Jumamosi, 17 Novemba, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 17 Novemba 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1180 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (AF). Imam Mahdi ni mwana wa Imam Hassan Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu. Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo". Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi, na mafakihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wacha-Mungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma. Kwa mujibu wa hadithi tukufu za Mtume (saw), Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu. ***

Miaka 301 iliyopita katika siku kama ya leo, Jean le Rond d'Alembert mwanahisabati wa Kifaransa alizaliwa katika mji wa Paris huko Ufaransa. Baba na mama yake walimtelekeza kando ya kanisa moja mjini Paris akiwa mtoto mchanga. Aliokotwa na kulelewa na mwanamke na mwanaume mmoja waliokuwa wauza vioo. Jean le Rond d'Alembert alisoma kwa bidi na baada ya kuhitimu masomo ya katialianza kusoma taaluma ya tiba na sharia. Hata hivyo baada ya muda aliondokea kuipenda mno taaluma ya hisabati ***

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, Catherine the Great malkia mashuhuri wa Russia aliaga dunia. Alizaliwa Mei Pili 1729 na akiwa na umri wa miaka 15 aliolewa na Peter III. Hata hivyo Peter III mfalme wa wakati huo wa Russia hakuwa akimpenda mkewe huyo na alikuwa akimvunjia heshima na kumdhalilisha mbele za watu. Mwaka 1762 wakati Peter III alipokuwa ametoka nje ya mji, Catherine the Great alijitangaza kuwa malkia wa Russia. Peter III ambaye alikuwa ameshtushwa na kupata pigo kwa hatua hiyo alilazimika kujiuzulu pasina ya mapambano na baada ya siku chache akaaga dunia. ***

Miaka 160 iliyopita katika siku kama ya leo, Robert Owen mpigania mageuzi ya kisoshalisti wa Wales na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Usoshalisti aliaga dunia. Alianza harakati zake tangu akiwa na umri wa miaka 18. ***

Katika siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, mfereji wa Suez ambao unauinganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu ulifunguliwa. Mfereji huo wenye urefu wa kilometa 167 na upana wa mita 120 hadi 200 ulichimbwa chini ya usimamizi wa mhandisi wa Ufaransa, Ferdinand de Lesseps. Mfereji wa Suezi pia unahesabiwa kuwa ni mpaka kati ya bara la Asia na bara la Afrika. ***

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Libya ulianza tena. Uhusiano huo ulikuwa umekatika kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Hilo lilitokana na hatua ya Kanali Muammar Gaddafi Kiongozi wa wakati huo wa Libya ambaye alikuwa akiutambuia utawala wa kifalme wa Kipahlavi hapa nchini kwamba, unafungamana na ubeberu wa Marekani ambao ulikuwa ukitanguliza mbele maslahi na manufaa ya Magharibi na utawala vamizi wa Israel mbele ya maslahi ya nchi za Kiarabu na Wapalestina. ***

Na miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq liliasisiwa kutokana na vyama na makundi mbalimbali yaliyokuwa yakiupinga utawala wa dikteta Saddam Hussein. Lengo la kuasisiwa baraza hilo lilikuwa ni kuwaokoa wananchi wa Iraq na dhulma pamoja na ukandamizaji wa utawala wa Chama cha Baath. Kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kuangushwa utawala dhalimu wa Saddam, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq, lilihamishia harakati zake za kisiasa ndani ya ardhi ya Iraq na kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo.
