Hadithi ya Uongofu (128)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala la kusalimia na kutoa salamu. Tulisema kuwa, kusalimia katika Uislamu ni jambo mustahabu, linalopendekezwa na la hiari.
Tulieleza kwamba, kusalimia na kutoa salamu ni haki miongoni mwa haki za Mwislamu kwa Mwislamu mwenziwe na jambo hili hupelekea kuusamehewa dhambi. Aidha tulibainisha kwamba, miongoni mwa mambo muhimu katika suala zima la kusalimia, maamkizi na kutoa salamu ni kutokuwa na ubaguzi katika kusalimia. Kuhusiana na maudhui hii tulinukuu hadithi kutoka kwa Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS inayosema: Endapo mtu hatamsalimia Mwislamu fakiri na masikini kama anavyomsalimia mtu tajiri na mwenye mali, Mwenyezi Mungu atamghadhibikia Siku ya Kiyama. Kadhalika tulieleza kwamba, miongoni mwa adabu njema za salamu ni kutoa jibu kamili zaidi la salamu au kwa uchache kujibu salamu kama ulivyosalimiwa. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 128 ya mfululizo huu kitaendelea na maudhui hii. Karibuni.
Kwa muujibu wa aya za Qur'ani Tukufu kusalimia na kutoa salamu ni nara na shaari ya mbinguni. Wakati mtu anapokata roho na roho yake kutengana na kiwiliwili, malaika wa mbinguni huwatolea salamu na kuwasailimia waja waumini. Salamu hii huondoa wasiwasi wote na ukosefu wa utulivu wa moyo. Wakati waja wema pia watakapokuwa wakiingia peponi kwa mara nyingine tena malaika watawatolea salamu wauumini kwa kusema:
Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyo subiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera.
Jabir al-Ju'ufi mmoja wa wapokezi wa hadithi na wafasiri wakubwa wa Qur'ani Tukufu ananukuu hadithi kutoka kwa Imam Muhammad al-Baqir AS ya kwamba amesema: Malaika miongoni mwa Malaika wa haki alipita sehemu moja na kumuona Bwana mmoja akiwa amesimama nje ya nyumba fulani kisha akamuuliza Bwana yule: Ewe mja wa Allah, kwa nini umesimama hapa? Bwana yule akajibu kwa kusema: Nimekuja hapa ili nimsalimie rafiki yangu muumini. Malaika akamuuliza, je kuna nasaba baina yako na yeye, ni mmoja kati ya ndugu na jamaa zako au una haja kutoka kwake? Bwana yule akajibu kwamba, Hapana, sina nasaba naye na wala sina shida na haja kutoka kwake. Akaendelea kusema, hakuna kitu kingine kilichonivuta mpaka hapa ghairi ya kuwa yeye ni ndugu yangu katika Uislamu na ninamheshimu. Sikufanya hili isipokuwa nimeona ni jambo la lazima kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu. Malaika yule akasema: Tambua kwamba, mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu kuja kwako na kukupatia salamu kutoka kwake na anasema kuwa, mja wangu amenizingatia na kufanya jambo hili kwa ajili yangu, hivyo basi nimemtunuku pepo na nimekuweka mbali na ghadhabu zangu na nimekuepusha na moto wa Jahanamu."
Wanadamu wote popote walipo katika kona ya dunia wanapokutana husalimiana na kuamkuana ili kuonyesha huba na upendo baina yao. Waislamu nao kwa upande wao wakiwa na lengo la kuvutia urafiki na udugu husalimiana na kutoleana salamu. Salamu kwa Waislamu ni muhimu mno kiasi kwamba, ni katika nembo rasmi za Waislamu ambapo husalimia pindi wanapokutana. Kwa maana kwamba, jambo la kwanza wanalolifanya Waislamu baada ya kukutana ni kusalimiana na kutoleana salamu ambayo ni mashuhuri kama "Assalaamu Alaykum".
Hata hivyo kuna nukta moja muhimu ya kuzingatia nayo ni kwamba, katika suala zima la kusalimiana na kutoleana salamu kama ilivyo ada na adabu yoyote ile katika Uislamu kuna haja ya kuchunga suala la uwiano na kati na kati. Kwa maana kwamba, katika kusalimia pia kuna haja ya kuchunga kutozembea na kutochupa mipaka.
Nukta hii ina maana kwamba, hata katika kusalimia Mwislamu anapaswa kujiepusha na uzembeaji na uchupaji mipaka. Uislamu unataka wakati mtu anaposalimia asalimie na kutoa maamkizi kwa heshima na adabu na kusiwe na hali ya ria, kujionyesha au kujikomba na kujipendekeza. Kuna watu wengine katika jamii kutokana na kukumbwa na maradhi ya kujionyesha au kutaka kujikomba kwa majirani zao wenye uwezo wa kifedha, mabosi wao au waajiri wao huwa na undumakuwili katika kusalimia. Yaani utawaona kwa watu wengine wakisalimia kwa unyenyekevu zaidi na kwa watu wengine wakisalimia kawaida sana au hata kwa uzembe na uvivu wa hali ya juu.
Nukta nyingine ni hii kwamba, katika kusalimia na kutoa salamu kuna wakati baadhi ya watu katika jamii hawasalimiwi kulingana na ustahiki wao wa kimaanawi. Yote mawili haya si yenye kufaa katika Uislamu. Yaani kusalimia kwa kujikomba na kikawaida na kuuosalimia kama inavyotakiwa. Katika mafundisho ya Uislamu kama maakizi na kutoa salamu yatakuwa na heshima ya kidhahiri na kutamka kwa ulimi tu na hilo kutokuwa na nafasi ya huba na upendo katika nyoyo za waumini, jambo hilo linahesabiwa kuwa ni nifaki na undumakuwili. Kwa hakika kama watu watapuuza maamkizi na kutotoa salamu kama inavyostahiki, watakuwa wamezembelea katika kutekeleza ada hii nzuri ya kidini na kijamii ambayo ni chimbuko la huba na upendo n ahata maelewano baina ya wanajamii. Ndio maana tunaona kuwa, kunapojitokeza hasama na ugomvi baina ya watu wawili jambo la kwanza ambalo hujitokeza baina yao ni kutosalimiana. Imamu Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Katika kuwasalimia ndugu zako (katika dini) usifanye hivyo katika kiwango cha ria na kujionyesha na wala usizembee kwa mujibu wanavyostahiki.
Kwa hakika mtu ambaye ana hali ya kati na kati na uwiano hujiona kama alivyo. Kwa maana kwamba, hajioni kama ni mtu wa daraja ya juu wala daraja ya chini. Mtu wa aina hii, katu hawezi kujitengenezea shakhsia ya uwongo na hivyo kujiona kuwa yuko juu zaidi ya wengine. Mtu wa aina hii hufanya urafiki na watu wa aina yake tena kwa huba na upendo wa hali ya juu na huwa na hamu na shauku kubwa ya kukutana nao. Ndio maana mtu wa aina hii hawezi kukumbwa na maradhi ya kiburi na kujiona au kujikweza.
Imamu Ja'afar bin Muhammad Swadiq AS amenukuliwa akisema: Katika ishara za unyenyekevu ni kumsalimia kila unaekutana naye.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kukusomeeni aya ya 56 ya Surat al-Ah'zab ambayo inawataka waumini wamswalie na kumsalimia Mtume SAW. Aya hiyo inasema:
Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo siku na wakati kama wa leo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh….