Jun 16, 2018 16:49 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 41 na ya mwisho ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia ongezeko kubwa la makundi yanayoendesha harakati za chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani tangu alipoingia madarakani Rais Donald Trump wa nchi hiyo. Tulisema kuwa hakuna rais yeyote nchini Marekani aliyewahi kuwa na chuki kubwa dhidi ya Uislamu kama Donald Trump na katika hilo rais huyo amekuwa akiweka wazi chuki yake hiyo. Tangu siku za mwanzoni mwa utawala wake ametoa amri ya kuwazuia raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia ardhi ya Marekani suala ambalo linabainisha wazi kiwango kikubwa cha chuki aliyonayo Trump kwa dini hiyo.

Rais Donald Trump wa Marekan i

Katika uwanja huo, Trump pia anawatuhumu Waislamu kuwa ni magaidi na katika matukio kadhaa ya kigaidi yaliyojiri ndani ya mwaka mmoja uliopita nchini Marekani na Ulaya, amejitahidi sana kuyahusisha matukio hayo na Waislamu. Aidha tunaweza kusema kuwa Trump si tu kwamba ni mwenye chuki kali dhidi ya Uislamu, bali pia ni mbaguzi mkubwa. Sehemu muhimu ya ubaguzi wake inahusiana na kipindi cha uchaguzi wa rais uliopita mwaka 2016, hasa pale alipowaaonyesha watu weupe kuwa ndio watu bora duniani. Suala hilo pia limethibitishwa na raia wa Marekani. Kwa mujibu wa matokeo ya kura ya maoni, nusu ya raia wa nchi hiyo inamtambua rais huyo kuwa mbaguzi mkubwa. Kura hiyo ya maoni iliyofanywa na kituo cha uchunguzi wa masuala ya umma ilionyesha kwamba, asilimia 57 ya watu wazima, inayowajumuisha watu nane kati ya kila watu 10 weusi, robo tatu ya watu wenye asili ya Uhispania na karibu nusu ya wazungu wote wa nchi hiyo wanaamini kwamba Trump ni mtu mbaguzi sana. Mbali na hayo ni kwamba asilimia 57 ya Wamarekani wanaamini kwamba, siasa zinazotekelezwa na rais huyo ni zenye madhara kwa Waislamu. Aidha asilimia 56 ya siasa hizo ni mbaya na zinazowadhuru watu wenye asili ya Uhispania, huku asilimia 57 ya robo tatu ya Wamarekani weusi ikiwa inaamini kwamba, siasa hizo ni haribifu dhidi yao.

*******

Ndugu wasikilizaji hivi karibuni Emily Swanson na Russell Contreras walitoa ripoti katika Shirika la habari la Associated Press kwamba: "Matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaonyesha kwamba, baada ya Trump kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais uliopita, alianza kuigawa kwa ubaguzi jamii ya Marekani.

Dini ya Kiislamu inakabiliwa na chuki na njama chafu za maadui

Hususan baada ya kujiri matukio ya maandamano ya wazungu weupe wanaojiona kuwa watu bora ambapo matamshi ya Trump mwenyewe ya kuzitaja nchi za Afrika kuwa shimo la choo na kadhalika pendekezo lake la kutaka kujengwa ukuta wa kibaguzi kati ya Marekani na Mexico, mambo ambayo yaliibua mpasuko wa kikaumu na kidini ndani ya jamii ya nchi hiyo." Mwisho wa kunukuu. Ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu na mirengo ya kibaguzi halikutokea nchini Marekani pekee katika mwaka mmoja uliopita, bali, ushindi wa vyama vyenye misimamo mikali na ya kibaguzi dhidi ya Uislamu katika kipindi hicho cha mwaka mmoja uliopita, ulienda sambamba na mashambulizi na hujuma za kuwalenga Waislamu na maeneo yao ya kidini. Kwa hakika kama tulivyosema katika vipindi vilivyopita, mwaka 2017 ulikuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa kwa vyama hivyo vya mrengo wa kulia ndani ya mataifa hayo ya Ulaya. Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani, mwaka jana pekee jumla ya mashambulizi 950 ya kibaguzi dhidi ya Uislamu yaliripotiwa. Aidha kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mashambulizi hayo watu 33 walijeruhiwa.

Magaidi wa kundi la Jab'hatu Nusra ambao nao ni Mawahabi wanaotekeleza mradi wa maadui wa Uislamu

Ripoti hiyo iliongeza kwamba, taasisi za serikali nchini Ujerumani zimeripoti kwamba, zaidi ya mashambulizi 60 yaliisababishia hasara misikiti na vituo vya Kiislamu, hujuma ambazo karibu zote zilitekelezwa na makundi ya mrengo wa kulia nchini humo. Baadhi ya jinai zilizosajiliwa za chuki dhidi ya Uislamu akthari yazo zilihusu propaganda pana zinazoenezwa katika mitandao ya kijamii dhidi ya Waislamu, barua za vitisho dhidi ya Waislamu, kushambuliwa wanawake na wasichana wa Kiislamu waliojistiri kwa hijabu, kuwashambulia moja kwa moja wanaume wa Kiislamu, kuharibiwa misikiti na vituo vya Kiislamu na kuandika maneno machafu kwenye kuta za misikiti.

*******

Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Kwa mujibu wa Ayman Matsik, Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani, katika takwimu zilizowasilishwa, jinai zote kuulenga Uislamu na wafuasi wake, hazikurekodiwa na kwamba idadi kamili ya jinai hizo ni zaidi ya ile iliyotangazwa rasmi.

