Jun 16, 2018 15:51 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 38 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia kwa ufupi mpango wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wa kuwawekea Waislamu sheria kali ambazo kimsingi zinalenga kuwabana ndani ya nchi hiyo ya Ulaya na leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo. Mwezi Mei mwaka jana Rais Macron akizungumza na viongozi wa dini kubwa nchini Ufaransa aliashiria mpango wake wa kufanya mabadiliko katika muundo wa harakati za Kiislamu nchini humo huku akisisitiza kwamba suala hilo haliwezi kuepukika. Katika miaka ya hivi karibuni, Ufaransa imekumbwa na mashambulizi kadhaa ya kigaidi. Hata hivyo aghlabu ya wahusika wa mashambulizi hayo, hata kama wanatoka katika familia za Kiislamu, lakini walizaliwa na kukulia nchini Ufaransa kwenyewe.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mwenye chuki na Uislamu

Aidha kudhihiri kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) nchini Iraq na Syria kulitokana na uungaji mkono wa idara za usalama na upelelezi za Ufaransa, ambazo ziliwaruhusu raia wa nchi hiyo kwenda kujiunga na kundi hilo eneo la Mashariki ya Kati. Hii ni kwa kuwa siasa za serikali ya Ufaransa zilikuwa zimejikita tu katika kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria na si vinginevyo. Katika uwanja huo serikali ya Paris ilikuwa ikipendelea kufikia lengo hilo kupitia baadhi ya Waislamu hata kama watakuwa na uraia wa Ufaransa au nchi nyingine za Ulaya na ambao kiuhalisia hawana uelewa wa mafundisho ya dini ya Uislamu, bali ni wenye majina ya Kiislamu tu. Ni watu ambao baadaye walikuja kufanya jinai na mauaji makubwa kwa jina la Uislamu, katika hali ambayo vitendo vyao hivyo havina uhusiano wowote na dini hiyo inayolingania amani, upendo na uadilifu.

Magaidi wa Daesh (ISIS)

Baadhi ya viongozi wa Ufaransa, waliamini kwamba kwa kutumia njia hiyo wangeweza kujiepusha na shari ya vijana wenye kufurutu ada na wanaotenda jinai na wakati huo huo kuiondoa madarakani serikali ya Syria. Wakati huo huo vyombo vya habari nchini Ufaransa vilianza kueneza propaganda katika ngazi ya kisiasa kwa kuvinasibisha vitendo hivyo vya genge potofu la Daesh (ISIS) na dini tukufu ya Uislamu kwa lengo la kuhalalisha siasa chafu za Ufaransa na baadhi ya nchi za Magharibi katika mataifa ya Iraq na Syria.

*******

Jinai za kutisha za kundi la ukufurishaji la Daesh, ilikuwa ni fursa ya dhahabu iliyowekwa wazi kwa makundi ya mrengo wa kulia na yenye kufurutu ada yanayoendesha kampeni za chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya. Hii ni kusema kuwa, kwa kutumia fursa hiyo makundi hayo yaliweza kueneza chuki dhidi ya Uislamu sambamba na kuitaja dini hiyo kuwa ni tishio kwa jamii ya watu wa Ufaransa. Kadhalika waendesha chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa na mataifa mengine ya Magharibi walihusika kwa kiwango kikubwa katika kueneza jinai za kundi la Daesh (ISIS) kwa lengo tu la kuuchafulia jina Uislamu. Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa maulama na baadhi ya wanasiasa katika nchi nyingi za Waislamu walisimama imara na kusisitiza kuwa jinai hizo hazina uhusiano wowote na mafundisho ya dini ya Uislamu, ndipo propaganda hizo zikapungua nguvu na kudhoofika.

Bendera ya kundi la Kiwahabi (Answar Suna) la Daesh (ISIS)

Hii ni katika hali ambayo akthari ya wahanga wa jinai za kundi hilo la Daesh ni Waislamu tena wa madhehebu tofauti, ambao kutokana na wao kusimama imara kupinga jinai za magaidi hao wanaofuata idolojia ya Uwahabi, walipoteza maisha yao tena kwa namna ya kutisha sana. Kadhalika watu wanaoeneza chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa na katika ngazi pana zaidi za vyombo vya habari ndani ya taifa hilo, huwataja wanachama wa genge la Daesh kwa jina la 'Wapiganaji wa Dola la Kiislamu, au Wapiganaji wa Jihadi' lengo kuu likiwa ni kuzinasibisha jinai zao na mafundisho mema ya Uislamu. Kutokana na propaganda hizo, makundi ya mrengo wa kulia yenye siasa kali na yanayoeneza chuki dhidi ya Uislamu, yameongezeka sana katika chaguzi za miaka miwili iliyopita nchini Ufaransa sambamba na kukubalika miongoni mwa jamii ya Wafaransa, hususan vijana na watu masikini.

