Jumanne tarehe 24 Julai 2018
Leo ni Jumanne tarehe 10 Dhulqaada 1439 Hijria sawa na Julai 24, 2018.
Siku kama ya leo miaka 235 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela. Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia.
Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea pia hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru.
Miaka 216 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa. Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa ulihalalisha suala hilo.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita kikosi cha anga cha jeshi la Uingereza kiliishambulia vikali bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulizi ya anga ya Ujerumani na Uingereza yalianza mwanzoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na kushadidi zaidi baadaye. Kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi mbili hizo waliuawa katika mashambulizi hayo. Makumi ya maelfu ya raia wa kawaida waliuawa kwa umati katika mashambulizi ya kikosi cha anga cha Uingereza dhidi ya bandari ya Hamburg mbali na kuangamizwa taasisi kadhaa za kijeshi na kiuchumi.
Na siku kama ya leo miaka 55 iliyopita baada ya vyombo vya usalama vya Shah kumtia nguvuni Imam Ruhullah Khomeini maulamaa na marajii wa miji ya Qum na Mash'had hapa nchini na miji mingine ya Iran walielekea Tehran wakitaka kuachiwa huru Imam Khomeini. Harakati hiyo na malalamiko ya wananchi iliulazimisha utawala wa Shah kumtoa jela Imam Khomeini na kumhamishia katika nyumba moja. Hata hivyo Imam aliendelea kuwekwa katika kifungo cha nyumbani bila ya kuwa na mawasiliano yoyote ya watu wengine. Siasa hizo hazikuwa na taathira katika kutuliza malalamiko ya wananchi wala kuweka ufa baina ya kiongozi wa harakati za mapinduzi ya wananchi kwa msingi huo utawala wa Shah uliamua kumpeleka Imam Khomeini uhamishoni nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye akapelekwa Iraq.