Waislamu nchini Ujerumani

Kuhusiana na suala hilo, Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchi Ujerumani sambamba na kuashiria anga ambayo haijawekwa wazi na isiyofahamika kuhusiana na kadhia hiyo alisisitiza kuwa, polisi na mwendesha mashtaka wa Ujerumani hadi sasa wanaonekana kuwa wasiotilia maanani hali hiyo na ni kwa ajili hiyo ndio maana hawaripoti kesi hizo ipasavyo. Makundi ya mrengo wa kulia na yenye misimamo mikali ya kigaidi nchini Ujerumani yanaitambua hatua ya Waislamu kuingia nchi hiyo kuwa ni hatari kubwa kwa ajili ya utamaduni wa Ujerumani na Ulaya nzima kwa ujumla. Katika uwanja huo, Oula Pelike mtaalamu wa masuala ya ndani nchini Ujerumani kutoka chama cha mrengo wa kushoto anaamini kwamba, chuki dhidi ya Uislamu ndani ya taifa hilo ina mahusiano na kudhihiri kwa kundi jipya la mrengo wa kulia la Alternative for Germany (AfD). Hivi karibuni chama hicho na katika katiba yake kilitangaza kwamba 'Uislamu hauna nafasi yoyote ndani ya Ujerumani.'

Alternative for Germany (AfD) Kundi la kigaidi linalieneza chuki dhidi ya Uislamu

Pelike aliendelea kufafanua kwamba, chama hicho kimekuwa kikichochea sana chuki dhidi ya Uislamu na wafuasi wa dini hiyo nchini humo kwa kusema: "Wale wanaoendesha harakati za chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu sasa wamefunguliwa milango na kuingia bungeni huku wakitumia jukwaa la bunge hilo kwa ajili ya kupandikiza sumu katika jamii dhidi ya Waislamu wanaoishi nchi hiyo." Mwisho wa kunukuu. Ndugu wasikilizaji ni vyema kufahamu kwamba, chuki dhidi ya Uislamu imeratibiwa hadi katika ngazi ya serikali za Ulaya. Katika uwanja huo haifai kufumbiwa macho njama chafu za lobi za Wazayuni wa Marekani na Ulaya katika kuchochea chuki hiyo. Kuhusiana na suala hilo, Arnaud Fandor, mwanasiasa wa Uholanzi ambaye baada ya kutengenezwa filamu ya 'fitina ' ya kuivunjia heshimu dini Tukufu ya Kiislamu aliamua kuweka wazi njama hizo chafu na maelekezo ya lobi ya Wazayuni wa Marekani na Israel katika kumuelekeza kuunda filamu hiyo kwa lengo la kuupaka matoke Uislamu na kuzidisha chuki na ubaguzi dhidi ya wafuasi wa dini hii. Aidha Fandor ambaye ni mbunge wa zamani wa mrengo wa kulia na aliyekuwa na chuki dhidi ya Uislamu alihusika kuandaa filamu hiyo ya 'Fitina' ambayo ndani yake alimshambulia Mtume Muhammad (saw), Qur'an Tukufu na dini ya Uislamu kwa amri na maelekezo kamili ya Wazayuni, kitendo alichokifanya miaka kadhaa iliyopita.


**********

Akizungumza na gazeti la al-Rai la Kuweit huku akijutia hatua yake hiyo katika kuunda filamu hiyo chafu, Arnaud Fandor aliweka wazi mazingira yote yaliyojiri katika kuunda filamu tajwa.

Chuki dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani

Fandor alisema: "Baada ya kuzalisha filamu hiyo nilikuja kufahamu kwamba jamii kubwa ya watu wamekasirika na hatua hiyo kama ambavyo nilizijeruhi nyoyo zao kwa kiasi kikubwa. Kile ambacho ninakifanya hivi sasa ni kujaribu kurekebisha makossa yaliyopita ambayo yalitokana na kuzalishwa kwa filamu hiyo." Kadhalika muandaaji wa filamu hiyo inayoyavunjia heshimu matukufu ya Waislamu alielezea sababu ya yeye kuamua kusilimu kwa kusema: "Suala hilo halikutokea ghafla, bali karibu mwaka mmoja na nusu na baada ya kuunda filamu ya (Fitina) na kupitia utafiti na uchunguzi nilioufanya kuihusu dini ya Uislamu, bado sikuwa na msukumo wa kuwa Mwislamu. Ni wakati huo ndipo lilinijia swali hili kwamba, je, inawezekana vipi Waislamu bilioni moja na nusu duniani kufuata dini hii ambayo inakabiliwa na propaganda nyingi za chuki na ubaguzi dhidi yake?" Anaendelea kusema: "Baada ya kufanya utafiti niligundua kuwa dini ya Uislamu ni dini bora ambayo inaweza kujibu kila swali la muulizaji.

Pande tatu zinazozalisha ugaidi duniani

Na hapo ndipo nilihisi kuwa sasa umewadia wakati wa mimi kuwa Mwislamu na baada ya kisa hicho kizito ndipo nikaanza kuwalingania watu kwenye Tauhidi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu huku nikishikamana na njia hii ya haki ya Mtume Muhammad (saw). Hata hivyo baada ya mimi kuwa Mwislamu, marafiki na jamaa zangu wa karibu walinitenga huku nikipoteza hata kazi yangu." Mwisho wa kunukuu.
Ndugu wasikilizaji sehemu ya 41 na ya mwisho ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

Tags