Jun 16, 2018 16:02 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 39 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia mipango ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuwawekea mashinikizo Waislamu wa nchi hiyo. Leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo. Ukweli ni kwamba hatua zozote mpya za Rais Macron za kuzuia harakati za Waislamu nchini Ufaransa na kuwawekea mipaka kama vile kuzuia vazi la hijabu kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa Kiislamu, zitayachochea mataifa mengine ya Ulaya kufuata mwenendo huo wa serikali ya Paris. Kufuatia matamshi ya rais huyo juu ya azma yake ya kuzifanyia marekebisho asasi za masomo ya Kiislamu nchini humo, Ahmet Orgas, mkuu wa Baraza la Waislamu wa Ufaransa (CFCM) ameonya juu ya nia mbaya iliyo nyuma ya pazia ya Emmanuel Macron kuwalenga Waislamu.

Waislamu nchini Ufaransa wakidhihirisha hisia zao

Kuhusiana na suala hilo, Orgas amesema: "Ufaransa inaongozwa na serikali ya Kisekulari, hivyo wadhifa wa Macron ni kutoa tu miongozi na maelekezo, lakini utekelezaji wa marekebisho ni wadhifa wa Baraza la Kiislamu na si vinginevyo." Mwisho wa kunukuu. Kadhalika Ahmet Orgas, amelaani vikali vita vya vyombo vya habari kuilenga dini ya Kiislamu na Waislamu nchini humo. Kwa hakika ikiwa serikali ya Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya yana wasi wasi kutokana na vijana wa Kiislamu kujiunga na makundi yenye kufurutu ada na wanaofanya jinai na ugaidi, basi kwanza yanatakiwa kuangalia upya uhusiano wao na nchi zinazolea na kuunga mkono makundi ya kigaidi kama vile Saudi Arabia na Imarati. Hii ni kwa kuwa nchi hizo ndio wahusika na wazalishaji wa kifikra za ugaidi na waungaji mkono kisiasa, kifedha na kijeshi kwa magenge hayo hatari na ya ukufurishaji kama vile Daesh (ISIS), Jab'hatu Nusra, Jaishul-Islam, Boko Haram, ash-Shabab na kadhalika. Suala ambalo pia wamelikiri viongozi wengi wa Ufaransa Marekani, Uingereza na Ujerumani, lakini pamoja na hayo bado hawajachukua hatua yoyote katika uwanja huo. Kinyume chake, madola hayo ya Magharibi yameitaja Saudia kuwa muitifaki wao mkubwa wa kistratijia katika eneo la Mashariki ya Kati.

Ash-Shabab, moja ya makundi ya kigaidi ya Kiwahabi yanayochafua Uislamu

Wakati hali ikiwa hivyo serikali ya Ufaransa na waitifaki wake ni wauzaji wakubwa wa silaha na zana za kijeshi kwa Saudia. Ikiwa serikali za Ulaya zina nia ya dhati ya kukata mizizi ya ugaidi na uchupaji mipaka, basi lazima zipambane na chanzo cha wimbi hilo katika jamii ya Waislamu duniani. Hata hivyo irada hiyo haipatikani si kwa Ufaransa wala nchi yoyote ya Magharibi. Bali kinachofanywa na serikali hizo ni kuyaunga mkono makundi hayo ya kigaidi na wazalishaji wake katika kutenda jinai kwa jina la Uislamu ili kuuhalalisha uingiliaji wao katika siasa za eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

**********

Huku hali ikiwa hivyo, nchini Uingereza nako wimbi la chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu limefikia kiasi cha kuwafanya wanasiasa wa nchi hiyo kukiri suala hilo. Katika uwanja huo hivi karibuni Jeremy Corbyn, Kiongozi wa chama cha Leba nchini humo alitembelea moja ya misikiti kaskazini mwa jiji la London ambapo alilaani vikali chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu nchini humo. Kuhusiana na suala hilo Corbyn alisema: "Chuki dhidi ya Uislamu ni moja ya matatizo makubwa katika jamii ya Uingereza ukilinganisha na majanga mengine ya kibaguzi nchini." Aidha aliyataja kuwa mabaya matukio ya kibaguzi nchini humo hususan dhidi ya wanawake wa Kiislamu wanaovalia hijabu kwa kusema: "Dini ya Uislamu ni alama ya amani na kujitolea." Mwisho wa kunukuu.

