwa wa Ndui. Hata kama hii leo hususan katika nchi zilizoendelea kuna kiwango kidogo cha athari inayotokana na ugonjwa huo, lakini hadi kufikia karne ya 18, maradhi hayo yalienea sana ndani ya mataifa hayo na kusababisha madhara makubwa. Mwaka 1717 mwanamke mmoja wa Uingereza alianzisha utafiti na uchunguzi mkubwa katika suala hilo, hasa baada ya kugundua kuwa eneo la mashariki mwa Ulaya kulikuwepo na mada za sumu zinazoweza kuzuia maradhi hayo, na kufanikiwa kueneza mbinu hiyo chanjo nchini Uingereza ambapo ilipunguza sana idadi ya waathiriwa. Hatimaye tarehe 14 Mei mwaka 1796 Miladia, Dakta Edward Jenner aliifanyia majaribio chanjo ya ndui kupitia mwili wa mtoto mdogo na kutoa majibu mazuri.***

Athari ya ugonjwa wa ndui

 

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, nchi ya Paraguay ilijipata uhuru wake. Paraguay iligunduliwa katika karne ya 16 Miladia na Muhispania mmoja na ikawa chini ya utawala wa Uhispania kwa zaidi ya karne mbili. Baada ya uhuru nchi hiyo ilitawaliwa na serikali ya kidikteta na kulishudiwa majaribio kadhaa ya mapinduzi na kila aliyeingia madarakani aliongoza kidikteta. Uchaguzi wa kwanza huru wa rais ulifanyika nchini humo mwaka 1989. Kijiografia Jamhuri ya Paraguay inapatikana huko Amerika Kusini baina ya nchi za Brazil, Argentina na Bolivia. ***

Bendera yay Paraguay

 

Miaka 151 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 74, Joseph Reinaud, msomi na mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufarasa. Kutokana na kupendelea sana lugha za eneo la Mashariki ya Kati, alianza kujifunza lugha na fasihi ya Kiarabu. Baada ya muda mfupi, Joseph Reinaud alianza kufundisha lugha hiyo katika chuo kikuu nchini Ufaransa. Aliandika vitabu kuhusiana na historia ya Uislamu ambapo moja ya vitabu hivyo ni 'Fat'hul-Arab' na 'Al-Islamu wal-Muslimin.'***

Joseph Reinaud

 

Katikka siku kama yya leo miakka 127 iliyopita, Ayatullah Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mar'ja' mashuhuri wa Kiislamu, katika hatua ya kukabiliana na ukoloni wa Uingereza, alitoa fatwa ya kuharamisha utumiaji tumbaku nchini Iran. Katika kipindi cha utawala wa Nassir Deen Shah kutoka ukoo wa Qajaar Uingereza ilikuwa ikiongeza satwa yake nchini Iran kwa kufungua makampuni ya tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini hapa. Fatua hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika fatwa hiyo iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, mkataba wa kisiasa na kijeshi wa Warsaw ulitiwa saini baina ya nchi nane za kikomonisti barani Ulaya. Makubaliano hayo yaliyojulikana kama The Warsaw Pact yalitiwa saini katika mji mkuu wa Poland, Warsaw na lengo lake lilikuwa ni kukabiliana na Mkataba wa Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi (NATO) uliotiwa saini na madola ya magharibi waitifaki wa Marekani. Nchi zilizotia saini makubaliano hayo ziliahidi kutotumia nguvu na mabavu katika ushirikiano wao. Aidha zilikubaliana kwamba, kushambuliwa kijeshi mwanachama mmoja ni sawa na kuchokozwa nchi zote wanachama. Hatimaye baada ya miaka 36, mkataba huo ulifutwa mwaka 1991 baada ya nchi hizo kukutana huko Budapest mji mkuu wa Hungary.***

Warsaw