May 16, 2018 02:43 UTC
  • Jumatano, Mei 16, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 29 Sha'ban 1439 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 16 Mei 2018 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1220 iliyopita, mwaka 219 Hijria Qamari, alifariki dunia faqihi, mtaalamu wa hadithi na mpokezi wa matukio ya kihistoria maarufu kwa jina la Abu Naiim. Alizaliwa mwaka 130 Hijria nchini Iraq na anatambulika kuwa mpokezi aliyetegemewa na kuheshimiwa sana na maulamaa wa Kiislamu wa hadithi. Ameandika kitabu cha As Salaat na mwanahistoria maarufu Ibn Nadim anasema kuwa, msomi huyo ameandika pia vitabu vya "al Manasik" na "Masailul Fiqhi".

@@@@

Siku kama ya leo miaka 1121 iliyopita sawa na 29 Shaaban mwaka 318 Hijria Qamaria alifariki dunia Ibn Mundhir, mtaalamu wa sheria za Kiislamu, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Ibn Mundhir alijifunza elimu ya fiq'hi na hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa zama zake huku akifanya safari pia kuelekea mjini Makkah, ambapo alisikiliza na kujifunza elimu ya hadithi hadi mwisho wa uhai wake. Aidha akiwa mjini Makkah alijishughulisha na uandishi wa vitabu tofauti. Katika kitabu cha 'Al-Ijmaa' alibainisha na kufafanua nadharia tofauti za wasomi katika uwanja wa sheria za Kiislamu.

@@@

Katika siku kama ya leo miaka 514 iliyopita, ardhi ya Honduras inayopatikana leo huko Amerika Kusini iliunganishwa na makoloni ya Muhispania. Kabla ya hapo Honduras ilikuwa kituo cha utamaduni wa kaumu ya Maya. Hata hivyo baada ya Honduras kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uhispania, kabila hilo liliangamizwa na kupotea. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na kutokana na kuvurugika hali ya ndani ya Uhispania, Honduras kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine, ilitumia fursa hiyo kuweza kujipatia uhuru wake. 

 

@@@

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, Jenerali Mobutu Sese Seko rais na dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zaire ya zamani, aliikimbia nchi hiyo baada ya vikosi vya majeshi ya waasi vilivyokuwa vikiongozwa na Laurent Kabila kukaribia mji wa Kinshasa. Mobutu alichukua madaraka ya nchi hiyo mnamo mwaka 1965 kupitia mapinduzi ya kijeshi na kisha kutawala kwa muda wa miaka 32. Licha ya kiongozi huyo kuwa dikteta asiye na huruma, lakini alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani na Ufaransa. Kutokana na Congo DR kuwa katika eneo nyeti na muhimu kijiografia katikati mwa bara la Afrika na kuwa na utajiri mkubwa wa madini ikiwemo almasi, imekuwa ikizingatiwa na kumezewa mate na nchi za Magharibi. Siku moja baada ya Mobutu kuikimbia nchi hiyo, vikosi vya waasi viliuteka mji wa Kinshasa na kiongozi wao yaani Laurent Kabila, akashika hatamu za uongozi wa nchi. 

Na Miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo, Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti lilianza kuondoka nchini Afghanistan. Baada ya Nur Muhammad Taraki kupinduliwa, serikali ya kwanza ya kikomunsti iliyokuwa ikipata himaya ya moja kwa moja ya Urusi ya zamani ilianzishwa nchini Afghanistan. Utawala wa Taraki uliondolewa madarakani mwanzoni mwa mwaka 1979 kupitia mapinduzi mengine yaliyoongozwa na Hafidhullah Amin mmoja wa watu wake wa karibu. Lakini Warusi walikuwa na mtazamo mbaya na Hafidhullah ambaye alikuwa akitaka kujikurubisha kwa Marekani na kuanzisha uhusiano kati ya Afghanistan na Mashariki na vilevile Magharibi na hivyo wakaipindua serikali yake.