David Donald Cameron, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza,

Naye kwa upande wake, Sayeeda Hussain Warsi, mmoja wa wajummbe wa baraza la mawaziri la David Donald Cameron, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, hivi karibuni alikosoa vikali mienendo hasi ya vyombo vya habari vya nchi hiyo kutokana na kuionyesha kwa sura mbaya dini ya Uislamu na wafuasi wake. Akizungumza katika bunge la nchi hiyo kuhusiana na jinai zinazosababishwa na chuki na ubaguzi nchini humo Warsi alisema: "Mtazamo hasi dhidi ya Uislamu na wafuasi wake ni jambo lililoshika kasi zaidi katika vyombo vya habari vya Uingereza ikilinganishwa na miaka iliyopita. Ninaweza kutumia masaa kadhaa kuzungumzia wimbi hilo katika vyombo vya habari hususan yale yanayoandikwa na kutangazwa katika vyombo hivyo." Mwisho wa kunukuu.

*********

Kadhalika Sayeeda Hussain Warsi, alizidi kufafanua kwamba, matokeo ya mwenendo huo usiofaa wa vyombo vya habari nchini humo umewafanya Waislamu hususan wasichana na wanawake wanaovaa hijabu, kupatwa na wasi wasi na khofu kubwa katika jamii inayowazunguka. Kwa ajili hiyo alimtaka Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza kukabiliana na hali hiyo sambamba na kuzungumzia nafasi chanya ya Waislamu katika jamii ya nchi hiyo. Chris Frost, mkuu wa jumuiya ya kitaifa ya waandishi wa habari wa magazeti nchini humo pia alithibitisha uwepo wa chuki, ubaguzi na propaganda chafu dhidi ya Waislamu na kulitaja suala hilo kuwa ni tatizo kubwa.

Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza

Frost alisema: "Ni suala la kuudhi kuwaona wahariri wakuu wa magazeti wakiakisi habari hasi zinazowaonyesha Waislamu katika mtazamo mbaya. Moja ya njia nzuri za kuuza nakala za magazeti ni kuwaaminisha wananchi kwamba wanakabiliwa na tishio kubwa. Kwa kuzingatia uwepo wa kundi hatari la Daesh (ISIS) hivyo kuwapachika Waislamu sifa za kundi hilo ni lengo kuu la kuuza kwa wingi nakala zao. Kwa mujibu wa Chris Frost, karibu asilimia 64 ya raia wa Uingereza hupata habari na taarifa kuwahusu Waislamu na dini yao kupitia vyombo vya habari ambavyo hueneza chuki dhidi ya dini hiyo na aghlabu yao hawako tayari kuufahamu Uislamu kupitia vyanzo vingine." Mwisho wa kunukuu.

******

Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi hii ikiwa ni sehemu ya 39.

Kufuatia kuongezeka kwa chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu nchini Uingereza na katika nchi nyingine za Magharibi, harakati za Waislamu kwa ajili ya kuyaarifisha mafundisho mema ya kulingania uadilifu, amani na udugu kati ya watu wa matabaka tofauti, zimeshika kasi zaidi. Katika uwanja huo, tarehe 18 Februari mwaka huu zaidi ya Waislamu 200 walishiriki katika kampeni ya kitaifa iliyopewa jina la 'Tembelea Msikiti Wangu' kwa kuwakaribisha misikitini wafuasi wa dini nyingine. Kutembelea misikiti imekuwa ni ratiba ya kila mwaka ambayo imekuwa ikitekelezwa na Baraza la Waislamu wa Uingereza kwa lengo la kuimarisha mahusiano mema kati ya Waislamu na raia na pia wafuasi wa dini nyingine za nchi hiyo. Katika ratiba hiyo, watu wasio Waislamu huwa wanatembelea misikiti ya miji tofauti kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusiana na dini hiyo ya amani, udugu na uadilifu. Mwaka huu misikiti ambayo imetangaza utayarifu wake wa kushiriki ratiba hiyo, imezidi idadi ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Waislamu wa nchini Uingereza

Kuhusiana na suala hilo, Haroon Khan, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Uingereza anasema: "Kwa mara nyingine Waislamu wa nchi nzima wanasisitiza kwamba kinyume na kile kinachoenezwa na vyombo vya habari, sisi ni jamii iliyo wazi na ya upendo." Alizidi kufafanua kwamba, mwaka jana zaidi ya watu elfu 10 walishiriki katika ratiba hiyo ya kufunguliwa misikiti. Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, karibu asilimia 90 ya raia wa Uingereza walikuwa hawajawahi kuingia msikitini. Kwa hakika hiyo ni fursa nzuri kwa ajili ya kuwapa elimu raia wengi wa nchi hiyo kupitia harakati za Waislamu ndani ya misikiti na kujibu maswali yao kwa namna ya moja kwa moja. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, karibu Waislamu milioni tatu, wanaishi nchini Uingereza wakiwa wanaunda asilimia tano ya jamii yote ya taifa hilo. Hali ikiwa hivyo, Uingereza ina jumla ya misikiti 1750 katika maeneo tofauti ya nchi.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 39 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./