Sep 17, 2018 02:24 UTC
  • Jumatatu,  17 Septemba, 2018

Leo ni Jumatatu tarehhe 7 Muharram 1440 Hijria sawa na 17 Septemba 2018.

Tarehe 7 Muharram mwaka 61 Hijria kamanda wa jeshi la Yazid bin Muawiya, Umar bin Sa'd aliliamuru jeshi lake kumzuia maji ya mto Furati Imam Hussein na watu waliokuwa katika msafara wake. Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kumzingira mjukuu wa Mtume (saw) akiwa na jeshi kubwa katika medani ya Karbala alimwandikia barua Umar bin Sa'd akimtaka amlazimishe Imam Hussein kutangaza utiifu wake kwa mtawala Yazid. Vilevile alimwandikia barua nyingine akimtaka kumzuia Imam Hussein na wafuasi wake wasitumie maji ya mto Furati. Imam Hussein, ndugu, watoto na masahaba zake waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka huo wakiwa na kiu tena kandokando ya mto Furati.

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, aliaga dunia Emil Ludwig mwandika wasifu wa Kijerumani. Alizaliwa 1881 katika mji wa Breslau nchini Ujerumani ambao leo hii ni sehemu ya ardhi ya Poland. Alipata umashuhuri katika nusu ya pili ya karne ya 19 baada ya kuandika wasifu wa Otto Van Bismarck Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, kiongozi wa zamani wa Russia Joseph Stalin, Beethoven na rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Ludwig alikuwa mwandishi wa habari aliyepata nafasi ya kufanya mahojiano na watawala waliokuwa na satua na ushawishi mkubwa katika kipindi hicho kama Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchil na Joseph Stalin. 

Emil Ludwig

Tarehe 17 Septemba miaka 57 iliyopita aliuawa waziri mkuu wa zamaji wa Uturuki, Adnan Menderes. Alizaliwa mwaka 1899 na kupata elimu katika taaluma ya sheria. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa bado kijana na alishika hatamu za uongozi nchini Uturuki kama waziri mkuu mwaka 1950. Menderes ambaye alikuwa akifuata siasa za sera za kimarekani, alituma vikosi vya jeshi kushambulia Wakurdi wa nchi hiyo, suala ambalo liliwakasirisha sana wasomi na wanafikra wengi nchini Uturuki. Mwaka 1957 alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Uturuki na kukandamiza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakipinga utawala wake na kudai marekebisho ya kisiasa. Mwaka 1960 Adnan Menderes aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kufikishwa mahakamani ambapo alihukumiwa kifo kwa kupatikana na hatia ya kuua wanafunzi wa vyuo vikuu, kukiuka katiba ya nchi na kuwa na mahusiano haramu. Usiku wa kutekelezwa hukumu ya kifo, Menderes alifanya jaribio la kujiua lakini madaktari waliwahi kuokoa maisha yake. Hatimaye tarehe 17 Septemba, Adnan Menderes alinyongwa akiwa na umri wa miaka 62.

Adnan Menderes

Tarehe 26 Shahrivar miaka 38 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, utawala wa zamani wa Iraq ulifuta kwa upande mmoja makubaliano ya mipaka ya mwaka 1975 yaliyojulikana kwa jina la Mkataba wa Algeria kati yake na Iran. Siku hiyo, Saddam Hussein kiongozi wa zamani wa Iraq aliuchana mkataba huo wa Algeria mbele ya kamera za televisheni akiungwa mkono na madola ya kibeberu. Siku kadhaa baadaye, Saddam Hussein alianzisha uvamizi wa miaka minane dhidi ya ardhi ya Iran.

 

Tags