********

Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi kinachokujia kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndugu wasikilizaji, hivi sasa siasa za serikali za Ulaya na kupitia uungaji mkono wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja kwa makundi ya ukufurishaji na kigaidi nchini Syria na Iraq, zimefeli vibaya kutokana na muqawama na kusimama imara mataifa hayo ya Waislamu na kadhalika kupitia msaada na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon, Waislamu wa nchini Afghanistan na Pakistan na uungaji mkono wa serikali ya Russia.

Wanamuqawama wa Hizbullah waliowasambaratisha magaidi wa Kiwahabi wa Daesh

Baada ya kushindwa makundi hayo huko Iraq na Syria,  sasa tishio la makundi hayo limegeuka na kuelekea kwa madola wafadhali wake ya Ulaya. Hii ni kusema kuwa, vijana waliosalia hai huku wakiwa na uzoefu mkubwa katika kutenda jinai kutoka mataifa ya Ulaya ikiwemo Ufaransa na ambao idara za usalama na intelijensia zilitoa taa ya kijani kwa kuwaruhusu kwenda Syria na Iraq kwa ajili ya kujiunga na makundi ya kigaidi na ukufurishaji, sasa wamerejea katika nchi hizohizo za Ulayai. Ni katika mazingira hayo ndipo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa,  akajawa na fikra ya kile alichosema kuwa ni mabadiliko dhidi ya asasi za Kiislamu nchini humo na pia kurekebisha mahusiano kati ya Waislamu na raia wengine wa taifa hilo. Hii ni katika hali ambayo kuna dalili nyingi ambazo zinathibitisha kwamba mpango wa rais huyo hauna maslahi kwa taasisi na harakati za Waislamu nchini humo, na hasa ikitiliwa maanani kwamba idadi kubwa ya Waislamu barani Ulaya inapatikana nchini Ufaransa. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, zaidi ya Waislamu milioni sita wanaishi nchini Ufaransa pekee. Aidha Uislamu ni dini ya pili kwa ukubwa baada ya Ukristo nchini humo. Hali ikiwa ni hiyo, Ufaransa ni nchi ya kwanza kabisa kuweka sheria kali dhidi ya Waislamu barani Ulaya.

********

Kwa mara ya kwanza wanafunzi wa kike wa Kiislamu waliovaa hijabu kupigwa marufuku kuingia darasani nchini Ufaransa ilikuwa mwaka 2000, ambapo serikali ilichukua hatua hiyo kwa kisingizio kwamba suala hilo linakiuka sheria ya muundo wa jamii. Katika kipindi cha utawala wa rais Nicolas Sarközy, mashinikizo hayo yalishika kasi zaidi hasa kwa kuzingatia nara za chama cha mrengo wa kitaifa na uliokuwa unaeneza chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu nchini humo. Ukweli ni kwamba, Sarközy katika mwenendo wake wa chuki dhidi ya Uislamu, alikuwa katika ushindani na mrengo wa kitaifa chini ya uongozi wa Jean-Marie Le Pen na kisha binti yake Marine Le Pen dhidi ya dini hiyo ya mbinguni.

Nicolas Sarközy, rais wa zamani wa Ufaransa

Kiasi kwamba,  mrengo wa kitaifa ulimtuhumu Nicolas Sarközy kwa kupotosha malengo na nara ya chama hicho. Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka jana, Marine Le Pen, alikuwa akimtuhumu Emmanuel Macron kwamba ni mtu dhaifu katika kukabiliana na Uislamu. Katika uwanja huo Le Pen alikuwa akisema kuwa, Macron hana ratiba yoyote kwa ajili ya kukabiliana na dini hiyo nchini Ufaransa. Pamoja na kupita miezi tisa tangu achaguliwe kuwa kiongozi wa Ufaransa ameendelea kufuata sheria ya Usekulari na kuwawekea mipaka na vizuizi Waislamu wa nchi hiyo. Kwa kuzingatia kwamba sheria ya Usekulari nchini Ufaransa inakandamiza harakati za mamilioni ya Waislamu nchini humo, hivyo inatazamiwa kwamba serikali ya nchi hiyo itazidisha upelelezi na ufuatiliaji wa maeneo ya Waislamu na kuwawekeza mashinikizo kwa lengo la kuwazuia kuishi katika msingi wa mafundisho ya dini yao ya Kiislamu. Tunaweza kusema kuwa, Macron anakusudia kuwa kama Jacques Chirac, rais wa zamani wa Ufaransa ambaye alijaribu kuugeuza Uislamu kuwa sawa na Usekulari nchini humo.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 38 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./